Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba waichapa Ihefu Chamazi, Baleke aendeleza balaa

Baleke 3.jpeg Jean Baleke alifunga mabao 3

Fri, 7 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Pambano la robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kati ya Simba na Ihefu FC limemalizika usiku huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es salaam kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 na kuifuata Azam Fc kwenye nusu fainali ya michuano hiyo.

Ilikuwa siku nzuri kazini kwa straika Jean Baleke akitupia mabao matatu (hat trick), huku mabao mengine yakiwekwa kimiani na Said Ntibazonkiza na Pape Ousmane Sakho aliyeingia kutoka benchi.

Baleke amefikisha mabao 12 kwenye mashindano yote na manne ya ASFC, mbali na matano ya Ligi Kuu na mengine matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Bao la kufutia machozi la Ihefu lilifungwa na kiungo Raphael Daud dakika ya 61 akiunganisha kwa kichwa mpira wa friikikii uliopigwa na Never Tigere.

Ushindi wa Simba unaipa nafasi ya kucheza nusu fainali dhidi ya Azam iliyoitoa Mtibwa Sugar kwa kuichapa mabao 2-0 mapema wiki hii.

Ihefu haijawahi kupata ushindi katika michezo mitatu iliyokutana kwenye Ligi na Simba, michezo miwili ya msimu wa 2020/21 walikubali kipigo cha 4-0 ugenini na 1-2 nyumbani na mchezo wa mzunguko wa kwanza uwanja msimu huu ugenini wamekubali kichapo cha bao 1-0.

Baleke alifunga mabao hayo katika dakika ya 3, 16 na 28 na kumfanya alingane na Moses Phiri aliyekuwa kinara wa mabao wa Simba kwenye michuano hiyo ya ASFC ambayo bingwa uwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Andrew Simchimbi wa Ihefu pamoja na kukosa nafasi ya kufunga ameendelea kuongoza akiwa na mabao saba akifuatiwa na Clement Mzize wa Yanga mwenye mabao sita.

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' aliwatoa Henock Inonga nafasi yake ilichukuliwa na Kennedy Juma, alitoka Baleke akaingia Mohammed Mussa, Jonas Mkude aliingia kuchukua nafasi ya Joash Onyango, alitoka Saido akaingia Pape Sakho na akatoa Aishi Manula nafasi yake ilichukuliwa na Beno Kakolanya.

Kwa upande wake Kocha wa Ihefu, Zuberi Katwila aliwaingiza Rashid Juma, Hussein Masalanga, Issa Ngao na Yacouba Sogne na kuwatoa Sinchimba, Peater Mwalyanzi, Shaban Kado na Never Tigere.

Ihefu FC hiyo ndio mara yake ya kwanza kutinga hatua ya robo fainali tangu ilipopanda daraja msimu wa 2020/21 baada ya kupanda na kushuka mara zote imekuwa ikiondolewa hatua za awali na sasa inarudi jijini Mbeya kuisubiri Simba kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Jumatatu ijayo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live