Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amefunguka kuhusu hali ya afya ya winga wao, Aubin Kramo raia wa Ivory Coast ambaye amekuwa akizua maswali na sintofahamu kuhusu afya yake.
Ahmed amekiri kuwa mchezaji huyo aliumia kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Ngoime FC juzi hivyo wanasubiri ripoti ya daktari ili kujua atakaa nje kwa muda gani na matibabu yake yatafanyikaje.
"Ni kweli Aubin Kramo wakati anafunga bao dhidi ya Ngome aliumia , akashindwa kuendelea na mchezo akatolewa na nafasi yake ikachukuliwa na Jean Baleke, tunasubiri taarifa ya madaktari tujue ameumia kiasi gani na atakaa nje ya Uwanja kwa muda upi," amesema Ahmed.
Majeraha haya ya Kramo yanakuja siku chache tu tangu arejee kambini baada ya kukaa nje kwa muda mrefu tangu asajiliwe na Simba msimu huu akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.