Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba sasa wanapiga hesabu za vidole

Mohammed Hussein Simba Msns Magazeti

Mon, 20 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kukubali kichapo cha pili kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wawakilishi wa Tanzania, Klabu ya Simba, sasa matarajio yao pekee ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo ni kwa kutegemea hesabu za vidole.

Simba ambayo imekuwa na rekodi nzuri ya ushindi inapocheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, juzi ilikubali kichapo cha mabao 3-0 uwanjani hapo dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco, hicho kikiwa kipigo cha pili katika hatua hiyo baada ya mechi ya awali ugenini nchini Guinea kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Horoya AC.  

Lakini kipigo hicho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa Simba ni cha kwanza kwao katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufungwa uwanjani hapo katika ushiriki wake wote wa michuano hiyo.

Matokeo hayo yanaifanya Raja Casablanca kuongoza Kundi C kwa kuwa na pointi sita, ikifuatiwa na Horoya AC yenye alama nne na Vipers ya Uganda ikishika nafasi ya tatu kwa pointi yake moja huku Simba ikiburuza mkia bila pointi yoyote.

Kwa maana hiyo, ili Simba iweze kutinga hatua ya robo fainali sasa inatabidi kutegemea hesabu za vidole, kwanza inapaswa kushinda michezo yake mitatu ijayo dhidi ya Vipers ugenini na nyumbani na kisha itapaoikaribisha Horoya AC hapa nchini, lakini kuiombea mema Raja Casablaca ishinde michezo yake mitatu ijayo kabla ya kuhitimisha kwa kukutana na Wekundu wa Msimbazi hao.

Hii ina maana kama Simba ikishinda mechi zake tatu kabla ya kuhitimisha dhidi ya Raja Casablaca, itafikisha pointi tisa, huku mimba hiyo ya Morocco ikishinda tu dhidi ya Horoya nyumbani na ugenini, itakuwa imefikisha pointi 12, wakati mabingwa hao wa Guinea watabaki na alama zao nne kabla ya kufunga hatua ya makundi dhidi ya Vipers.

Hivyo, hata kama Horoya itashinda dhidi ya Vipers na kutoka sare mechi moja dhidi ya Raja Casablanca ina maana itamaliza na pointi nane, moja nyuma ya Simba ambayo haipewi nafasi kubwa ya kwenda kuambulia hata sare ugenini dhidi ya miamba hiyo ya Morocco.

Akizungumzia mchezo huo wa juzi dhidi ya Raja Casablanca, Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho Oliveira, alisema uzoefu na ubora wa kikosi cha wapinzani wao, ndicho kilichowagaribu katika mchezo huo wa pili wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Robertinho alisema wachezaji wake walicheza vizuri, lakini walipaswa kufanya zaidi ya walichofanya kwa sababu ya ubora na uzoefu mkubwa wa Raja Casablanca.

“Kipindi cha pili tulitulia tukafanya mambo kwa usahihi, ila bado haikutosha, lakini huu ni mpira na matokeo haya si ya kushangaza badala yake tunajiandaa na mchezo ujao wa ugenini dhidi ya Vipers wikiendi ijayo,” alisema Robertinho.

Alisema nyota wake wawili, Jean Baleke na Saido Ntibanzokiza hawakuwa fiti kwa asilimia kubwa kwa sababu ya kutoka katika majeraha.

Robertinho alisema matokeo ya juzi wanapaswa kuyasahau na kujiandaa na mchezo ujao wa ugenini dhidi ya Vipers ya Uganda, kwa kufanya maandalizi mazuri ili kupata matokeo chanya.

“Bado tuna mechi nyingine mbele, ni vizuri kujipanga kuliko kusononeka na matokeo haya, kuma michezo mingine iliyopo mbele yetu kujiandaa kwa kufanyia kazi madhaifu yote  yaliyojitokeza katika mchezo wa leo (juzi),” alisema Robertinho.

Naye Kocha Mkuu wa Raja Casablanca, Modher Keboir, alisema kabla ya kucheza mchezo huo alitumia muda mwingi kuwasoma Simba katika michezo mbalimbali na kufanikiwa katika mbinu zake.

Alisema anatambua ugumu wa kuifunga Simba nyumbani kwao na amefanikiwa katika mipango aliyoingia nayo kwa kucheza kwa uzoefu mkubwa na kushinda kwa mabao 3-0.

“Simba ni timu nzuri na ngumu kuwafunga katika uwanja wa nyumbani kwao, nimefanikiwa katika mbinu zetu baada ya kuwasoma wapinzani wetu vizuri,” alisema Keboir.

Simba itasafiri kwenda kuivaa Vipers nchini Uganda Jumamosi wiki hii wakati Raja Casablanca itakuwa nyumbani kuikaribisha Horoya FC.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live