Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba sasa washindwe wao tu kwenda robo fainali ya CAFCL

Ahmed Ally Awatetea Mastraika Simba .jpeg Simba sasa washindwe wao tu kwenda robo fainali ya CAFCL

Sat, 24 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba imekaa patamu na sasa ni ishu ya kushinda kwa Mkapa na kutinga kibabe robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hii ni baada ya kupata sare ya pili dhidi ya ASEC Mimosas kule ugenini Ivory Coast katika mechi iliyomalizika bila ya mabao.

Matokeo hayo yanaifanya ASEC kujihakikishia kumaliza kinara ikifikisha pointi 11 ikiiacha Simba yenye pointi 6 katika nafasi nzuri ya kuamua yenyewe kwenda robo fainali yao ya tano ya CAF katika miaka sita kwa kuifunga tu Jwaneng Galaxy kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Machi 2. Na kama inavyofahamika ‘Kwa Mkapa hatoki mtu’, hii ni nafasi ya dhahabu kwa Wekundu wa Msimbazi kuendelea kutisha katika michuano hii mikubwa zaidi ya ngazi ya klabu Afrika.

Galaxy iliyo katika nafasi ya tatu katika Kundi B itaikabili Wydad Casablanca inayoshika ikiwa na pointi 3. Kama Jwaneng itashinda leo dhidi ya Wydad itafikisha pointi 7 na kukaa juu ya Simba kwa tofauti ya pointi moja, lakini hilo sio tatizo kama Wekundu wa Msimbazi wataizamisha Galaxy Kwa Mkapa.

Simba ikiifunga Galaxy hata kwa bao 1-0 tu linatosha maana itakuwa na pointi 9 ambazo zitaweza kufikiwa na Wydad tu kama itashinda mechi zake mbili kuanzia ya leo na Galaxy na mwisho Machi 2 dhidi ya Asec.

Simba ikishinda mechi na Galaxy itasonga mbele kwa kuwa na matokeo bora dhidi ya Wydad kwani iliifunga 2-0 Dar es Salaam na Wekundu wakafungwa 1-0 ugenini.

 Simba na Galaxy zilitoka 0-0 katika mechi yao ya kwanza kule Botswana, hivyo Wekundu wakishinda hata kwa bao 1-0 Kwa Mkapa watakuwa na matokeo bora dhidi ya Galaxy na dhidi ya Wydad pia.

Simba Jana haikucheza vizuri kipindi cha kwanza ikiwa na mashambulizi machache ambapo licha ya kupiga mashuti mawili yaliyolenga lango bado yalikuwa mepesi kupitika mbele ya ngome ya Asec.

Idara pekee ya wekundu hao ambayo ilicheza kwa utulivu ni eneo la ulinzi ambalo licha ya wenyeji kufanya majaribio kadhaa iliyazima kirahisi kupitia ukuta huo uliowarudisha beki Henock Inonga na kipa Aishi Manula yakiifanya ASEC kumaliza kipindi hicho Cha kwanza bila kuwa na shuti lililolenga lango.

Sadio Kanoute alikosa bao la wazi katika dakika ya kwanza ya kipindi cha pili ambalo lingeiweka Simba katika nafasi nzuri zaidi ya kufuzu.

AYOUB, ONANA

Wakati msafara huo wenye wachezaji 22 ukijipanga kurejea Bongo, mastaa wengine watano wa timu hiyo, wamejifungia Dar es Salaam wakiendelea kujifua katika ‘Gym’ tofauti.

Mastaa hao ni kipa Ayoub Lakred aliyeachwa Dar es Salaam kutokana na kuwa na kadi tatu za njano, na Mawinga Willy Onana, Salehe Karabaka, Edwin Balua, Ladack Chasambi sambamba na nahodha John Bocco ambaye amepewa ruhusa maalumu kwa ajili ya kusoma kozi za ukocha.

Onana, Karabaka na Chasambi waliachwa kutokana na majeraha madogo madogo huku Balua akiachwa kwa sababu za kiufundi.

Taarifa tuliyopenyezewabna mmoja wa vigogo wa Simba kuwa licha ya mastaa hao kubaki nchini, lakini waliachiwa programu maalumu za mazoezi na wanaendelea nazo.

“Shida ya Ayoub ni ya kikanuni lakini hao wengine wengi wao walikuwa na majeraha madogo. Hata hivyo, hawajaachwa kizembe, wameachiwa programu,” alisema kiongozi huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live