Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba ya sasa kama upepo wa kisulisuli

80971 Simba+pic Simba ya sasa kama upepo wa kisulisuli

Mon, 21 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

HUKO mtaani kwa sasa Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa Moto, Dk Getrude Rwakatare ndio habari ya mjini baada ya video ya mahubiri yake kusambaa ikiutaja upeo wa kisulisuli, ambao maana yake ni upepo unaosafiri na kuzunguka na kwenda kwa kasi au kwa haraka, yaani kimbunga. Sasa achana na hiyo unaambiwa Simba ya sasa haina tofauti na kimbunga kwa namna ilivyo na kikosi bora.

Haya sio maneno ya Mwanaspoti, ila yametolewa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems aliyesema kwa namna kikosi chake kilivyo, anaona ana nafasi nzuri ya kufanya vyema mbele ya Azam watakaovaana nao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Jumatano ijayo, jijini Dar es Salaam.

Aussems amesema viwango walivyoonyesha wachezaji hao ambao hawakuwa wanapata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza kimemfanya aumize kichwa kwenye upangaji wa kikosi kutokana na kila mmoja kuonekana bora.

Amesema hakuwa anaangalia matokeo katika mechi tatu za kirafiki ambazo wamecheza, bali alikuwa anaangalia jinsi gani wachezaji wake watatumika kwa vile ambavyo walikuwa wanavifanyia kazi katika mazoezi ili kuimarika katika mechi za ligi.

“Ukiangalia viwango ambavyo wameonyesha Ibrahim Ajibu, Benno Kakolanya, Yusuph Mlipili, Rashid Juma na Haruna Shamte vinashawishi kuwapa nafasi ya kucheza kwenye mechi zinazofuata jambo ambalo nilikuwa nataka kuliona kutoka kwao licha ya kwamba hawakupata nafasi ya kucheza mara kwa mara,” alisema.

“Naona nitakuwa na wakati mgumu pindi wachezaji waliokuwa katika majukumu ya timu za taifa, kwani ushindani utakuwa mkubwa jambo ambalo nitalazimika kumuweka nje mchezaji aliyekuwa na uwezo wa kucheza, lakini jambo hili ni zuri kwetu benchi la ufundi kwani kila mchezaji akipata nafasi atakuwa anatumika kweli ili asiachie nafasi hiyo kwa mwingine.”

Pia Soma

Advertisement
Alisema, “mbali ya viwango ambavyo wameonyesha wachezaji hao, tumerudi Dar es Salaam kufanya maandalizi ya kutosha kuelekea katika mchezo wa ligi unaofuata ambao tunacheza dhidi ya Azam, na kwa jinsi timu yangu nilivyoiona tunaweza kuondoka na ushindi kwenye mechi hiyo kwani hayo ndio malengo yetu.

“Kukosekana kwa karibu wachezaji wanane waliopo kwenye majukumu ya timu za taifa huenda ikawa imeathiri maandalizi yetu kwani hao wote waliondoka ni kikosi cha kwanza, lakini viwango walivyoonyesha waliobaki kwenye timu wakija kuungana na wenzao nadhani mambo yatakwenda vizuri kwani inadhihirisha Simba ina kikosi kipana.”

Aussems alisema hayo mara baada ya kikosi chake kutua Dar kutokea Kigoma ambapo walitoka kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Mashujaa na Aigle Noir kutokea Burundi.

SHIBOUB, AJIBU WAMKUNA

Katika hatua nyingine Aussems ameshindwa kujizuia kwa kiungo Msudan Sharafeldin Shiboub kutokana na kiwango ambacho ameonyesha katika michezo mitatu ya kirafiki ambayo wamecheza katika kipindi hiki ligi ikiwa imesimama.

Amesema mchezaji huyo licha ya kumtumia kwenye kikosi cha kwanza mara kwa mara, lakini amekuwa hachagui aina ya mechi kwani amekuwa akicheza katika kiwango cha juu - uwe mchezo wa kimashindano au kirafiki bila kujali aina ya viwanja, kitu ambacho kwake anaona ni faida ya kuwa na nyota wa aina hiyo.

“Mara nyingi wachezaji wa kigeni wamekuwa hata wakishindwa kutumia viwanja vya mikoani, lakini kwa Shiboub ameonyesha hana kuchagua aina ya mechi kwani amecheza katika kiwango kilekile kwenye mechi za zote,” alisema.

Shiboub ni miongoni mwa wachezaji saba wa kigeni waliosajiliwa msimu huu na kikosi cha Simba akitokea katika klabu ya Al Hilal ya nchini Sudan.

Chanzo: mwananchi.co.tz