Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba vs Vipers, watake wasitake kipigo lazima

Simba Leo 7 March Simba vs Vipers, watake wasitake kipigo lazima

Tue, 7 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Simba, kinatarajiwa kushuka uwanjani kuanzia saa 1:00 usiku leo ili kuikabili Vipers ya Uganda kwenye mechi ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikiwa na kazi mbili muhimu ya kuweka hai matumaini yake ya kutinga hatua ya robo fainali michuano hiyo.

Simba itakuwa wenyeji wa Vipers kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ikiwa ni wiki moja na ushei tangu iliposhinda bao 1-0 ugenini kwenye mechi ya kwanza iliyopigwa jijini Entebbe na kwenye mchezo huo wa marudiano, kazi ya kwanza itakuwa ni kuhakikisha inaibuka na ushindi ili wavune pointi tatu ambazo zinaweza kuwasogeza hadi nafasi ya pili katika msimamo.

Pia itakuwa na kibarua cha pili cha kuiombea mabaya AC Horoya ya Guinea inayocheza na Raja Casablanca nyumbani leo hii, ipoteze mchezo huo ili igande na pointi zake nne ilizokusanya katika mechi tatu zilizopita katika kundi hilo linaloongozwa kwa sasa na Raja yenye pointi 9 mabao 10.

Bila ya shaka kazi ya kwanza ya kusaka ushindi inapaswa kufanywa zaidi na nyota wa safu ya ushambuliaji ambao wanatakiwa kuongeza umakini na utulivu ili waweze kuzitumia vyema nafasi ambazo watakuwa wanatengeneza tofauti na mechi zilizopita ambazo walipoteza nafasi nyingi.

Hilo la kusaka mabao ndilo linaonekana kutiliwa mkazo zaidi na Simba na haikushangaza kuona wiki nzima, benchi la ufundi la timu hiyo likijikita zaidi na mazoezi ya kushambulia na kufunga mabao ingawa pia mara kadhaa ikifanya yale ya kujilinda.

Silaha kubwa inayotegemewa na Simba leo ni mshambuliaji Moses Phiri ambaye katika mechi tisa za mashindano hayo ambazo timu yake imecheza hadi sasa, amefumania nyavu mara tano.

TAKWIMU ZA KIBABE

Simba imekuwa bora katika umiliki wa mchezo na utengenezaji mashambulizi kulinganisha na Vipers jambo linalowapa matumaini makubwa timu hiyo kuibuka na ushindi leo Kwa Mkapa.

Takwimu za mechi tatu zilizopita kwa kila timu kundini, zinaonyesha Simba imekuwa imara katika maeneo mengi kulinganisha na Vipers, japo kuna vitu inapaswa kujiepusha navyo ili iwe salama.

Katika upigaji wa pasi, Simba kwenye mechi tatu zilizopita imepiga pasi 1,332 huku pasi kamili zikiwa ni 1,002, wakati Vipers imepiga 1,014 na zilizokamilika zikiwa ni 717 tu, pia Simba imepiga jumla ya mashuti 36 katika mechi hizo zilizopita ikiwa ni wastani wa mashuti 12 kwa mchezo, huku 11 yakilenga lango.

Kwa upande wa Vipers yenyewe imepiga mashuti 17 tu, ikiwa ni wastani wa mashuti 5.7 kwa mechi huku yaliyolenga lango yakiwa ni mawili tu, ilihali Simba imetengeneza nafasi sita za hatari tofauti na Vipers ambayo haikutengeneza hata moja, huku ikifanya faulo 59 dhidi ya 45 za Wekundu hao.

SIMBA ISHINDWE YENYEWE

Kama historia itatoa hukumu, Simba ina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi leo kutokana na rekodi nzuri inapokuwa nyumbani katika michuano ya klabu Afrika wakati wapinzani wao wamekuwa dhaifu pindi wanapocheza ugenini.

Tangu Vipers ipande Ligi Kuu Uganda, imecheza michezo 12 ya mashindano ya Afrika ugenini na kushinda mara moja tu, ikitoka sare tatu na kupoteza mechi nane na wakati hali ikiwa hivyo kwa timu hiyo ikiwa ugenini, Simba katika mechi 12 zilizopita za CAF ikicheza nyumbani, imeshinda 10 na wamepoteza mechi mbili tu.

REFA MSOMI

Pambano la leo litachezeshwa na refa Bamlak Tessema (42) atakayesaidiwa na Temesgin Atango, Tigle Belachew na Belay Tadesse wote wakiwa wanatoka Ethiopia. Refa Tessema ni mtafiti wa tiba na mratibu wa matibabu nchini Etrhiopia akiwa na shahada ya Sosholojia aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa.

Katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika, refa huyo ameonyesha jumla ya kadi 36 ikiwa ni wastani wa kadi 3.6 kwa kila mechi, za njano zikiwa ni 35 na moja nyekundu.

MSIKE MBRAZILI

Kocha wa Simba, Robert Oliveira 'Robertinho; alisema kuwa wamepata muda wa kutosha kujiandaa na mechi hiyo na wana imani ya kufanya vizuri.

"Tunaanza na wachezaji muhimu, wengine kama hamtowaona basi watacheza mechi inayokuja. Sasa hivi wachezaji wamerudisha ari na morali hivyo tunaamini tutashinda," alisema kocha huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live