Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba ya Mgunda ni mwendo wa dozi tu

Simba Rekodi CAF Simba ya Mgunda ni mwendo wa dozi tu

Sun, 6 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mastaa wa Simba tayari wapo kambini baada ya kupewa mapumziko mafupi mara walipoinyoosha Mtibwa Sugar kwa mabao 5-0, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda akibadilisha ratiba ya mazoezi kutoka kufanya jioni na kuhamishia asubuhi.

Simba inafanya mazoezi hayo kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bunju pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya michezo ijayo ya Ligi Kuu dhidi ya Singida Big Stars na ule wa Ihefu, huku Mgunda akipania kuendeleza dozi kwa kuwafanyisha mastaa wake mazoezi ya asubuhi kati ya saa 3:00-4:30 asubuhi.

Mgunda aliwaambia wachezaji wake watakuwa wanafanya mazoezi hayo kisha kwenda nyumbani kupumzika na wataingia kambini siku chache kabla ya kusafiri kuifuata Singida Big Stars watakayocheza nayo Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida. Mechi hiyo ni ya kiporo tangu mwezi uliopita.

Katika mazoezi ya juzi ya Simba kiungo aliyekosekana kwenye mechi tatu za Ligi Kuu kati ya Yanga, Azam na Mtibwa, Sadio Kanoute aliiyekuwa anaumwa amerejea na kuliamsha sawasawa na wenzake waliokuwa majeruhi. Kurejea kwa nyota hao kumeifanya kambi hiyo kuzidi kunoga na pia ikimpa kicheko Mgunda na benchi zima la ufundi la timu hiyo iliyotinga pia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba iliyocheza mechi nane hadi sasa ipo katika nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga wanaoongoza msimamo kwa pointi 20, ikiwa ni zaidi ya pointi tatu na walizonazo Wekundu hao na ushindi wa kishindo dhidi ya Mtibwa umempa mzuka zaidi Mgunda akiamini dozi itaendelea mechi zijazo.

Wekundu hao ndio vinara wa timu zilizotupia mara nyingi kambani ikifanya hivyo mara 17, huku yenyewe ikifungwa manne tu ikifuatiwa na Yanga yenye mabao 14 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara tano katika mechi nane ilizocheza hadi sasa ikitetea taji inayotwaa msimu uliopita.

KANOUTE AVUNJA UKIMYA

Akizungumza na Mwanaspoti, Kanoute alisema amerejea akiwa vizuri na awamu tatu za mazoezi alizofanya na wenzake amefanya bila ya kuwa na shida yoyote huku mwili wake ukionyesha upo tayari kwa kupambana kama hapo awali.

Alisema maendeleo ni mazuri amerejea kamili hakuna tena maumivu ya mwili na hali ya kujisikia vibaya imeondoka huku kila zoezi alilopewa kufanya akifanya bila shida yoyote kama ilivyokuwa kwa wachezaji wenzake.

“Kukaa bila kucheza mechi tatu nimekuwa na hamu ya kurudi uwanjani kuipigania timu kufanya vizuri. Ndio maana kwenye mazoezi nimekuwa nikifanya kwa nguvu kadri ambavyo naweza ili kushawishi benchi la ufundi kunipa nafasi ya kucheza,” alisema Kanoute na kuongeza:

“Kama nitacheza kikosi cha kwanza, nitatokea benchi au kutokutumika hilo si jukumu langu bali ni kazi ya benchi la ufundi lenyewe lina uamuzi wa mwisho kwa wachezaji wa kucheza kulingana na mchezo husika.

“Kuhusu afya yangu imeimarika. Nimefanya vizuri mazoezi yote tangu kurejea, wale mashabiki waliokuwa wananiulizia wasiwe na wasi wasi wowote nimerejea kwa nguvu zote kwenye majukumu.”

Kanoute alipokosekana katika kikosi cha kwanza nafasi yake walicheza Jonas Mkude, Nassoro Kapana na Victor Akpan.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live