Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba nguvu yote kwa JKT leo

C6339ed675d7ea627ee8e1077a629b0f Simba nguvu yote kwa JKT leo

Mon, 1 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KIKOSI cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, Simba, leo kinashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kumenyana na JKT Tanzania katika mchezo wa kiporo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Timu hizo zinakuta zikiwa katika nafasi tofauti, Simba ambayo itakuwa mwenyeji ipo nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 42 katika michezo 18 iliyocheza, wakati JKT Tanzania imecheza mechi 21 na ipo nafasi ya 10 kwenye msimamo ikiwa imesanya pointi 24.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza timu hizo zilipokutana Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Simba iliibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0, wafungaji wakiwa ni Meddie Kagere aliyefunga mawili, Chris Mugalu na Luis Miquissone kila mmoja akifunga bao moja.

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema mchezo huo ni mgumu lakini ni muhimu kwao kushinda katika jitihada za kutetea ubingwa wao wa ligi msimu huu na hiyo inatokana na wachezaji wake wote kuwa fiti kiafya.

“Tunakwenda kucheza na timu ngumu iliyopo kwenye nafasi za katikati kwenye msimamo, kwetu ni mchezo ambao tumeupa umuhimu mkubwa sababu lengo ni kutetea taji letu na tukishinda mechi hizi ndio zina tupa matumaini kulingana na ushindani uliopo kwenye ligi,” alisema Gomes.

Mfaransa huyo alisema pamoja na kutambua umuhimu wa ushindi katika mchezo huo, ataendelea kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake kwa kupumzisha baadhi ya wachezaji kutokana kukabiliwa na mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Merreikh utakaochezwa tarehe 6, mwezi huu nchini Sudan.

Gomes alisema klabu yake ina kikosi kipana hivyo ana imani kila mchezaji atakayepata nafasi atacheza kwa kujitolea kuipigania Simba ipate ushindi, hivyo pamoja na kuwapumzisha baadhi ya nyota muhimu lakini hana hofu ya kupoteza mchezo huo wa leo.

Kwa upande wake, kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed ‘Bares’ amesema anatambua wanakwenda kupambana na timu bora na ngumu Afrika Mashariki na kati kutokana na ushiriki wa michuano ya kimataifa, lakini wamejipanga kutoa upinzani ili kuhakikisha wanapa chochote katika mchezo huo.

Bares pamoja na kukiri kuwa mchezo utakuwa mgumu, lakini amesema vijana wake wapo tayari kuikabili Simba leo na wanataka kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuwafunga baada ya wawakilishi hao wa Tanzania Bara kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Najua kama watu wengi hawatupi nafasi pengine kutokana na ubora iliokuwa nao Simba na matokeo ya ushindi ambayo wanayapata kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ukweli tumejipanga na haitokuwa mara ya kwanza kuwafunga Simba kwenye uwanja huo huo wa Mkapa,” alisema.

Kocha huyo alisema ukimtoa mshambuliaji wake tegemezi, Adam Adam ambaye ataukosa mchezo huo kutokana na kwenda kufanya majaribio nje ya nchi, wachezaji wengine waliobaki wapo fiti na wameupania mchezo huo wa leo ili kulipa kisasi cha mabao 4-0 walichokipata kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza.

Chanzo: habarileo.co.tz