Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba na bato kali dhidi ya ASEC leo

Simba Scaled Simba na bato kali dhidi ya ASEC leo

Fri, 23 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kama ilivyo kauli mbiu ya Simba “Nguvu Moja”, mashabiki wa soka leo usiku watakuwa kitu kimoja wakiombea matokeo ya aina mbili kwenye mechi za kundi B. Matokeo ya kwanza ni Simba ishinde ugenini dhidi ya ASEC leo saa 4 usiku, lakini kesho jioni Galaxy akiwa nyumbani aambulie sare dhidi ya Wydad. 

Lakini matokeo yakiwa tofauti bado Simba italazimika kutumia nguvu kwenye mechi ya mwisho nyumbani huku ikisikilizia na matokeo mengine ili kufuzu robofainali ya Ligi ya Mabingwa.

Simba ikishinda leo itafikisha pointi nane ambazo hata Galaxy na Wydad wanaweza kukaza wakazifikia na kuzivuka kama yoyote atapata matokeo kesho kwenye mechi yao. Hesabu za Simba huko Ivory Coast ni kufanya kama ilivyokuwa kwa Horoya ya Guinea kwenye Uwanja wa Charles Konan (Yamoussoukro) ambako mashabiki wa soka nchini humo walishindwa kuamini kilichotokea.

Nini kilitokea? Msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ASEC Mimosas ikiwa na matumaini ya kutinga hatua ya makundi, ilipigwa na kitu kizito katika raundi ya pili, mbele ya mashabiki wao, walipotandikwa bao 1-0 wakiwa nyumbani dhidi ya Horoya na safari yao kwenye michuano hiyo iliishia hapo maana kwenye mchezo wa marudiano huko Guinea ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Rekodi zinaonyesha ndani ya michezo 10 iliyopita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Simba imecheza ugenini, imeshinda mara nne ambazo ni dhidi ya Galaxy (2-0), Nyasa Big Bullets (2-0), 1º de Agosto (3-1) na Vipers (1-0), imetoa sare mbili dhidi ya Power Dynamos (2-2) na Galaxy (0-0).

Wekundu wa Msimbazi pia walipoteza mara nne ambazo ni dhidi ya vigogo, Raja Casablanca (3-1), Wydad Casablanca mara mbili kila mchezo walifungwa 1-0 na Horoya (1-0) kwa takwimu hizo, Simba ina uwezo wa zaidi asilimia 50 wa kupata matokeo mazuri ikiwa ugenini.

Akiongelea mchezo huo na maandalizi ya mwisho ambayo Simba iliyafanya kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Abidjan na wachezaji 22 waliosafiri, kocha mkuu, Abdelhak Benchikha alisema:

“Tunatakiwa kucheza kwenye kiwango chetu bila ya kujali kwamba tupo ugenini, mpango wetu ni kupata matokeo mazuri kwa sababu hayo ndio yatatuweka kwenye nafasi nzuri, tumekuwa na wakati mzuri kama timu kujiandaa kimchezo.”

Kwa upande wake, Aishi Manula ambaye atasimama langoni kufuatia Ayoub Lakred kutumikia adhabu ya kadi, alisema pamoja na ugumu na umuhimu wa mchezo huo hawataingia kwa presha ili kufanikisha mpango wao.

“Hatutaogopa wala kuhofia bali tutafuata maelekezo ya walimu na lengo letu ni kuhakikisha tunashinda. Simba ni timu kubwa na tumecheza mechi nyingi za aina hii katika mazingira tofauti kwahiyo tupo tayari kukabiliana na kila kitakachotokea,” alisema kipa huyo mzoefu zaidi nchini.

FOMU ZILIVYO Simba imeenda Ivory Coast huku ikionekana kuimarika chini ya Benchikha ambaye amerejesha morali ya timu ambayo ilionekana kupotea. Ndani ya michezo mitano iliyopita Wekundu wa Msimbazi hawajapoteza hata mara moja wakishinda mara nne ambazo ni dhidi ya Mashujaa (1-0), Tabora United (4-0), Geita Gold na JKT Tanzania zote kwa bao 1-0 huku wakitoa sare moja dhidi ya Azam FC kwa bao 1-1.

Vijana hao wa Benchikha wamefunga mabao manane kwenye michezo mitano, wana wastani wa kufunga bao 1.6 kwenye kila mchezo huku nyavu zao zikiguswa mara moja ikiwa ni wastani wa 0.2. Takwimu za Mnyama ni nzuri ukilinganisha na wapinzani wao ASEC Mimosas ambao hawajacheza mchezo wowote wa ushindani mwaka huu.  

ASEC Mimosas yenye pigo la mshambuliaji wake hatari, Sankara Karamoko ambaye ameuzwa kwenda Wolfsberger AC ya Austria, katika michezo yao mitano iliyopita katika mashindano yote, imeshinda mechi mbili ambazo ni dhidi ya Stade d’Abidjan (1-0),Jwaneng Galaxy (3-0), wametoa sare dhidi ya BOL (0-0) huku wakipoteza mara mbili dhidi ya Zoman (1-0) na Stella Adjame (2-1).

Miamba hiyo na soka la Ivory Coast ambayo imeshafuzu hatua ya robo fainali, inaongoza msimamo wa kundi B ikiwa na pointi 10 huku Mnyama akishika nafasi ya pili akiwa na tano, imefunga mabao matano tu kwenye michezo mitano iliyopita, wana wastani wa kufunga bao moja kwenye kila mchezo (1.0), wameruhusu mabao matatu wastani wake ni 0.6.

ASEC INAFUNGIKA Takwimu za mechi tano zilizopita zinaonyesha kuwa ASEC Mimosas ni timu yenye uwezo wa kufunga zaidi katika kipindi cha kwanza kwani kwenye mabao matano waliyonayo zaidi ya nusu (3) yamefungwa katika dakika 45 za kwanza huku mawili wakifunga kipindi cha pili.

Hivyo mabeki wa Simba wakiongozwa na Henock Inonga ambaye amerejea baada ya fainali za mataifa ya Afrika kwa kushirikiana na Che Malone Fondoh wanatakiwa kuwa makini dhidi ya wenyeji hao ambao wanaweza wasiitolee macho sana mechi hii baada ya kuwa wameshafuzu robo fainali.

Wakati ASEC Mimosas ikionekana kuwa hatari katika kipindi cha pili pia inaonekana kuwa ni timu ambayo inafungika kipindi hicho kwani kati ya mabao matatu waliyoruhusu mawili wamefungwa kipindi cha kwanza huku moja ikiwa cha pili.

Kwa upande wa Simba hawatabiriki hivyo ASEC Mimosas inaweza kuwa na wakati mgumu kuwadhibiti kwani kati ya mabao manane waliyonayo manne wamefunga kipindi cha kwanza na mengine cha pili. BATO LENYEWE Katika mchezo wa mwisho wa Simba kucheza kwenye ligi dhidi ya JKT Tanzania, Benchikha alitumia viungo watatu wote wenye asili ya kukaba japo mmoja ambaye alikuwa ni Sadio Kanoute alimpa uhuru wa kushambulia.  Fabrice Ngoma na Babacar Sarr walicheza nyuma ya Kanoute huku Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza na Kibu Denis wakiwa sehemu ya safu ya ushambuliaji licha ya changamoto ya ubora wa Uwanja wa Meja Jenerali Michael Isamuhyo, ufanisi wa wachezaji hao ulionekana  hivyo huenda Benchikha akaanza na nyota hao.

Shughuli inaweza kuwa pevu katika eneo la kati la uwanja kutokana na ASEC Mimosas nao kuwa na wachezaji wenye ubora wa aina yake kama vile, Salifou Diarrassouba, Christian Kouame Koffi na Essis Baudelaire Aka ambaye ndiye nahodha wao kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Julien Chevalier.

REFA   Mwamuzi Lahlou Benbraham kutoka Algeria. Ametoa kadi za njano 22 na nyekundu moja msimu huu ndani ya michezo mitano tu aliyochezesha Algeria kwenye Ligi.

Mechi aliyomwaga kadi nyingi zaidi katika uchezeshaji wake ilikuwa Desemba 15 mwaka jana, 2023 kati ya MC El Bayadh dhidi ya USM Alger, alitoa kadi saba za njano.

Kadi chache zaidi alitoa kwenye mechi yake ya mwisho Desemba 28, 2023 kucheza kati ya CR Belouizdad dhidi ya CS Constantine alitoa mbili tu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live