Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba mpya yamshtua Gamondi, afunguka haya

Gamondi Simba Pc Simba mpya yamshtua Gamondi, afunguka haya

Tue, 6 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba mpya ya msimu ujao wa 2024-2025 imeonekana kumshtua Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi baada ya kutamka kwamba wapinzani wake hao wamefanya usajili mzuri na kutengeneza timu nzuri tofauti na ile iliyopita, hivyo amewaambia mastaa wake kuna kitu cha kufanya.

Gamondi ametoa kauli hiyo baada ya kuishuhudia Simba Jumamosi iliyopita ikishinda mabao 2-0 dhidi ya APR ya Rwanda katika Tamasha la Simba Day, kabla ya juzi Jumapili kikosi cha Yanga nacho kuichapa Red Arrows ya Zambia mabao 2-1 kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi. Mechi zote hizo zilichezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Yanga na Simba zinatarajiwa kukutana Agosti 8, mwaka huu katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii kuelekea ufunguzi wa msimu wa 2024-2025.

“Sasa tunaanza hesabu mpya kwa ajili ya mchezo wa dabi. Nilijaribu kuwaangalia Simba nimeona kwamba wamefanya usajili mzuri na kwa ujumla wana timu nzuri. Nataka kuwakumbusha wachezaji wetu waachane na picha ya wapinzani wetu kama ilivyokuwa msimu uliopita,” alisema Gamondi.

Gamondi ambaye msimu uliopita aliiongoza Yanga kuifunga Simba jumla ya mabao 7-2 katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara walizokutana, amesisitiza kwamba dabi ya Agosti 8 mwaka huu ni muhimu sana kwani itatoa picha halisi kuhusu jinsi Yanga inavyoanza msimu mpya.

“Mchezo huu utakuwa mgumu na utatoa picha halisi ya jinsi tunavyokuja msimu huu. Tunakwenda kukutana na kikosi ambacho hakikufanikiwa kupata ushindi dhidi yetu msimu uliopita, lazima watakuja kivingine,” alibainisha Gamondi.

Kocha huyo raia wa Argentina, amefichua kuwa anakumbuka msimu uliopita walifungwa na Simba katika fainali ya Ngao ya Jamii na kushindwa kutetea taji lao hilo, hivyo safari hii anataka kupindua meza.

“Sasa tunahitaji kuingia uwanjani kwa lengo la kubadilisha matokeo, hatutaki kurudia kile kilichotokea,” alisema Gamondi na kuongeza.

“Timu yetu itapangwa kulingana na uwezo wa mchezaji atakaouonyesha katika maandalizi yetu, sio kwa majina. Tunahitaji wachezaji watakaokuwa tayari kuonyesha uwezo wao na kufanikisha malengo yetu.”

Kuhusu mechi yao ya Wiki ya Mwananchi dhidi ya Red Arrows waliyoshinda 2-1, Gamondi amesema: “Mchezo ulikuwa maalum kwa kuwafurahisha mashabiki wetu ambao wamefanya kitu kikubwa kwenye siku yao kubwa.”

Hata hivyo, Gamondi aliongeza kuwa furaha ya mechi hiyo sasa imepita na wanahitaji kuanza maandalizi kwa ajili ya mchezo ujao wa dabi dhidi ya Simba.

Wakati Yanga na Simba wakicheza nusu fainali ya pili katika Ngao ya Jamii Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1 usiku, siku hiyohiyo ya Agosti 8 Coastal Union itapambana na Coastal Union kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Simba ndiyo mabingwa watetezi wa Ngao ya Jamii baada ya msimu uliopita kuichapa Yanga kwa penalti 3-1 katika fainli iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa 0-0.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live