Mwenyekiti wa Kamati ya Maboresho ya Katiba ya klabu ya Simba, Hussein Kitta amesema wanachama wamepitisha mambo sita waliyotakiwa kufanyia maboresho huku suala la uwakilishi wa mwanachama likigonga mwamba.
Alisema katika mambo hayo wanachama wamekataa kupitisha kipengele kimoja kinachoeleza kutoa mwakilishi wa mwanachama katika mkutano mkuu. "Hicho kipengele tuliambiwa tukiweke kulingana na namna ya kuendesha mikutano yetu, lakini wanachama wamekikataa, kutokana na hilo ni sehemu ya mapendekezo tu tuliopewa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT ) ambayo haikuwa na ulazima," alisema Kitta.
Mjumbe wa bodi ya ushauri wa klabu ya Simba, Geofrey Kaburu amempongeza mwenyekiti wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu kwa kuendesha mkutano vizuri na kufuata matakwa ya wanachama.
Mangungu alisema mkutano ulikuwa mfupi wenye ajenda nzuri zilizo na mafanikio kwa klabu huku akikisisitiza kuwa katiba ni jambo mtambuka na ni mahitaji ya wanachama hivyo kupewa nafasi ya kusikilizwa ni jambo zuri.
“Pia Baraza letu limeingizwa kwenye katiba ya klabu hivyo tutakuwa tunashauri kwa mujibu wa katiba kwasababu tayari tunatambulika;
“Mbali na sisi kutambulika kikatiba rasmi mwenyekiti wa klabu kapewa nafasi maalum kwa mujibu wa katiba kusimama kwa ajili ya wanachama,” alisema.