Beki Mtanzania wa Chippa United, Abdi Banda baada ya Simba kupoteza mbele ya Raja Casablanca kwa mabao 3-0 Uwanja wa Benjamin Mkapa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, amesema kuna kitu amekiona cha kuisaidia timu hiyo mechi zijazo.
Simba mchezo unaofuata inakwenda kukutana na Vipers ya Uganda, hivyo Banda alishauri mabeki kukumbushana majukumu na kuwasoma wapinzani wao ni hatari kwa mipira gani kuwafikia langoni kwao.
Banda ambaye aliichezea timu hiyo msimu wa (2014-2017), kisha alikwenda kujiunga na Baroka (2017-2019), alisema michuano ya CAF inahitaji mambo muhimu kama nafasi, ulinzi na kufunga.
"Nikitazama kikosi cha Simba kina wachezaji wazuri wa kuamua matokeo, kufungwa na Raja Casablanca haimanishi ni wabaya ila ni aina ya timu waliyocheza nayo, ilikuwa kimbinu zaidi, hivyo kupitia mchezo huo yapo mengi wanapaswa wajifunze.
"Kwenye mchezo wao na Vipers ya Uganda, mabeki wajitahidi kuwa na mawasiliano mmoja akitoka basi wanaobaki lazima wawe makini na miondoko ya wapinzani wao wanapokuwa wanakwenda kwenye lango lao.
"Kwa upande wa viungo na washambuliaji wanatakiwa kushambulia kulingana na hali ya mchezo husika, mfano timu pinzani ikiwa na wachezaji warefu lazima watacheza mipira ya juu, hivyo inapaswa icheze mpira wa chini na wa moja kwa moja wenye faida."
Alisema bado ana imani wanaweza wakafanya mambo makubwa kwenye mchezo unaofuata licha ya kupoteza michezo miwili kwenye hatua hiyo.
Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ana kazi ngumu ya kuhakikisha angalau anashinda mechi zinazokuja mbele yake kwani aliyekuwa anakaimu Juma Mgunda alifanya kitu kwenye michuano hiyo.
ROBERTO CAF
Horoya 1-0 Simba
Simba 0-3 Raja Casablanca
MGUNDA/ MATOLA CAF
Big Bullets 0-2 Simba
Simba 2-0 Big Bullets
Primeiro de Agosto 0-2 Simba
Simba 1-0 Primeiro de Agosto.