Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba mpya yamtikisa Gamondi, awapa mastaa wiki mbili

Miguel Angel Gamondi Simba mpya yamtikisa Gamondi, awapa mastaa wiki mbili

Sat, 1 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha mpya wa Yanga, Miguel Angel Gamondi mjanja sana, japo yupo kwao Argentina, lakini anafuatilia kila kitu kinachoendelea nchini. Amewapigia simu mastaa wake wa kikosi cha kwanza lakini akashtuka kusikia Simba na Azam zimepukutisha idadi kubwa ya nyota wao muhimu.

Mwanaspoti linajua kwamba kocha huyo, ameomba simu za mastaa karibu wote wa kikosi cha kwanza akitaka kuzungumza na mmoja baada ya mwingine kumsabahi na kusikia mpango wake kuelekea msimu mpya, lakini baadhi yao wakamueleza jinsi Azam na Simba zinavyojitafuta kuelekea msimu mpya.

Baadhi ya mastaa aliozungumza nao ni pamoja na Aziz Ki, Fiston Mayele, Djigui Diarra, Kibwana, Bakari Mwamnyeto, Joyce Lomalisa, Yanick Bangala na Khalid Aucho.

Habari za uhakika zinasema kwamba katika mazungumzo yake na mastaa hao kuna wachache wa kikosi cha kwanza waliotumika sana ambao amewaambia wapumzike, lakini wengine amewapa programu za kufanya ndani ya muda mfupi ili kujiweka sawa.

Habari zinasema kwamba amewaambia wachezaji hao kwamba atakuwa kwenye ardhi ya Tanzania ndani ya siku 14 zijazo akiwa na wasaidizi wake wapya watatu ambao wataungana na Mrundi Cedrick Kaze kama Kocha Msaidizi kwani wasaidizi wengine wa awali wamepata madili nje ya Yanga.

Habari kutoka ndani ya Yanga, zinasema kocha hiyo anaamini kitendo cha wapinzani wao wa ndani wakitema wachezaji wengi ni kujipanga kwa msimu ujao, hivyo ni lazima kuanza kujiweka sawa na baadhi ya nyota wa kikosi cha kwanza ambao anapenda kufanya nao kazi na kumrahishia kazi.

Ipo Hivi. Wakati wachezaji wa Yanga wakiwa kwenye mapumziko ya mwisho wa msimu kocha huyo mpya hajapumzika, kwani yuko kazini na sasa anapitia mafaili ya kila mchezaji kisha anashuka na maelekezo.

Kitu cha kwanza ambacho kocha alichokifanya amevuta mafaili ya wachezaji wote waliobaki kwenye kikosi chake kisha akaangalia kila mmoja alivyotumika katika michezo yote 55 ambazo timu hiyo imecheza katika mashindano yote, huku akipitia taarifa zote zinazozishusu timu nyingine pinzani.

Baada ya kupitia faili hilo Gamondi amewavutia waya mastaa wa kikosi cha kwanza cha kocha Nabi kisha kutoa maelekezo ya jinsi wanavyotakiwa kutumia muda huu wa mapumziko.

Mwanaspoti linajua mastaa wachache sana ndio wamepewa kibali cha kupumzika kikamilifu wakiwemo mabeki Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad 'Bacca', kipa Djigui Diarra na mshambuliaji Fiston Mayele ambaye bado hatma yake haijakaa vizuri licha ya kuwekewa dau kubwa mezani la mshahara.

Wengine waliosalia wamepewa programu maalumu ya mapumziko pamoja na mazoezi madogo ya kutoharibu miili yao wakati huu wa mapumziko.

Kundi la wachezaji waliokaa sana benchi Gamondi amewataka kutumia muda mrefu kujiweka sawa kutokana na kutocheza mechi za kutosha, ili atakapokutana nao wawe fiti kuweza kukimbizana na mastaa wenzao wa timu pinzani zinazotarajiwa kuingia kambini punde.

Kocha huyo kuonyesha yupo siriazi, amewaweka masharti magumu kwa kila mchezaji atakayeshindwa kutekeleza programu hiyo na iwapo akigundua hayakufuatwa watakumbana na mwanzo mgumu wa adhabu kutoka kwake.

"Kuna mambo mengi anayafanyia kazi huko huko aliko kifupi hayupo hapa ila ameshaanza kazi, tunapokea simu zake nyingi sana asubuhi, mchana na hata usiku," alidokeza bosi mmoja wa Yanga na kuongeza;

"Ni kocha ambaye anaijua kazi yake, zipo tathimini kubwa anazifanya ambazo sisi kama viongozi tunaona ni mtu muafaka kwa maendeleo ya soka la klabu yetu na hata wachezaji wetu kabla ya msimu mpya haujaanza.

"Kina Diarra wamemwambia jinsi Simba na Azam zilivyoacha wachezaji wengi na yeye mwenyewe kaona kwenye mitandao akawapa angalizo kubwa, anafuatilia sana huyu kocha,"aliongeza kiongozi huyo.

TOP 5-THANK YOU

COASTAL 14

SIMBA 12

AZAM 10

YANGA 7

PRISONS 5

Simba imeachana na wachezaji mahiri akiwamo kipa Beno Kakolanya, mwandamizi Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Gadiel Michael na mastaa wa kigeni akiwamo Mghana, Augustine Okrah.

Wengine waliotemwa ni Wanigeria, Nelson Okwa na Victor Akpan pamoja na Mohamed Ouattara kutoka Burkina Faso. Azam ikiwapa Thank You wachezaji kibao wa kikosi cha kwanza huku ikisainisha wapya watatu akiwamo Feisal Salum na Wasenegal Djibril Sillah na Cheikh Tidiane Sidibe.

Azam imeachana na watu wa maana kama Bruce Kangwa, Rodgers Kola, Ismail Aziz, Cleophas Mkandala, Wilbol Maseke, Aggrey Morris na Kenneth Muguna, huku ikiwasainisha mikataba mipya nyota waliopo kikosi cha sasa sambamba na kutambulisha wachezaji wapya watakaounda kikosi cha msimu ujao.

Kitendo hicho cha kuachwa kwa wachezaji na kuanza kuletwa majembe kumemfanya Gamondi kuamini kabisa wapinzani wao wapo siriazi na msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa baada ya msimu uliomalizika hivi karibuni timu hizo kutoka kapa mbele ya kikosi cha Yanga.

Simba imemaliza msimu wa pili mfululizo ikishindwa kutwaa taji lolote kwa michuano ya ndani na anga la kimataifa ikiishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, huku Azam ikiishia kucheza fainali ya ASFC na kwenye ligi ikimaliza nafasi ya tatu kama ilivyokuwa misimu mitatu mfululizo iliyopita.

Inaelezwa kocha huyo aliyechukua nafasi ya Nasreddine Nabi aliyeipa timu hiyo mataji saba katika miaka miwili na nusu aliyokuwepo Jangwani, amepania kufanya vizuri haswa kwenye Ligi ya Mabingwa inayoanza mwezi Agosti na viongozi wamempa malengo makubwa.

ROBERTINHO KUIFUNGA YANGA

Ukiachilia mbali, usajili mpya hata kitendo cha Robertinho ambaye ni Mbrazili wa Simba, kuifunga mara kadhaa kumemfanya ajipange.

Yanga ilifungwa mabao 2-0 kwenye Wiki ya Mwananchi Agosti mwaka jana kabla ya Simba kumnyakua na kwenye mechi ya kwanza ya Kariakoo Derby ya kwanza iliisha kwa sare ya 1-1,Aprili 16 akashinda mabao 2-0 ya Henock Inonga na Kibu Denis waliopo bado kikosini.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: