Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yaipiga bao AS Vita

As Vita Pic Data Simba yaipiga bao AS Vita

Thu, 25 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

SIMBA imepokea habari njema kuhusu wachezaji wao walioitwa kwenye timu zao za Taifa juu ya uwezekano wao wa kuwahi haraka nchini kwa ajili ya mechi dhidi ya AS Vita, lakini wakati hali ikiwa hivyo kwao mambo huenda yasiwe mazuri kwa wapinzani wao.

Awali Simba ilikuwa na wasiwasi huenda baadhi ya wachezaji wake muhimu na tegemeo wa kikosi cha kwanza waliopo kwenye timu zao za taifa wakachelewa kurejea nchini kufanya maandalizi au kucheza mechi hiyo ya raundi ya tano ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita iliyopangwa kuchezwa mwanzoni mwa Aprili lakini juhudi za uongozi wake zimewapa uhakika wa kuwapata karibia wachezaji wote kwa wakati.

Wasiwasi huo wa Simba ulisababisha uongozi wa Simba kuandika rasmi barua kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kuomba mechi hiyo ambayo awali ilipangwa kuchezwa katika Uwanja wa Mkapa, Aprili 2 isogezwe hadi Aprili 4 lakini shirikisho hilo lilikubaliana kidogo na maombi hayo kwa kupanga mechi hiyo ichezwe Jumamosi, Aprili 3.

Lakini wakati huohuo juhudi zao za kuwapata wachezaji wao mapema, umefanikiwa baada ya kuhakikishiwa na vyama na mashirikisho ya soka kwenye nchi zao, kurejea kwao muda mfupi baada ya majukumu hayo

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema ukiondoa Meddie Kagere ambaye ndiye atachelewa na anatarajiwa kuwasili nchini Aprili 2, wengine 17 watakuwa wamejiunga na kikosi kabla ya Aprili Mosi.

“Hadi kufikia Aprili Mosi, asilimia 99 ya wachezaji wote waliopo katika timu zao za taifa watakuwa wamejiunga na kikosi ukiondoa Kagere (Meddie) ambaye ataingia Aprili 2 lakini wengi watafika kabla ya hapo na angalau watapata muda wa kufanya mazoezi ya pamoja kujiandaa na mechi hiyo.

Tungependa wapate muda zaidi lakini ndio hivyo ratiba imepangwa na kama kuathirika hata wapinzani wetu nao wataathirika. Jambo kubwa ambalo tunaamini ni kwamba wachezaji wetu wamepevuka na wana ubora wa kuwafanya wacheze mechi hiyo bila tatizo lolote hata kama watafanya maandalizi kwa muda mfupi.

Kwanza ikumbukwe mechi ilipangwa kuchezwa Aprili 2 lakini wenye mashindano yao wakaona kama walikosea wakaamua kuisogeza hadi Aprili 3 sasa ni lazima tucheze kwa sababu hata wakiisogeza tena bado tuna mechi kule Misri dhidi ya Al Ahly Aprili 9 hivyo tungelazimika kwenda mapema,” alisema Rweyemamu.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo alilithibitishia Mwanaspoti mechi hiyo itachezwa Aprili 3 na sio 2 kama ratiba ya mwanzo ya CAF ilivyokuwa inaonyesha.

“Ninachofahamu, mechi itachezwa Aprili 3 na sio Aprili 2,” alisema Ndimbo.

Lakini wakati Simba ikiwa na uhakika wa kuwapata wachezaji wake mapema, athari kubwa inaonekana upande wa AS Vita ambao huenda wachezaji wao saba (7) wakachelewa kufika nchini kuungana katika maandalizi ya mechi hiyo kutokana na changamoto ya usafiri wa kutoka maeneo ambako timu zao za taifa zitacheza mechi kuja hapa nchini na ratiba ya muda wa mechi ambazo timu zao za taifa zitacheza.

Ratiba inaonekana angalau itakuwa rafiki kwa Simba kwani wachezaji wake 10 waliopo Taifa Stars, hawatakumbana na adha ya usafiri kwani timu hiyo ya taifa ya Tanzania mechi yake ya mwisho itaikaribisha Libya nyumbani, Machi 29.

“Kwa bahati nzuri tuna wachezaji 10 kwenye kikosi cha Stars ambayo itacheza mechi ya mwisho hapa nyumbani hivyo wao watawahi mapema zaidi,” alisema Rweyemamu.

Mazingira rafiki ya usafiri, yanawapa uhakika nyota wengine sita wa Simba ambao watakuwa na majukumu ya kutumikia timu zao za taifa ambao ni Peter Muduhwa (Zimbabwe), Clatous Chama na Rally Bwalya (Zambia) Luis Miquissone (Msumbiji) na Lwanga Taddeo (Uganda).

Muduhwa atakuwa katika kikosi cha Zimbabwe kitakachokikabili nyumbani timu ya taifa ya Zambia yenye wachezaji nyota wa Simba kama Chama na Bwalya siku ya Machi 29, wakati Lwanga atakuwa ugenini na kikosi cha Uganda kitakachoikabili Malawi, siku hiyo hiyo.

Pia winga Luis naye ana nafasi kubwa ya kuwahi nchini kwani timu yake ya taifa ya Msumbiji, itacheza mechi yake ya mwisho nyumbani dhidi ya Cape Verde, Machi 29.

Mchezaji mwingine aliyekuwa akiipa wasiwasi Simba, ni Joash Onyango ambaye yupo kikosi cha Kenya lakini habari njema zaidi ni kwamba mechi ya mwisho ambayo Kenya walikuwa wacheze ugenini dhidi ya Togo, Machi 30 imerudishwa nyuma hadi Machi 29.

Kwa upande wa AS Vita wao wana wakati mgumu zaidi kwani wachezaji wake saba watakuwa na muda mfupi wa kuungana na kikosi chao hapa Dar es Salaam baada ya mechi zao za mwisho za timu zao za Taifa.

Nyota wanne wa Vita, Shaban Djuma, Luzolo Sita, Mumbere Jeremie na Glody Makabi waliopo katika kikosi cha DR Congo, watakuwa na mchezo nyumbani dhidi ya Gambia utakaochezwa Machi 30.

Kipa Simon Omossola ataingia nchini Aprili 2 kama Kagere kwani yumo katika kikosi cha Cameroon kitakachoivaa Rwanda nyumbani, Machi 30.

Kiungo wa Ivory Coast, Ousmane Outtara atakuwa na majukumu na timu yake ya taifa itakayocheza nyumbani dhidi ya Ethiopia, Machi 30 huku kiungo wa Mauritania, Sidi Yacoub timu yake ya taifa itakuwa ugenini kucheza na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Machi 30.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz