Kipigo cha bao 1-0 ilichopewa Simba kutoka kwa Horoya ya Guinea, imewapa hasira mastaa wa timu hiyo na leo wanarejea nchini ili kuanza kuiwinda Raja Casablanca ya Morocco kwenye mchezo wa pili wa Kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba itaikaribisha Raja kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Februari 18. na unaambiwa kabla ya safari ya kuja nchini jana jioni kuanzia saa 10:00 hadi saa 1:00 usiku, benchi la ufundi lilianzia huko huko kuiwinda Raja kwa kuifanyisha timu mazoezi.
Ni hivi. kipigo cha Horoya kimeifanya Simba kuanza mapema maandalizi kwa ajili ya Raja ambao waliichapa Vipers ya Uganda mabao 5-0.
Makocha wa Simba, Oliveira Robertinho na Juma Mgunda walisimamia mazoezi hayo ya kuweka miili sawa kwa wachezaji waliotumika sana kwenye mchezo huo kama Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein na wengine.
Mazoezi waliopewa ni yale ya viungo na yalisimamiwa na kocha msaidizi, Ouanane Sellami, kabla ya kupewa muda wa kupumzika na kuangalia wenzao waliokuwa wakiendelea na mazoezi tofauti na yao.
Mazoezi waliyopewa wale ambao hawakutumika kwenye nchezo huo ni yale kawaida na walifanya kwa muda wote.
Wachezaji hao ni Nassoro Kapama, Benno Kakolanya, Habibu Kyombo na wale waliocheza dakika chache kama Kibu Denis na yalisimamiwa na makocha, Oliveira Robertinho na Juma Mgunda.
Programu hiyo maalumu ni kwa ajili ya kurejesha miili sawa kwa wachezaji wote kuwa sawa kwa waliotumika na wasiotumika kabla timu haijapanda ndege kurejea nchini na ilitarajiwa kutua alfajiri ya leo.
Simba inarudi kujiandaa na mchezo wa pili dhidi ya Raja Casablanca na ina matumaini ya kupata pointi tatu kwenye Uwanja wa Mkapa ambao wamekuwa na rekodi nzuri ya kutopoteza dhidi ya wageni kwenye mechi za kimataifa.