Klabu ya Simba imezidi kujizatiti kuhakikisha mazoezi yao yanafanyika kwa siri tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma kwa kuhama kutoka uwanja wao wa Mo Simba Arena na kwenda Gymkhana au viwanja vingine.
Mwanaspoti ambalo lilienda kwenye mazoezi ya timu hiyo lilikuta Uwanja wa Mo Arena ukiwa umebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na kujengwa ukuta mkubwa ambao unawaweka mashabiki nje kabisa kiasi cha kushindwa kuona mazoezi hayo.
Awali mashabiki walikuwa na uwezo wa kuingia hadi karibu na uwanja huku wakishuhudia mazoezi kwa ukaribu wakiegemea senyenge lakini kwa sasa hali ni tofauti kabisa.
Hadi ufike karibu na senyenge za uwanja ni lazima upite ukuta mkubwa ambao bado haujawekwa geti lakini wapo walinzi ambao wanakagua nani na nani ambaye anaingia uwanjani.
Ukuta huo umezunguka eneo lote la Simba ambalo wanamiliki na hata zile nyumba ambazo zilijengwa ndani yake zimevunjwa na ukuta huo kupita huku ukiwa na senyenge.
Mmoja wa watu wa Simba alilidokeza Mwanaspoti akisema; “Unajua uongozi umefanya hivi kwa sababu ilikuwa tukijiandaa na mechi kubwa tunahama kwa kuhofia watu kuangalia mazoezi yetu wakati hapa ni uwanja wa nyumbani, kwa sasa ni ngumu mtu wa kawaida kuja kwani ataishia kule mbali na kushindwa hata kujua nini kinaendelea.”
Mwanaspoti liliambiwa kuwa ukuta huo unajengwa kwa sababu za kiusalama na ukimalizika hadi juu itakuwa vigumu mtu kuona kinachoendelea ndani.