Klabu ya Simba imesema kuwa inakamilisha mambo kadhaa ili kumalizana na winga wake, Peter banda raia wa Malawi ambaye anatajwa kuondoka kikosini hapo.
Hayo yamesemwa na Meneja Habari wa Simba Sc, Ahmed Ally wakati akizungumza na Wasafi TV kufuatia sintofahamu kuhusu hatima ya mchezaji huyo ndani ya Msimbazi.
Banda ambaye alijiunga na Simba msimu wa mwaka 2021/22 amelazimika kuachana na Simba msimu huu kumpisha kipa mpya kutoka Morocco, Ayoub Lakred.
“Taarifa kuhusu Peter Banda itatoka muda si mrefu, ndani ya wiki hii itawekwa hadharani, kwa sasa tuwe na subira kidogo, yapo mambo ambayo yanamalizika, ikishakuwa sawaswa basi jambo litakuwa hadharani," amesema Ahmed.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa kulikuwa na mvutano mkali kati ya mchezaji huyo na mabosi wa Simba ambao walitaka wamtoe kwa mkopo huku yeye akitaka aachiwe huru ili akatafute changamoto nyingine nje lakini mazungumzo tayari yapo hatua za mwisho.