Wawakilishi wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba SC wametolewa na mabingwa watetezi, Wydad Casablanca katika moja ya mechi bora sana kwa timu za Tanzania.
Ukirejea namna timu nyingi kutoka sehemu mbalimbali Afrika zinavyoteseka zikienda Morocco dhidi ya miamba hao, na wale ndugu zao Raja Casablanca, utakubali kwamba kwa kweli Simba walicheza kikubwa sana.
Lakini hata hivyo, licha ya hali ya upambanaji waliyokuwa nayo wachezaji, kuna kitu uongozi wa klabu ulikosea na kikawagharimu.
Kwa kiasi fulani mechi ile imeamuliwa na uchanga wa kipa, Ally Salim Khatoro. Achilia mbali goli alilofungwa, yawezekana kipa yoyote angeweza kufungwa, lakini huku kwenye mikwaju ya penati ndiko kwenye walakini.
Sote tunajua ubora wa Aishi Manula linapokuja suala la penati, hata Wydad wenyewe bila shaka taarifa za Aishi kwenye penati lazima watakuwa nazo.
Isingewezekana penati zote nne zilizopigwa ziingie, hapana...Aishi lazima angekufa na penati angalau moja.
Hii ni kwa mujibu wa rekodi zake katika nyakati zote za kukabiliana na mikwaju ya penati, ziwe zile za ndani ya mchezo au hata za kuamua mshindi kama hizi za Wydad.
Mtu anaweza akashituka kwa nini nawalamu viongozi wa Simba kwa kukosekana kwa Aishi ilihali taarifa rasmi ni kwamba yuko majeruhi?
Ni hivi...ni ukweli kwamba Aishi ni majeruhi na aliumia kwenye mchezo wa robo fainali ya ASFC dhidi ya Ihefu pale Azam Complex.
Lakini kuumia kwake kwa asilimia tisini kunatokana na makosa ya viongozi, na hapa ndipo kwenye uti wa mgongo wa hoja yangu.
Baada ya mechi ya mwisho ya makundi ya ligi ya mabingwa dhidi ya Raja Calablanca, Simba iliwapumzisha baadhi ya wachezaji muhimu, akiwemo Aishi Manula.
Wachezaji hao walipewa mapumziko na ruhusa ya kuukosa mchezo dhidi ya Ihefu, wa ASFC, uliokuwa ukifuata baada ya kurudi kutoka Morocco.
Mpango ulikuwa Beno Kakolanya, kipa namba mbili wa Simba, adake mechi hiyo ya robo fainali dhidi ya Ihefu.
Lakini siku moja kabla ya huo mchezo, viongozi wakapata taarifa kwamba Kakolanya amesaini kuitumikia Singida Big Stars msimu ujao.
Viongozi wakapata 'ubaridi' kwamba nini kimetokea. Lakini 'ubaridi huo haukuishia kwenye kujiuliza tu nini kimetokea, bali ulienda mbali zaidi hadi kufikia kuunganisha nukta za mmiliki Singida Big Stars na uhusiano wake na watani wa jadi wa Simba, yaani, Yanga.
Viongozi hao walikuwa na hofu kwamba kutokana na ukaribu huo, yawezekana Kakolanya akatumika kuwahujumu ili watolewe, hivyo asicheze mchezo huo.
Ukimtoa Kakolanya, kipa aliyebaki alikuwa Ally Salim, ambaye hawakuwa na imani naye kutokana na uchanga wake, hivyo wakamuita Aishi kutoka mapumzikoni aje acheze mechi hiyo.
Aishi ambaye alikuwa 'bize' na familia yake ambayo alikuwa mbali nayo kwa muda kidogo, akaitwa aje acheze mechi ya kimashindano bila kufanya mazoezi na akili yake ikiwa imewekwa kwenye hali ya kupumzika.
Mpira wa miguu unachezwa kichwani kupitia akili, miguu ni vifaa tu vya kuchezea. Kwa hiyo akili ikiwa kwenye kupumzika, mwili nao unakuwa huko huko, ukilazimisha ndipo majeraha huja kama matokeo.
Na hiyo ndiyo mechi aliyoumia Aishi...na ndiyo yuko majeruhi hadi leo.
Naam, kwenye mchezo ule Aishi akatoka na akaingia Kakolanya, kipa yule yule waliyemkataa. Akamalizia dakika zilizosalia, bila hujuma wala dalili zake.
Kumuingiza Kakolanya kumalizia zile dakika ulikuwa uamuzi wa kiufundi wa watu waliokuwa kwenye benchi kwa sababu hakukuwa na muda wa majadiliano na wanasiasa wa klabu, yaani viongozi.
Lakini baada ya hapo, wanasiasa wakalichukua hilo na kusema, "Beno Kalolanya marufuku", na kweli, hajacheza tena hadi sasa.
Bwana mdogo Ally Salim akacheza mechi ya ligi dhidi ya Ihefu, akacheza mechi ya ligi ya wataji wa jadi, na akacheza mechi ya robo fainali ya kwanza ya ligi ya mabingwa dhidi ya Wydad, mjini Dar Es Salaam.
Na mechi zote hizo alicheza vizuri sana, na hata mechi ya mkondo wa pili pia aliicheza vizuri sana...lakini kwenye mikwaju ya penati ndipo palipoleta shida.
Mpira kama mchezo wa kitimu, wachezaji husaidiana sana kukumbashana au kufichiana madhaifu na mapungufu muda wote wa mchezo, lakini linapokuja suala upigianaji wa penati, mchezo huu unatoka kuwa mchezo wa kitimu na kuwa mchezo wa mtu mmoja mmoja, kama masumbwi.
Hapo ndipo panahitaji uzoefu mkubwa sana wa kuhimili presha, na kusoma hatua za mtu unayekabiliana naye, yaani kama kipa kusoma hatua za mpigaji na kama mpigaji kusoma hatua za kipa.
Bwana mdogo Ally Salim alivikosa vitu hivyo. Na kuna wakati utakuwa uliona, kipa wa Wydad alikuwa akimtoa mchezoni bwana mdogo kwa kumsukuma sukuma na kumeletea usumbufu.
Hivi vitu ni rahisi sana kuivuruga akili ya kipa mdogo kama Ally Salim, hasa katika uwanja wa ugenini wenye mashabiki wanaopiga kelele kama wamemeza spika ya 'sabufa'.
Aishi Manula asingevurugwa na vitu kama hivyo kwa sababu ameshakutana na mengi sana kwenye maisha yake ya soka. Angekufa na mkwaju angalau mmoja ambao ungeweza kuwatia hofu wapigaji wengine wa Wydad na kuipa Simba faida.
Lakini ndiyo hivyo tena, viongozi hawakupiga hesabu sahihi mapema. Wanaweza kujifariji kwamba wamefanikiwa kumvumbua golikipa mwingine bora kwenye timu yao.
Hilo ni sahihi lakini halikupaswa kutokea kwa gharama hii. Ally Salim ni kipa mzuri na ndiyo maana wanaye tangu zamani.
Ametokea kwenye timu zao za vijana na walimuona ana kitu ndiyo maana wakabaki naye miaka yote, japo hakuwa akicheza.
Na hata kama asingepata nafasi kipindi hiki, angekuja kupata tu huko mbele, lakini haikupaswa kumkurupusha Aishi Manula kutoka mapumzikoni kuja kucheza dhidi ya Ihefu, eti kwa sababu Beno atahujumu.
Matokeo ya maamuzi hayo ndiyo yale kwenye dimba la Mohamed V, penati zote zikaingia.
Hakuna kipindi ambacho Simba walikuwa na nafasi ya kufuzu nusu fainali kama hiki, tena mbele ya bingwa mtetezi na katika uwanja wake wa nyumbani.
Kilichotakiwa ni kuokolewa penati moja tu, uwanja mzima uingie hofu kisha ukae kimya. Kimya hicho kiwashtue wachezaji, wakose na penati zingine...lakini wapi, viongozi ndiyo waliamua!