Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba ya msimu huu weka mbali na watoto

Simba Sc Usajili Simba ya msimu huu weka mbali na watoto

Thu, 11 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba imeamua. Baada ya misimu mitatu ya unyonge katika Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA), Wekundu wa Msimbazi wamezinduka na kufanya usajili wa kibabe.

Ikiwa na hasira ya kutolewa kinyonge na Mashujaa, kisha kumaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu na kujikuta kwa mara ya kwanza ndani ya misimu sita, timu hiyo hiyo imeshindwa kufuzu ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Huenda hilo na kelele za Yanga ambayo iliifumua jumla ya mabao 7-2 katika Dabi ya Kariakoo, ndivyo vilivyomfanya bilionea wa klabu hiyo, Mohamed Dewji kuingia kikamilifu kusimamia usajili wa timu na hii ndio Simba mpya.

Imeshusha benchi la ufundi jipya kutoka Sauzi lenye vichwa vitano, kisha imeleta mashine mpya nane za kigeni, kuonyesha msimu ujao wapinzani lazima wajipange.

Tuanzie na benchi. Lina sura ngeni na vijana haswa, kulinganisha na makocha wawili waliotangulia akiwamo Roberto Oliveira na Abdelhak Benchikha, pia hata wachezaji wanaounda kikosi hicho wastani wao ni miaka 22 ikiwa ni moja ya timu yenye wachezaji vijana zaidi.

BENCHI LA UFUNDI Simba dilisha hili limefanya mapinduzi kwenye eneo la benchi la ufundi kwa kumbakiza Seleman Matola pekee huku wakishusha makocha wanne kwenye maeneo mbalimbali. Matola ndiye kocha mwenye umri mkubwa pia kulinganisha na wenzake waliopo kwa sasa, akiwa na miaka 46.

Kocha mkuu, Fadlu Davids ana umri wa miaka 43 tu na amefanya kazi na makocha wengi wenye uzoefu mkubwa akiwa Raja Casablanca. Kocha huyo anachukua nafasi ya Benchikha aliyeondoka mwishoni mwa msimu na kuiacha timu mikononi kwa Juma Mgunda aliyemaliza mkataba Msimbazi.

Fadlu ametua na wasaidizi wanne akiwamo Darian Wilken (29), Wayne Sandilands (40) anayenoa makipa, kuna mtathmini wa video, Mueez Kajee anayetajwa kuwa na umri usiofika miaka 38 na kocha wa viungo, Riedoh Berdien (42).

Makocha hao wapya wakiungana na Matola wanachukua nafasi zilizoachwa wazi na Benchikha aliyeondoka na wasaidizi wawili, Kamal Boujnane na Farid Zemit, sambamba na Dani Cadena aliyekuwa akiwanoa makipa na Culvin Mavunga aliyekuwa mtathmini wa video kutokea Zimbabwe.

MAKIPA Eneo hili Simba haijafanya usajili ni wazi kuwa wataendelea na makipa wao wa msimu uliopita ambao ni Ayoub Lakred, Aishi Manula ambaye anatajwa kutua Azam FC kwa mkopo, Ally Salim, Ahmed Feruzi na Hussein Abel.

Kati ya makipa hao watano Lakred ndiye kipa namba moja baada ya Manula kutupwa benchi tangu alipopata jeraha la nyonga akikaa nje ya uwanja kwa muda mrefu. MABEKI

Eneo hili Simba limefanya maboresho kwa kuongeza wachezaji wapya kila hadi beki namba mbili ambayo tayari ina Shomari Kapombe, David Kameta ‘Duchu’ na Israel Mwenda ambao wataendelea kubaki ndani ya timu hiyo. Simba pia imemsajili Kelvin Kijiri anayeenda kusimama eneo hilo kutokana na taarifa kwamba Mwenda amesaini pia Singida Black Stars.

Eneo la beki namba tatu ambalo lilikuwa bora chini ya nahodha msaidizi Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye anarekodi nzuri kwa kucheza misimu minne mfululizo kwa ubora ule ule ameongezewa nguvu baada ya kufanya usajili wa Valentin Nouma (24) akitokea timu ya St. Eloi Lupopo ya DR Congo.

Beki ya kati ambayo ilikuwa bora chini ya Henock Inonga na Che Malone Fondoh imeongezwa nguvu baada ya kufanya biashara ya Inonga kwenda FAR Rabat ya Morocco na kuwamsajili Chamou Karaboue ili kuziba pengo hilo, pia Simba imemsajili mzawa Abdulrazack Mohamed Hamza (23) akitokea Supersport United ya Sauzi samba na kuwepo kwa Hussein Kazi ambaye hata hivyo inaelezwa huenda akapelekwa kwa mkopo Singida Black Stars dili ambalo bado halijakamilika.

KIUNGO Eneo hili Simba haijataka kufanya masihala mara baada ya kuondoka kwa Said Ntibazonkiza ‘Saido’, Luis Miquissone, Sadio Kanoute na Clatous Chama ambao mikataba yao iliisha, imefanya usajili wa wachezaji wa watano, wanne wa kigeni na mmoja mzawa ambao tayari hadi sasa imewatambulisha.

Ilianza na Joshua Mutale (22), Augustine Okajepha (20), Debora Mavambo (24), Jean Charles Ahoua (22) na Yusuf Kagoma (28) ambao wote wanacheza eneo la kiungo hivyo ni wazi wamejipanga kutengeneza timu kwenye maeneo yote, mbali na ongezeko hilo pia Simba bado ina Mzamiru Yassin na Fabrice Ngoma ambao wataendelea kubaki ndani ya kikosi hicho baada ya kufanya vizuri msimu ulioisha.

Kuna wazawa wawili wapya pia walioongezwa katika eneo hilo akiwamo Awesu Awesu aliyekuwa KMC na Omary Omary kutoka Mashujaa, hivyo kulifanya eneo hilo la kiungo kuwa na vichwa vya kutosha kwa sasa.

STRAIKA Eneo la ushambuliaji ambalo limekuwa likifanyiwa maboresho mara kwa mara baada ya kuondoka kwa Moses Phiri na Jean Baleke, Simba imefanya usajili wa mchezaji mmoja tu ambaye ni Steven Mukwala ambaye ametoka Asante Kotoko ya Ghana.

Mshambuliaji huyo msimu ulioisha akiwa Kotoko ameifungia timu yake mabao 14 na kutoa pasi mbili zilizozaa mabao kwenye mechi 28 za ligi, anaungana na Kibu Denis eneo hilo ambaye ameongeza mkataba wa miaka miwili pamoja na Freddy Michael ambaye amesalia kikosini baada ya kutua katika dirisha dogo lililopita.

Katika nusu msimu alioitumikia Simba, Freddy amefunga mabao sita katika Ligi Kuu Bara na mengine ya Kombe la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho la michuano ya CAF. Pia kuna ingizo jipya la Valentino Mashaka (18) kutoka Geita Gold.

WASIKIE WADAU Kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema walichokifanya Simba ni kuamua kuvunja timu na kufanya usajili ambao utaweza kuibeba timu hiyo kwa misimu zaidi ya mitatu hadi minne mbele endapo watavumilia kuijenga bila kuangalia ushindani kutoka kwa wapinzani.

“Kusajili timu nzima ni kucheza kamari siwezi kusema watafeli au watafaulu ila wamejenga timu nzuri iliyojaa vijana wengi.  Kuhusiana na ushindani ngoja tuone siwezi kuzungumzia wachezaji ambao hawajacheza, usajili unaweza ukapatia au ukakosea,” alisema na kuongeza:

“Kujenga timu kunahitaji uvumilivu hakuna timu ambayo ilikusanywa na ikafanya vizuri muda huohuo japo lolote linaweza kutokea ukiangalia misimu itatu nyuma Yanga walikuwa wanajitafuta sasa wametengeneza timu na wanaonyesha ushindani,” alisema.

Kocha wa zamani wa Tanzania Prisons, Mohamed ‘Adolf’ Rishard, alisema uamuzi walioufanya ni sahihi suala la matokeo ni baada ya ligi kuanza huku akiweka wazi kuwa kuvunja timu Simba haitakuwa mara ya kwanza na ameona kuna wazoefu wapo hiyo ni bora zaidi.

“Kuna Tshabalala, Kapombe, Ngoma ambaye ana msimu mmoja na Che Malone watasaidia kutoa muongozo kwa wachezaji wapya siwezi kuzungumza mengi zaidi,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live