Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba mpya inasukwa, subirini balaa

Dsv Joshua Mutale Simba mpya inasukwa, subirini balaa

Wed, 26 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba inaendelea kusuka kikosi chao kimyakimya huku ikielezwa kwamba kati ya mastaa wao 12 wa kigeni waliomaliza na timu hiyo msimu wa 2023-2024, ni nyota watatu tu wanaweza kubaki kwa ajili ya msimu ujao. Je wanaokuja wataweza kutoboa?

Katika wachezaji hao watatu wa kigeni wanaobaki anaongezwa Aubrin Kramo ambaye alijiunga na timu hiyo msimu wa 2023-2024 lakini hakucheza mechi yoyote ya kimashindano kutokana na kuuguza majeraha ya muda mrefu, jina lake likawekwa kando. Kwa sasa amepona na anarudi kukiwasha.

Mbali na wachezaji wa kimataifa, pia Simba imepitisha fagio kwa wazawa ikianza na nahodha John Bocco, Kennedy Juma na Shaban Chilunda. Wazawa wengine wanaosubiri kuagwa ni Abdallah Hamis na Jimmson Mwanuke aliyepelekwa kwa mkopo Mtibwa Sugar.

Kitendo hicho kinadhihirisha wazi kwamba Simba inajengwa upya na viongozi wamekubali kuanza upya kwani kati ya wale inaoachana nao wapo waliokuwa wakitengeneza kizazi cha dhahabu.

Wanaondoka Simba ambayo imemaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita, tayari imetangaza kumalizana na wachezaji wake watatu wa kigeni ambao ni Saidi Ntibazonkiza 'Saido', Luis Miquissone na Henock Inonga aliyeuzwa kwenda FAR Rabat ya Morocco.

Wengine wa kimataifa ambao wanatajwa kwamba muda wowote wanaweza kuachana na timu hiyo ni Clatous Chama ambaye ameitumikia timu hiyo kwa misimu minne na nusu.

Mbali na Chama pia inaelezwa kuwa Sadio Kanoute, Willy Onana, Babacar Sarr, Pa Omar Jobe, Freddy Koubalan baadhi wapo kwenye mazungumzo lakini wengi wao wanaweza kuachwa wakaondoka kwa lengo la kupisha usajili mpya. Wakati ikielezwa nyota hao wanaachwa mastaa wanaosalia

ndani ya timu hiyo kwa upande wa wachezaji wa kigeni ni Kramo, Ayoub Lakred, Fabrice Ngoma na Che Malone Fondoh.

Mtu kutoka ndani ya Simba amethibitisha kwamba kiungo mkabaji, Kanoute amemaliza mkataba na hajataka kubaki ingawa bado hadi jana mchana kulikuwa na mazungumzo, hivyo kama watashindwana timu hiyo fasta itamalizana na Augustine Okejepha ambaye anakipiga Rivers United ya Nigeria kwa lengo la kuziba pengo hilo.

"Kanoute ameshamaliza mkataba na sisi ndio maana unasikia tetesi nyingi za usajili wa kiungo mkabaji kutoka mataifa mbalimbali na huenda akawa miongoni mwa majina yatakayotangazwa kuachana na timu hii kama mazungumzo yataenda kama yalivyo sasa," kilisema chanzo hicho.

Kizazi cha dhahabu byebye Simba kuanzia mwaka 2017, ilianza kujengwa kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi ndani na nje ya nchi ambapo ilifanikiwa kwa takribani misimu minne mfululizo.

Kikosi cha Simba kilitawala Ligi Kuu Bara na kubeba ubingwa huo mara nne mfululizo 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021 kabla ya watani zao wa jadi Yanga kujibu mapigo mara tatu kuanzia 2021-2022, 2022-2023 na 2023-2024.

Mbali na kufanya vizuri katika michuano ya ndani, Simba imetikisa Afrika kwa kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika mara tano katika misimu sita iliyopita. Upande wa Ligi ya Mabingwa ni 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023 na 2023-2024 wakati Kombe la Shirikisho ikiwa 2021-2022.

Kwa wale waliocheza robo fainali hizo zote waliobaki ni Mohamed Hussein 'Tshabalala', Mzamiru Yassin, Shomari Kapombe na Aishi Manula ambao hao wote nao hawana muda mrefu sana watafikia ukomo.

Chama na Luis nao walikuwa sehemu ya mafanikio hayo ya Simba huku nyota hao wawili wakifunga mabao muhimu zaidi ikiwemo lile la Machi 16, 2019 Simba ilipofuzu robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga AS Vita mabao 2-1. Chama alifunga bao la ushindi dakika ya 90.

Pia Simba ilipozitesa timu vigogo Afrika zilipokuja Uwanja wa Benjamin Mkapa,  Luis anakumbukwa zaidi kwa bao safi aliloifunga dhidi ya Al Ahly kwenye Ligi ya Mabingwa Katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkapa na vijana hao wa Msimbazi wakaibuka na ushindi wa bao 1-0.

Kuondoka kwao kunaacha mtihani mzito kwa wale wanaokuja kurithi mikoba yao kama wataweza kuifikisha Simba katika mafanikio zaidi ya hayo kwani hivi sasa klabu hiyo malengo yake ni kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wanaoingia Wakati majina hayo yakitajwa kukatwa ndani ya Simba, majina mapya yanayoingia ni pamoja na Joshua Mutale ambaye inaelezwa amesaini mkataba wa miaka miwili akimudu kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji. Mwingine ni kiungo mshambuliaji kutoka Mashujaa, Omary Abdallah Omary.

Pia yupo beki wa kati raia wa DR Congo, Nathan Idumba Fasika anayecheza Valerenga ya Norway kwa mkopo akitokea Cape Town City ya Afrika Kusini. Yusufu Kagoma kiungo mkabaji kutoka Singida Fountaine Gate, Lameck Lawi ambaye licha ya Simba kumtambulisha kama mchezaji wao kutoka Coastal Union usajili wake umeingia doa lakini inaelezwa wamemalizana.

Kambini kesho Kwa mujibu wa taarifa za uhakika ni kwamba timu hiyo inatakiwa kuingia kambini kesho ikiwa kamili na wachezaji wote wapya pamoja na benchi la ufundi huku ikielezwa kuwa Seleman Matola anabaki kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo. Wadau wanasemaje?

Kipa wa zamani wa Simba, Steven Nemes amesema uamuzi walioufanya Simba ni sahihi kwasababu timu waliyokuwa nayo misimu miwili mfululizo imeshindwa kuthibitisha ukubwa wa timu hiyo huku akitaja kwamba walikuwa na wachezaji wengi ambao hawana uwezo wa kuichezea timu hiyo.

"Simba huwezi kuifananisha na Yanga ambao wanafanya maboresho maeneo machache sana na wanaweza wasisajili msimu huu bado wakawa bora, ukiangalia hata wao walipambana kwa misimu minne baadae wakatulia na kuamua kufanya uamuzi magumu ambayo yamewapa faida," alisema na kuongeza;

"Wengi hawataweza kuielewa Simba kwasasa lakini baada ya miaka miwili au mmoja baadae watakuwa bora na wataleta ushindani kwa timu zilizo imarika sasa Yanga na Azam FC."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live