Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yabariki Barbara kusepa, yaanza kutafuta mrithi wake

Barbara Mk.jpeg Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez

Mon, 12 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Uongozi wa Klabu ya Simba umeridhia uamuzi wa kujiuzulu kwa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez na umeanza mchakato wa kutafuta mbadala wake.

Barbara ataondoka rasmi kwenye Simba ifikapo Januari mwakani 2023, na tayari amewasilisha barua ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’.

Barbara alitoa taarifao mwishoni mwa wiki iliyopita kupitia akaunti yake ya Instagram, akitaja sababu kuu mbili za kujiuzulu kwake.

Amesema uamuzi wake wa kujiuzulu ni kutoa nafasi kwa uteuzi wa mtendaji mkuu mpya wa klabu hiyo, ambaye ataendeleza maono ya klabu.

Barbara pia alisema alitaka kufuata masilahi sehemu nyingine.

Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salim Abdallah 'Try Again' aliliambia Mwananchi ambalo ni gazeti mama la Mwanaspoti jana Jumapili kuwa, bodi imeridhia kujiuzulu kwa Barbara na inamtakia kila la kheri.

Alisema bodi hiyo itakutana hivi karibuni na kuanza mchakato wa awali katika kujaza nafasi hiyo iliyoachwa wazi.

“Tumeridhia uamuzi wake na taratibu nyingine zitafuata ikiwa ni pamoja na kukabidhi ofisi kwa taratibu zilizowekwa.

“Sasa tuna jukumu ambalo ni kutafuta Mkurugenzi Mtendaji mpya. Tutakutana muda kwa muda mfupi wiki ijayo kujadili suala hilo na masuala mengine yanayohusu klabu,” Abdallah alisema.

Aliongeza kuwa bodi hiyo inamshukuru Barbara kwa kujitolea kwake wakati akiwa madarakani, ambapo amekuwa na mchango mkubwa katika kuifanya Simba kuwa na nguvu katika soka la klabu Afrika.

"Amefanya mengi kwa klabu yetu na atakumbukwa sana. Tunatumaini ataendelea kuisaidia klabu na kutoa ushauri hata baada ya kuacha wadhifa huo,” alisema Abdallah.

Barbara aliwashukuru wote walioshiriki kuifanya Simba kuwa klabu kubwa. Alisema klabu hiyo ilipata mafanikio makubwa ndani na nje ya uwanja wakati alipokuwa katika nafasi hiyo, ikiwa ni pamoja na kushinda mataji, kuvutia udhamini, na kutambulika kama moja ya vilabu vikubwa vya barani Afrika.

Barbara alisema haikuwa rahisi kwake kufikia uamuzi wa kujiuzulu kama mtendaji mkuu.

"Ni vigumu kujiuzulu kutoka kwa kazi ambayo umekuwa ukifanya kwa kujitolea, lakini mambo yote mazuri hatimaye yamefikia mwisho," alisema.

Barbara aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Simba mwaka 2020 kuchukua nafasi ya Senzo Mazingiza ambaye ni raia wa Afrika Kusini aliyejiuzulu na kujiunga na wapinzani wao Klabu ya Yanga.

Hata hivyo, Mazingiza aliachana na Yanga mapema mwaka huu na kurejea Afrika Kusini.

Chanzo: Mwanaspoti