Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yafuata mbadala wa Ayoub Lakred

Kamala 579394 Golikipa wa Horoya FC Moussa Camara.

Sun, 28 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Simba imetajwa kuwa kwenye mazungumzo na Horoya FC ya nchini Guinea kwa ajili ya kumsajili golikipa wa timu hiyo Moussa Camara anayeichezea pia timu ya taifa hilo ili kuziba nafasi ya Ayoub Lakred ambaye ameumia mazoezini na kutarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa angalau wiki nne mpaka sita.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa Simba inataka dili hilo likamilike kabla ya kilele cha tamasha lao la kila mwaka la 'Simba Day' Agosti 3, ili kipa huyo mwenye miaka 25, awe mmoja wa wachezaji watakaotambulishwa.

Mtoa taarifa amesema kuwa ingewezekana kumsubiri Ayoub, lakini inaona mechi nyingi muhimu ambazo ni za Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Tanzania na mechi za hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitachezwa mapema zaidi na haitaki kufanya makosa kama ya msimu uliopita ya kusubiri wachezaji wapone au wawe fiti.

"Ukweli ni kwamba Ayoub hayupo fiti kudaka kwa siku za hivi karibuni, kwanza licha ya kuumia na madaktari kusema anaweza kupona baada ya wiki nne mpaka sita, lakini ameongezeka sana uzito, kutokana na hilo hata kama atarudi ndani ya muda huo bado hatokuwa fiti, kwa sababu anatakiwa aanze tena mazoezi kwa ajili ya kujiweka fiti, kimahesabu anaweza kukaa hata miezi miwili, watu hawawezi kusubiri hilo kwa sababu tuna michuano mingi mikubwa na muhimu ambayo tunatakiwa tuanze vizuri ", alisema mtoa taarifa ndani ya Simba.

Inaelezwa iwapo dili hilo litafanikiwa, Simba inaweza kukata jina la Ayoub kwenye usajili wa Ligi Kuu na nafasi yake kuchukuliwa na Camara kwa sababu kanuni inataka wachezaji wa kigeni 12 tu, lakini likiachwa katika mechi ya kimataifa hadi kipindi cha dirisha dogo watakapoamua vinginevyo.

Kama Camara atafanikiwa kutua nchini atakuwa kipa wa pili kusajiliwa nchini kutoka Horoya ya Guinea kwani tayari klabu ya Singida Black Stars imemsajili golikipa Mohamed Kamara kutoka klabu hiyo hiyo.

Tofauti yao ni kwamba kipa wa Singida Black Stars anaichezea timu ya taifa ya Sierra Leone na wa Simba yuko kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Guinea.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema pamoja na kuwatambulisha wachezaji wapya, lakini bado hawajamaliza usajili, hivyo chochote kinaweza kutokea.

Aliwataka wanachama na mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha la kilele cha Simba Day kwani kuna 'sapraizi' za nguvu.

"Sisi hatujamaliza, chochote kinaweza kutokea wakati wowote kwa hiyo nawataka wanachama na mashabiki wa Simba wajitokeze Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya burudani, soka na pia kuwaona wachezaji wao wapya waliosajiliwa, na wanaweza kupata 'sapraizi' nyingine ya mchezaji ambao hawajamsikia kabisa," alisema Ahmed.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live