Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba na hofu ya mambo ya Uturuki kujitokeza Misri

Simba Kufanya Mazoezi Usiku Kisa Al Ahly.jpeg Simba na hofu ya mambo ya Uturuki kujitokeza Misri

Mon, 24 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Simba imewatoa hofu wanachama na mashabiki wake kuwa itakwenda nchini Misri kuweka kambi ikiwa kamili na si mafungu kama wanavyodhani.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema safari hii wanakwenda wakiwa kamili, ambapo wachezaji wote walioongezwa mikataba na wapya waliosajiliwa, pamoja na jopo lote la makocha litaondoka pamoja kwenda Ismailia nchini humo kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.

"Timu ikiondoka hapa Tanzania mwanzoni mwa mwezi wa saba, tutaondoka tukiwa kamili, kwa maana ya makocha wote; mkuu, msaidizi, wa makipa, wa viungo na meneja, kila mtu atakuwa kwenye nafasi yake, pia tutaondoka wote pamoja hapa hapa na wachezaji wote walioongezewa mikataba na wapya, kuelekea kambini kuanza 'pre season' yetu," alisema Ahmed.

Alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya baadhi ya wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa na wasiwasi, kwani moja kati ya vitu ambavyo viliifanya Simba kutofanya vyema msimu uliopita ni wachezaji wake kuonekana hawana stamina, na hii ilichangiwa na kikosi kwenda nchini Uturuki kimafungu.

Katika kuanza msimu uliomalizika, kikosi hicho kilikwenda kupiga kambi yake nchini Uturuki, katika namna ya kushangaza ilikwenda na baadhi ya wachezaji wachache, wengine wakibaki nchini kwa sababu mbalimbali za kimikataba, wengine kukosa viza.

Baadhi ya wachezaji walisajiliwa wakati 'pre season' inaendelea, na walipofika zilibaki siku chache tu kabla ya kurejea, hivyo wakashindwa kuwa na utimamu wa mwili.

"Tunatarajia kuweka kambi huko, ambapo tathmini yetu imetuonyesha ya kwamba hali ya hewa ni rafiki kwa timu, hoteli tunayokwenda kufikia ni ya kisasa, hapo hapo kuna gym, ina viwanja visivyopungua vinne," alisema Meneja Habari huyo.

Wakati hayo yakiendelea klabu hiyo imetajwa ipo katika hatua za mwisho kupata saini ya kiungo mkabaji raia wa Nigeria, Augustine Okejepha mwenye umri wa miaka 20, kutoka Klabu ya Rivers United.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo na vyanzo vingine kutoka nchini Nigeria zinasema mchezaji huyo amekubali kujiunga na kikosi hicho, ambapo amepata ofa ya mkataba wa miaka mitatu.

"Kila kitu kimekwenda vizuri na kilichobaki ni kutia saini tu, mazungumzo baina ya pande zote mbili yamekamilika," kilisema chanzo hicho.

Mchezaji huyo aling'ara msimu uliomalizika kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuwavutia mabosi wa Simba ambao kwa sasa wako kwenye hatua za mwisho kumaliza dili hilo.

Ahmed amewaambia wanachama na mashabiki wa Simba kuwa usajili wa safari hii utakuwa mkubwa, kwani watasajiliwa wachezaji wenye viwango vya juu, kwa kuwa anayefanya kazi hiyo ni mwenyewe, Mwekezaji, Rais wa Heshima na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohameed Dewji.

"Ule usajili wa kusuasua umeshapitwa na wakati, anayeongoza mashambulizi safari hii ni Mo mwenyewe," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live