Mabosi wa Simba wamekutana wameweka mipango mizito kwenye michuano ya Shirikisho Afrika huku wakisisitiza; “Tunaitaka robo fainali.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu hiyo, Said Salim ‘Try Again’ amesisitiza lengo ni kushinda mechi zao zote za nyumbani na kupata pointi kadhaa ugenini.
Simba itaanzia Dar es Salaam wikiendi ijayo dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast kisha wataenda ugenini nchini Niger kuwavaa USGN.
Mwanaspoti linajua Simba wameweka mkakati mzito baada ya mechi ya Jumapili hawataonekana tena Tanzania mpaka mwezi ujao.
Iko hivi; wakishakiwasha na Asec watakwenda Niger kwa ajili ya mchezo wa pili kwenye dhidi ya USGN wakitoka huko wataunganisha moja kwa moja Morocco kwa RS Berkane.
Simba wameamua kufanya maamuzi hayo ili kukwepa gharama katika maeneo mbalimbali pamoja na mizengwe ya nje ya Uwanja wanapokuwa ugenini.
Simba wanaamini kwamba wakitua mapema Morocco itawasaidia kujipanga na vilevile kuwaepusha wachezaji wao na ugonjwa wowote au kusumbuliwa na hali ya hewa.
Ratiba inaonyesha Simba watacheza na USGN Februari 20 na siku saba mbele Februari 27, watakuwa RS Berkane wanayochezea Tuisila Kisinda na Fiston Fiston Abdoulrazak waliowahi kucheza soka nchini katika kikosi cha Yanga.
Mwanaspoti linajua Simba wametanguliza watu wao wawili katika nchi hizo mbili ili kuweka mazingira sawa kabla ya kikosi kufika kucheza michezo hiyo muhimu kurejesha heshima yao Africa.
Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema; “Simba tunapofika katika hatua kama hii hatuna mzaha kabisa tunaamini wachezaji wetu pamoja na benchi la ufundi watakwenda kupambana katika mechi hizo za hatua ya makundi na tutakwenda hatua inayofuata.”
Alisema viongozi kwa upande wao wamejipanga kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri kwa kikosi ili kufikia malengo yao na mwaka huu wako makini zaidi ya misimu iliyopita kwavile wamejifunza mengi ndani na nje ya Uwanja haswa wanapokuwa Arabuni.