Kikosi cha Simba kinashuka kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi leo kucheza na Ihefu SC katika mchezo wa hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) utakaopigwa saa 1:00 usiku.
Simba ilifika hatua hiyo baada ya kuiondosha African Sports kwa mabao 4-0 huku Ihefu ikiitoa Pan Africans kwa kuichapa 2-0, hatua ya 16 bora ambapo timu zote zikishiriki Ligi ya Championship.
Timu hizo zinakutana kabla ya kurudiana tena Aprili 10 kwenye Uwanja wa Highland Estate Mbeya huku Ihefu ikikumbuka kupoteza bao 1-0 mara ya mwisho ilipokutana na Simba Novemba 12, mwaka jana.
Simba inatazama kwa jicho la kipekee kwenye michuano hii baada ya kuona katika Ligi Kuu Bara ni ngumu kutokana na kasi ya wapinzani wao Yanga iliyokuwa kileleni kwa tofauti ya pointi nane.
Kikosi hicho kinachonolewa na Roberto Oliveira 'Robertinho' kina kazi kubwa ya kusaka taji hilo ambalo ililikosa kwa msimu uliopita baada ya kwenda Yanga na kuifanya kuchukua kwa mara ya sita.
Ihefu wao hawajawahi kuchukua kombe hili hivyo nao wanahitaji kuandika historia kwenye vitabu vya kumbukumbu kama itafanikiwa kufuzu nusu fainali na hata fainali na kulichukua kwa mara ya kwanza.
Simba imechukua taji hili mara nne kuanzia msimu wa 1995, 2016-2017, 2019-2020, 2020-2021 huku mara ya mwisho ikishinda na Yanga kwa kuifunga bao 1-0 Julai 25, 2021 Uwanja wa Lake Tanganyika.
KUKUTANA NA AZAM FC
Mshindi wa mchezo huu atakutana na bingwa wa michuano hii msimu wa 2018-2019 timu ya Azam FC iliyotinga nusu fainali baada ya kuiondosha Mtibwa Sugar kwa mabao 2-0, mchezo uliochezwa Aprili 3.
VITA YA MABAO
Andrew Simchimba wa Ihefu ndiye kinara wa mabao kwenye michuano hii ambapo amefunga saba hadi sasa akifuatiwa kwa ukaribu na mshambuliaji nyota wa timu ya Yanga, Clement Mzize mwenye sita.
Simchimba huenda akaitumia vizuri nafasi hii kuendeleza kufunga na kujiwekea kwenye mazingira mazuri ya kuivunja rekodi iliyowekwa msimu uliopita na nyota wa zamani wa Coastal Union, Abdul Suleiman 'Sopu ya kufunga mabao tisa.
Kwa upande wa Simba kinara wa mabao kwenye mashindano haya ni Moses Phiri mwenye manne ambaye huenda asiwe sehemu ya kikosi kitakachocheza kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mguu wake.
KAULI ZA MAKOCHA
Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho alisema ni mchezo muhimu kwao hasa kutokana na uhitaji wa taji hilo.
"Moses Phiri, Augustine Okrah bado hawajakuwa fiti kwa asilimia mia hivyo wanaweza wakakosekana ingawa waliobaki kwa kiasi kikubwa wako tayari kwa mchezo huo muhimu wa kutuongezea heshima."
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Ihefu, John Simkoko alisema wamejiandaa vyema kukabiliana na mchezo huo huku wakitambua ugumu uliopo ingawa wamekuwa na maandalizi mazuri ya kimwili na kiakili.