Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba vs Mashujaa ni boli na pointi tatu

Simba Kukila Kiporo Chake Na Mashujaa Simba vs Mashujaa ni boli na pointi tatu

Fri, 15 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Simba kikiwa chini ya Kocha Abdelhak Benchikha kinarejea tena uwanjani leo katika pambano la Ligi Kuu ikiikaribisha Mashujaa kwenye Uwanja wa Azam Complex, ikisaka ushindi wa mechi ya 13 kwa msimu huu ili kuua ndege wawili kwa jiwe moja.

Katika mechi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 2:15 usiku, Simba itakuwa inahitaji kupata ushindi ili kufikisha pointi 45 na kuing’oa Azam FC kwenye nafasi ya pili ya msimamo, lakini kupunguza pia pengo la pointi baina ya timu hiyo Yanga ambayo usiku wa jana ilikuwa uwanjani kupepetana na Geita Gold.

Kwa sasa Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 42 baada ya mechi 18, huku Azam ikishika nafasi ya pili kwa alama 44 kwa mechi 20 na Yanga kabla ya mechi ya jana ilikuwa inaongoza kwa pointi 49, saba zaidi na ilizonazo watani wao wa jadi.

Mashujaa inayoshiriki Ligi Kuu kwa msimu wa kwanza, inaikabili Simba ikiwa nafasi ya 11 ikiwa na pointi 21, lakini ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa bao 1-0 katika mchezo wa duru la kwanza lililopigwa mjini Kigoma kwa bao la mkwaju wa penalti iliyopigwa na Saido Ntibazonkiza, lakini kikosi cha timu hiyo kikionekana kuimarika zaidi kwa sasa.

Rekodi zinaonyesha katika mechi nane zilizopita tangu kurejea kwa Ligi Kuu baada ya mapumziko yaliyopisha fainali za Afcon 2023 na Kombe la Mapinduzi 2024, Mashujaa imepoteza mara mbili mbele ya Simba na Yanga, kisha ikashinda tatu zikiwamo mbili mfululizo zilizopita na nyingine tatu pia zikiisha kwa sare ya 1-1.

Kwa rekodi hizo na mwendo wa Simba ni wazi mchezo huo utakuwa mgumu ikizingatiwa kuwa, Simba imerejea katika wimbi la ushindi baada ya Tanzania Prisons kuitibulia kwa kuifumua mabao 2-1 mjini Morogoro wiki mbili zilizopita.

Simba iliyoshinda wa mechi mbili mfululizo zilizopita dhidi ya Coastal Union (2-1) na Singida FG (3-1) itapaswa kuikabili Mashujaa kwa tahadhari kwani hata kwenye mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Mnyama jasho liliwatoka kwa wapinzani hao hao kabla ya penalti ya Saido kuamua matokeo.

Ikiwa na sura mpya zilizosajiliwa kupitia dirisha dogo, akiwamo Mapinduzi Balama, Reliants Lusajo, Emmanuel Mtumbuka, Abrahaman Mussa, Samson Madeleke, David Olomi na wengine wameifanya timu hiyo kuimarika zaidi, lakini hata Simba nayo maingizo mapya yameifanya eneo la mbili na kiungo kuchangamka licha ya ukuta kuruhusu mabao manne katika mechi tatu mfululizo zilizopita za ligi.

Katika mchezo wa leo, Simba itaendelea kutegemea Saido Ntibazonkiza mwenye mabao saba, Willy Onana, Freddy Michael aliyeanza kujipata kikosini, Clatous Chama, Kibu Denis na wengine huku langoni Ayoub Lakred akiwa na nafasi kubwa ya kuanza kutokana na kiwango kizuri alichonacho kwa mechi mbili zilizopita Simba ikiibuka na ushindi.

Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola alisema mechi itakuwa ngumu, lakini kiu yao ni kupata matokeo mazuri kabla ligi haijasimama kupisha kalenda ya FIFA kwa mechi za timu za taifa, pia kupunguza pengo baina yao na timu zilizopo juu katika msimamo, huku beki Israel Mwenda alisema wachezaji wamejiandaa kuendelea kukusanya pointi.

“Ligi inaelekea ukingoni, kila timu inataka kuondoka nafasi iliyopo kujiweka pazuri zaidi. Tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Mashujaa, lakini tumejipanga,” alisema Matola, huku Mwenda alikoleza kwa kusema;”Tunajua Mashujaa wamekuja kwa nia ya kutafuta pointi, lakini sisi tumejiandaa kwa ushindi na mechi itakuwa ngumu, muhimu mashabiki wajitokeze uwanjani kutusapoti,” alisema Mwenda.

Kwa upande wa kocha wa Mashujaa Abdallah Mohammed ‘Baresi’ alisema wamekuja Dar kutafuta pointi tatu.

“Haitakuwa mechi rahisi kwa timu zote, Simba ni bora na tunaiheshimu, lakini hata sisi watuheshimu kwani tumezidi kuimarika na tumekuja kupambana kusaka pointi tatu, licha ya kwamba mechi ya mwisho kupoteza ilikuwa ni Chamazi dhidi ya Yanga,” alisema Baresi huku mmoja ya wachezaji nyota wa timu hiyo, Baraka Mtuwi akisema wachezaji wa Mashujaa wamejiandaa kuendelea wimbi zuri la matokeo kwa timu yao licha ya ukubwa wa Simba.

Mbali na mechi hiyo, leo pia utapigwa mchezo mwingine wa mapema saa 10:00 wakati Namungo itakapokuwa wageni wa Singida FG kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Timu hizo zinakutana huku kila moja ikitoka kupoteza mechi ya mwisho kwa mabao 3-1 mbele ya Simba na Yanga. Singida ilifungwa na Simba kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam huku Namungo ikipasuliwa na nyumbani mjini Lindi na Yanga.

Huu utakuwa mchezo wa kwanza kwa Singida kucheza chini ya kocha mkuu mpya, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ aliyepewa timu hiyo baada ya uongozi kulitema benchi zina la ufundi lililokuwa chini ya kocha Msauzi, Thabo Senong, huku Namungo inayonolewa na Mwinyi Zahera ikiendelea kupambana kujiweka mahali pazuri kwenye msimamo wa ligi.

Chanzo: Mwanaspoti