Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yajifungia kuisoma Galaxy

FBBlfuiUcAADxKx Wachezaji wa Simba Inonga, Morisson

Sat, 9 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

Mchezo wa hatua ya kwanza ya ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy utapigwa Oktoba 17 katika Uwanja wa Taifa wa Botswana, awali mchezo huo ulipangwa kucheza kati ya Oktoba 14 na 15 nchini humo.

Benchi la ufundi la Simba linaloongozwa na Kocha Mkuu Didier Gomes akisaidiwa na Thierry Hitimana na Seleman Matola, tayari wameashaanza kupata baadhi ya majina ya nyota wa Jwaneng Galaxy ambao ni Bertrand ambaye ni usajili mpya kutoka Rwanda katika klabu ya Gasoline United na Gape Mohutsiwa.

Kocha Msaidizi wa Simba, Hitimana alisema wameanza kuwafuatilia wapinzani wao licha ya kuangalia michezo ya nyuma kuanzia Februari ambapo walikuwa kwenye ligi na michuano hiyo ya hatua za awali.

Amesema hatua hiyo ni baada ya kuchelewa kuanza kwa ligi ya Botswana hali iliyopelekea kukosa mechi nyingi za wapinzani hao.

"Tumeanza kuwafuatilia licha ya wenzetu ligi yao imechelewa kuanza, tunatumia mechi za hivi karibuni pamoja na taarifa za wachezaji wao ikiwemo usajili waliofanya kwa mchezaji kutoka Rwanda," amesema Kocha huyo.

Alisema wanatambua umuhimu wa mechi hiyo pamoja na ushindani wao na kuhakikisha kutumia vizuri ya kalenda ya FIFA na wachezaji waliobaki kufanya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Jwaneng Galaxy.

“Hawa waliobaki katika timu tutaanza nao mazoezi mepesi, kisha baada ya hapo tutakwenda kwenye mbinu ambayo na wale waliokuwa timu za taifa wataungana na wenzao katika hili,” amesema.

“Baada ya hapo tutakuwa na muda mwingi wa awamu ya kuangalia mechi za Galaxy - zile za mashindano ya kwao na mchezo wa hatua ya kwanza waliocheza kisha kufahamu ubora na upungufu waliokuwa nayo," amesema kocha huyo.

Amesema kutokana na mipango waliyonayo kwa wachezaji na mbinu wanazofanya kipindi hiki, wana matarajio makubwa ya kwenda kufanya vizuri katika michezo yote miwili ya ugenini na nyumbani dhidi ya Watswana hao na kufuzu kucheza makundi.

Chanzo: ippmedia.com