Klabu ya Simba imelikosa Kombe la Dunia la Twitter 2023 baada ya kuzidiwa kura na RC Bangalore ya India ambayo wamepata asilimia 54 ya kura, huku simba wakiambulia asilimia 46.
Mchuano huo uliendeshwa na mtandao wa Twitter wa Deportes & Finanzas kutoka Brazil kuanzia Mei 3, 2023 na kukamilia Mei 5, 2023.
Kombe hilo lilihusisha vilabu mbalimbali duniani vikiwemo vilabu vikubwa kutoka Bara la Ulaya kama Real Madrid, Manchester United, Liverpool na limekuwa likiendeshwa kwa wafuasi wa mtandao huo wa Twitter kupiga kura kwa kuichagua timu moja wapo kati ya mbili zitakazokutanishwa.
Kutoka Tanzania Simba SC ndio ilikuwa Timu pekee iliyoshiriki Kombe hilo kutoka na kuwa ndiyo klabu yenye wafuasi wengi zaidi kwenye mitandao ya kijamii.
Katika hatua ya nusu fainali Simba ilifanikiwa kumtoa Fenerbahce ya Uturuki kwa kupata kura asilimia 51 huku Fenerbahce wakipata asilimia 41.
Ikumbukwe hatua hiyo inakuja wiki moja baada ya Simba SC kutupwa nje ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa mikwaju ya penalti na Wydad AC ya Morocco katika hatua ya robo fainali.
Hata hivyo, licha ya Simba SC kulikosa Kombe la Dunia 2023 la Twitter, bado timu hiyo inaendelea kuongoza Tanzania, Afrika Mashariki na Kati kwa kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao huo ikiwa nao zaidi ya milioni 1.2.
Utakumbuka data kutoka Kepios zinaonyesha kuna watumiaji wa mitandao ya kijamii bilioni 4.70 dunani hadi kufikia Julai 2022, idadi hiyo ni sawa na asilimia 59.0 ya watu wote ulimwenguni.
Idadi ya watumiaji imeongezeka zaidi kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita ambapo watu milioni 227 walijiunga katika mitandao hiyo.
Hiyo ni sawa na ukuaji wa kila mwaka wa asilimia 5.1, kwa wastani wa zaidi ya watumiaji saba wapya kila sekunde moja, takwimu za Global Digital zinamebainisha kati ya watumiaji 10 wa Inteneti tisa wapo katika mitandao ya kijamii.