Mabao matatu ( hat-trick) aliyofunga kiungo wa Simba, Sadio Kanoute juzi usiku katika ushindi wa mabao 6-0 kwenye mechi ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya TRA ya Kilimanjaro, umeifanya timu hiyo kufunika kwa kufikisha nyota watatu waliondoka na mpira tofauti na Yanga katika misimu miwili mfululizo ya michuano hiyo.
Katika mchezo huo wa uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam umemfanya Kanoute kufikisha idadi ya wachezaji saba waliofunga ‘hat-trick’ msimu huu sawa na msimu uliopita, ingawa bado rekodi hiyo inaweza kuvunjwa baada ya kufikiwa kwa sasa.
Msimu uliopita, Simba iliongoza kwa kutoa wachezaji wawili waliofunga ‘hat-trick’ ambao ni Moses Phiri aliyefunga mabao manne wakati timu hiyo ikishinda 8-0, dhidi ya Eagle FC na Jean Baleke wakati kikosi hicho kikishinda 5-1, kwa Ihefu.
Nyota hao wawili kwa sasa hawapo Simba baada ya kuondoka dirisha la usajili la Januari mwaka huu na kufikia idadi ya watatu.
Kwa Yanga ni Clement Mzize tu, aliyefanya hivyo kwa misimu miwili mfululizo akifunga mabao manne katika ushindi wa 8-0 dhidi ya Kurugenzi FC huku kwa msimu huu akifunga tena wakati mabingwa hao watetezi wakishinda 5-1, mbele ya Hausung FC.
Wachezaji wengine kwa msimu huu waliopiga hat- trick ni pamoja na Edward Songo wa JKT Tanzania, Kelvin Sabato na Pascal Wagana, huku timu 16 zimeshatinga hatua inayofuata na watetezi Yanga itavaana na Dodoma Jiji, wakati Simba ikicheza na Mashujaa, Azam FC itacheza na Mtibwa Sugar.