Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba wakishughulikia hili tatizo, wanatoboa

Simba SC 300.jpeg Simba wakishughulikia hili tatizo, wanatoboa

Mon, 27 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Simba imeanza kinyonge mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kucheza dakika 90 za kwanza za michuano hiyo ikilazimishwa sare ya 1-1 na ASEC Mimosas ya Ivory Coast huku kukiwa na maswali kwa aina ya soka lililopigwa na Wekundu wa Msimbazi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika mchezo huo wa Kundi B, Simba ilionekana kucheza kinyonge tofauti na kawaida yao inapokuwa Kwa Mkapa, kwani ukiondoa dakika 35 za kwanza za kipindi cha kwanza na penalti iliyowapa bao dakika ya 44 kupitia kwa Saido Ntibazonkiza, Simba haikuwa na maajabu yoyote.

Kiwango kibovu cha timu hiyo na hasa kipindi cha pili baada ya kufanyika kwa mabadiliko ya wachezaji kadhaa, kuliwafanya hata mashabiki wachache wa timu hiyo waliofika uwanjani hapo kuwaka kwa hasira wakitishia kulishambulia basi, hadi watu wa usalama uwanjani hapo kufanya kazi ya ziada kuepusha shari.

Sio mashabiki na wapenzi wa timu hiyo tu, bali hata mabosi wa klabu ya Simba walionekana kukerwa na soka hilo bovu na kuamua kuvamia chumba cha kubadilishia nguo na kuwaweka wachezaji hao kitimoto kwa muda wa zaidi ya saa 2 kama njia ya kuwakumbusha wajibu wao uwanjani kwa manufaa ya timu.

Mwanaspoti lilikuwa uwanjani kwenye pambano hilo na hapa chini ni baadhi ya mambo yaliyojiri kwenye mchezo huo na kuonyesha namna gani timu hiyo inapaswa kujipanga kabla ya kuifuata Jwaneng Galaxy ya Botswana na baadae Wydad Casablanca ya Morocco itakazocheza nao kwenye mechi zijazo za kundi hilo.

MASTAA WAKO HOI

Shida kubwa ya Simba ni mastaa wa timu hiyo kuonekana kutokuwa fiti, kwani mchezo huo umethibitisha kwamba wekundu hao wanahitaji msaada wa haraka wa kocha bora wa viungo atakayewarudishia ubora wa kucheza soka la nguvu la kupigania ushindi.

Simba ilikuwa imechoka hakuna mchezaji ambaye alionekana kuwa na nguvu ya kukimbia kwa dakika 70-90 kwa kiwango kilekile, mashabiki wa Simba kila mchezaji waliyetamani kumuona anaingia kusaidia timu walikuwa wale wale sawa na aliyetoka.

WANASHAMBULIA WACHACHE

Simba ilikuwa ngumu kupata mabao ya kutosha kutokana na jinsi walivyokuwa wanashambulia kwa idadi ndogo na kujikuta wanakuwa wanne dhidi ya wenzao watano mpaka sita.

Hawakuwa na ubora wa kupanda wengi kutokana na kukosa nguvu ya kukimbia haraka na kurudi wengi walibaki kuwa watazamaji na sio kusaidiana, hili liliwapa wepesi ASEC kuwadhibiti.

KIBU MMOJA SAWA NA WAWILI

Kwenye mstari wa mbele wa ushambuliaji kulikuwa na mtu mmoja pekee Kibu Denis ambaye alikuwa anaonekana yuko hai kwa kujaribu kutengeneza mbio kwenda lango la wapinzani na juhudi zake zilizalisha bao hilo pekee ingawa alikuwa na uwezo wa kufanya mazuri zaidi.

Baada ya Kibu kutolewa kipindi cha pili Simba ilionekana kama imewatoa watu wawili ndani ya mtu mmoja hakukuwa tena na nguvu ya kupandisha mashambulizi mbele.

Hata walipoingia Luis Miquissone, John Bocco na Clatous Chama kipindi cha pili walikuwa wakicheza kifaza zaidi na kuzidi kuwapa wageni nafasi ya kujitawala Kwa Mkapa, sema tu nayo haikuwa na bahati.

KIUNGO MKABAJI

Simba wakati inafanyia marekebisho ya kikosi chao inatakiwa kutafuta kiungo mkabaji kutokana na eneo hilo hadi sasa bado halijapata mtu sahihi wa kupunguza presha ya mashambulizi kutoka kwa timu pinzani.

Simba imekuwa ikiwatumia Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma na juzi Che Malone Fondoh wakipishana kucheza eneo hilo lakini bado unaona kuna ubora unakosekana na kuwarahisishia wapinzani kufika kirahisi kwenye ngome yao.

SIMBA IJIVUE GAMBA

Msaada unaohitajika Simba unaweza kuwa wa sura mbili kwanza wa mpango wa muda mfupi ambapo hapa haraka anatakiwa kuanza kazi kocha mkuu kuja kuanza kazi ambaye tayari imeshampata Abdelhak Benchikha sambamba na huyo anatakiwa kuja kocha wa viungo bora atakayekuja kupandisha ufiti wa wachezaji.

Kwenye mipango ya muda mrefu hapa sasa Simba inatakiwa kuvaa ngozi ngumu kwa kuwaondoa wachezaji wengi ambao hawana tena kasi ya kuweza kushindana kwa kiwango kikubwa.

Kama inahitaji huduma kama ya gari iliyokufa injini kwa kuivua na kubadilisha upya kwani mastaa walionao sasa hata vipimo vya mazoezi tu wakitumia GPRS zao walizonazo mazoezini zinaweza kuwapa majibu kwamba kuna kundi la wachezaji linatakiwa kupewa mkono wa kwaheri.

ASEC HAIKUWA BORA

Makosa yote ya Simba yaliyojionyesha kwenye mchezo huo bado Asec ilishindwa kuwaadhibu wenyeji, kama Wekundu hao wangekutana na timu bora zaidi inayojua kutumia nafasi au kucheza soka la kasi basi matokeo hayakustahili kuwa haya tunayoyaona sasa.

Hata hivyo, kama Simba itaenda kichovu kwenye mechi hizo mbili mfululizo za ugenini, isitarajie miujiza hata kama itakuwa na kocha mpya, Benchikha aliyetarajiwa kutua nchini jana ili kuanza kazi kuchukua nafasi ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyetimuliwa baada ya zile 5-1 za Yanga na timu kuachiwa Dani Cadena.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live