Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba waichapa Singida Big Stars kwa Mkapa

Simba Full Time Simba waichapa Singida Big Stars kwa Mkapa

Fri, 3 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mchezo wa Simba dhidi ya Singida Big Stars umeamuliwa kwa mipira ya adhabu ambayo wachezaji wake walitumia vizuri.

Simba imeshinda 3-1 mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Mkapa.

Katika mchezo huo Simba ilifunga mabao mawili kwa mpira wa adhabu na moja bao lililotokana na krosi huku upande wa Singida nao wakifunga bao lao kwa mpira wa faulo.

Simba ndio timu ya kwanza kupata bao dakika ya 8 kwa mpira wa adhabu (Faulo) iliyochongwa na Clatous Chama na Mshambuliaji Jean Baleke aliunganisha mpira uliojaa wavuni.

Kiungo Clatous Chama ameonyesha ubora wa kupiga mipira iliyokufa na kuzalisha mabao mawili ndani ya dakika ya 20 baada ya kutoa pasi ya bao la pili kwa Saido Ntibazonkiza dakika ya 21 kumfanya kufikisha pasi 15 za mabao msimu huu.

Upande wa Singida katika kipindi cha kwanza ilipiga faulo nane huku kiungo Bruno Gomes akipiga tatu na moja aliweka wavuni dakika ya 35.

Upande wa kona kwenye kipindi cha kwanza Singida ilipiga kona mbili huku Simba ikipiga kona moja.

Singida ililazimika kufanya mabadiliko ya mapema baada ya kumtoa Aziz Andambwile dakika ya 32 na kuingia Said Ndemla.

Upande wa kadi za njano kwenye kipindi cha kwanza zilitoka mbili, Yusuph Kagoma moja (Singida Bs) na Sadio Kanoute moja (Simba) ambayo inakuwa ya tisa kwake msimu huu.

Kipindi cha pili Singida BS ilionekana kuingia na akili za kuzui zaidi kwani ilicheza faulo nyingi kwa wachezaji wa Simba kuwapelekea Kelvin Nashon, Pascal Wawa, Bruno Gomes na Biemes Carno kuonyeshwa kadi za njano.

Simba ilipata bao la tatu dakika ya 64 baada ya beki Shomari Kapombe kupiga krosi iliyotua kwenye ya Pape Sakho alipiga ‘acrobatic kick’ iliyomshinda golkipa wa Singida Benedikt Haule na kujaa wavuni.

Bao hilo ni kama alilofunga msimu uliopita katika kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Asec Mimosas katika kundi D na kumfanya achukue tuzo ya bao la msimu.

Kwa matokeo hayo Simba inakuwa wababe wa Singida BS iliyopanda msimu huu baada ya mchezo wa kwanza kumalizika kwa sare 1-1 iliyochezwa Uwanja wa Liti.

Simba inafikisha pointi 53 baada mechi 22 nyuma ya vinara wa ligi Yanga yenye pointi 56 baada ya mechi 21.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live