'Hata Uviko-19 ilipita'. Ni kauli ya wanachama na mashabiki wa Simba jijini hapa wakielezea machungu wanayopitia hasa baada ya kufungwa mabao 5-1 dhidi ya Yanga wakisema hata hilo litapita wakiwaomba wenzao nchini kutokata tamaa wala kunyosheana vidole.
Pia wamesema badala ya kuwalaumu viongozi wa juu kwa tuhumu mbalimbali ikiwamo 'kuuza' mechi hiyo kwa watani bali waungane kuhakikisha wanaendeleza umoja katika mechi zinazofuata, wakiahidi kufurika uwanja wa Mkapa katika mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas Novemba 25 mwaka huu.
Akizungumza jijini hapa Mwenyekiti wa tawi la Soweto Lunch Time, Yusuph Mwambete amesema kwa sasa kipindi wanachopitia ni kigumu lakini lazima wakubaliane na matokeo hayo akisema waliingia mtego wa watani zao na kunasa.
Amesema wanaowabeza baadhi ya viongozi na kuwajia juu kwa tuhuma mbalimbali lazima wakumbuke Simba imekuwa timu ya mfano kwa mashindano ya ndani na nje ikiwamo kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa misimu minne mfululizo.
"Tumeitwa 'mwakarobo' kutokana na kazi nzuri ya viongozi hao wanaobezwa kwa sasa, hivyo lazima turudi nyuma kujiuliza tulitoka wapi, tunajua ni kipindi cha mpito hiki na kitapita, tuliona vita ya dunia ilipita, vita ya Majimaji ikapita hata Uviko-19 ilipita na hili pia litapita"
"Wenzetu walijipanga na kuweka mitego na tukanasa, sisi tulijisahau kwa kujiamini kwamba tuna kikosi bora ndio maana unaona wenzetu wanafurahia hadi kuweka mabango na kupika supu, hao wanaozungumza tuchukulie kama mtazamo kisha turekebishe panapostahili," amesema Mwambete.
Naye Mwenyekiti wa matawi ya Wekundu hao mkoani humo, Abel Edson amesema kwa sasa siyo kipindi cha kunyosheana vidole bali kujipanga upya na mechi zinazofuata kuhakikisha wanafanya vizuri.
Ameongeza kuwa Mbeya haikuwa na wanachama wengi lakini kupitia uongozi wa juu chini ya Mwenyekiti wa klabu Murtaza Mangungu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdalah 'Try Again' kwa sasa wamefikisha mashabiki na wanachama 800 mafanikio ambayo si ya kubezwa.
"Na bahati nzuri Afrika inatambua nguvu ya mashabiki wa Simba na juzi tuliona tuzo, hatuishii hapo, tunaanza mipango kwa ajili ya kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Mimosas na tutaondoka Alhamisi"
"Mechi iliyopita dhidi ya Al Ahly michuano ya African Football League (AFL) tuliondoka na gari 17, sasa hii ya Novemba 25 tutafurika zaidi kuonesha utayari na umoja wetu kwa timu, mashabiki Mbeya tutafurika Taifa na hawataamini" amesema Edson