Nadhani mmeona sasa ukubwa wa Simba na Yanga kwenye hii nchi hivyo sasa mtapunguza ubishi usio na tija.
Kila siku watu tunasema kuwa hizo timu ndio zimeshikilia soka la hii nchi lakini watu mnataka kulazimisha tuwe kama Ulaya kwamba timu zote za ligi zipewe uzito sawa. Sio Tanzania bwana.
Sasa kilichotokea juzi kwenye mgawanyo wa mapato ya mechi ya ligi kati ya Simba na Yanga, uliochezwa Aprili 16 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wenyewe mmekiona?
Hizo Simba na Yanga mnazotaka zipewe uzito sawa na nyingine kwenye Ligi, zimeufanya Uwanja wa Benjamin Mkapa upate Sh 47 milioni kwa mechi moja wakati timu nyingine zikicheza hapo au kukiwa matukio makubwa kama lile tamasha la yule Mchungaji, gharama za kukodi Uwanja ni Sh 20 milioni tu.
Sh 62 milioni ambayo serikali imepata kupitia kodi iliyokatwa kwa mchezo ni kiasi kikubwa ambacho sidhani kama kuna mechi nyingine inayohusisha timu tofauti na hizo hapa nchini inaweza kuipa serikali kupitia kodi.
Angalia mamilioni ambayo mechi hiyo imechangia kwa TFF, Bodi ya Ligi, gharama za tiketi, gharama za mchezo, BMT na Chama cha Mkoa halafu linganisha na yale yanayochangiwa na mechi nyingine je ni sawa? Si mnaona hayo ndio mengi zaidi?
Kwa hiyo lazima tuwe wakweli kwamba Simba na Yanga bwana ndio zenye mpira wake hapa Tanzania.
Ndio zipo timu nyingine na zinapaswa kupata haki lakini nguvu kubwa ya Yanga na Simba inazifanya zipate kipaumbele katika mambo mengi kwani hata zenyewe nazo zinaipa neema nchi.
Haya achana na mashindano ya ndani, si mnaona ambacho zinafanya kimataifa?
Huwezi kuukata mkono unaokulisha bwana acheni tu Simba na Yanga zile mema ya nchi.