Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba mpya goma limewaka, wakubaki, kusepa na wapya

Simba Imaraaaa Simba mpya goma limewaka, wakubaki, kusepa na wapya

Thu, 15 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba imemaliza msimu ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara nafasi ambayo ilimaliza nayo msimu uliopita.

Kwenye Ligi Kuu hayo siyo mafanikio makubwa kwa kuwa matarajio yao yalikuwa kutwaa ubingwa.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika iliendelea ilipoishia msimu uliopita hatua ya robo fainali ikatolewa na Wydad Casablanca ya Morocco kwa mikwaju ya penalti.

Hata hivyo, kama ilivyo msimu uliopita pia ilishindwa kufanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) baada ya kutupwa nje nusu na Azam hivyo kumaliza msimu wakiwa watupu.

Mambo mengi yanaelezwa kusababisha hali hiyo, ikiwamo kubadilisha kocha mwanzoni mwa msimu ilianza na Zoran Maki akaja Selemani Matola, Juma Mgunda na kumaliza na Robert Oliviera ‘Robertinho’.

Kila mmoja alifanya kazi, lakini inaonekana ingemaliza na Maki ambaye ilienda naye kwenye maandalizi ya mwanzo wa msimu ilikuwa na nafasi kubwa ya kumaliza kwenye nafasi nzuri.

Sasa Simba inakwenda mapumziko, lakini ikiwa na makovu mengi kutokana na kuwaachia wapinzani wao Yanga makombe yote ya msimu, ingawa ilimaliza ikiwa timu iliyofunga mabao mengi, lakini iliyoruhusu machache.

Simba ilifeli kabisa eneo la usajili msimu huu.

Wachezaji wawili tu wapya ndiyo walifanya vizuri, tena ambao waliingia kwenye dirisha dogo la usajili Saido Ntibazonkiza aliyetokea Geita Gold na Jean Baleke aliyejiunga kwa mkopo akitokea TP Mazembe.

Lakini kundi kubwa liliwaangusha viongozi wa timu na sasa ni wakati wa kusafisha ili kubaki na wachezaji sahihi.

Ufanisi unaonyesha kuna majina yanatakiwa kuondoka moja kwa moja, mengine kwenda kwa mkopo angalau yakajiulize mara mbili na Simba inatakiwa kupambana kuwabakiza wengine kwa ajili ya msimu ujao.

ISMAEL SAWADOGO (AONDOKE)

Alisajiliwa Simba kwenye dirisha kubwa akitajwa kuwa mbadala wa kiungo mahiri, Jonas Mkude, alianza akionekana anaweza kubadilika kadri muda unavyokwenda lakini baada ya kucheza michezo kadhaa, maji na mafuta yalijitenga akakosa nafasi kikosi cha kwanza kwa kuonekana hana uwezo, lakini pia aliathiriwa na kutocheza muda mrefu huko nyuma. Si aina ya wachezaji ambao Simba inawahitaji kwasasa kama inataka kulinda hadhi yao kimataifa. Ni vyema Simba ikaachana naye na kusajili mtu wa kazi.

MOHAMED OUATTARA (AONDOKE)

Ni beki mwenye umri wa miaka 23 raia wa Ivory Coast, ambaye alisajiliwa na Zoran Maki ili kuwa mbadala ya Onyago ambaye kocha huyo alisema hamhitaji kikosini. Alianza michezo ya mwanzo wa msimu lakini hakuonekana kuwa bora. Baada ya kuondoka Maki, Simba walifanya mazungumzo na Onyango ambaye alisusa na kumrudisha, Ouattara akakosa namba kikosi cha kwanza na hata cha pili, baadaye ilielezwa ameomba kuondoka lakini wakamgomea, rasmi mkataba wake umemalizika. Jezi ya Simba imemkataa.

KENNEDY JUMA (ABAKI)

Ana kitu. Huyu hajapata nafasi michezo mingi msimu huu kutokana na ubora wa mabeki wa kati Onyango na Inonga Baka, lakini muda mchache aliocheza ameonyesha anaweza kuwa bora na hana mambo mengi. Asitegemewe msimu ujao, lakini wamwamini.

PAPE SAKHO (ABAKI)

Huyu ni mmoja kati ya wachezaji ambao walisajiliwa Simba kwa mbwembwe. Msimu uliopita alisimama jukwaani kupokea tuzo ya bao bora la CAF. Huu ni mwaka wa tatu akiwa Simba, msimu huu hakupata nafasi kubwa ya kucheza, lakini ameitwa mara mbili mfululizo timu ya taifa ya Senegal. Anaonekana kuwa ni mchezaji mzuri akipewa nafasi na msimu huu amefunga mabao 10 yakiwa ni mengi kuliko uliopita.

JOHN BOCCO (ABAKI)

Hajacheza michezo mingi lakini amefunga mabao 10 ya ligi. Ana mchango mkubwa haswa kwa ukongwe wake na bado ana kitu mguuni. Abaki.

HABIB KYOMBO (AONDOKE)

Alianza vizuri lakini kadiri muda ulivyokwenda alionekana kuporomoka na kuzidiwa na ukubwa wa Simba. Kamaliza msimu akiwa na mabao mawili tu. Ni vizuri akaondoka, kwa kasi Simba inayoingia nayo sokoni hata msimu ujao hatacheza.

MZAMIRU YASSIN (ABAKI)

Amecheza michezo mingi zaidi ya Simba msimu huu kwa ubora wa hali ya juu, msimu uliopita hakuwa na kiwango kizuri. Ameisaidia Simba kwenye mechi nyingi ikiwemo ile kubwa dhidi ya Wydad kwenye Ligi ya Mabingwa, kwa wazawa ndiye kiungo bora kwa sasa, Simba wanatakiwa kumbakiza. Msimu ujao atakuwa bora zaidi akiongezewa watu.

MOHAMMED HUSSEIN TSHABALALA (ABAKI)

Pamoja na kwamba timu yake imemaliza ligi ikiwa haijaruhusu mabao mengi, Tshabalala binafsi amefunga msimu akiwa na asisti sita akiwa beki wa pili kwa pasi nyingi.

Pia ameingia kwenye kikosi bora cha msimu, amefanya kazi kubwa ana uzoefu wa kutosha anatakiwa na Kaizer Chiefs, Simba wambakize kwa nguvu yoyote.

SHOMARY KAPOMBE (ABAKI)

Ni kinara wa pasi za mabao kutokea kwenye ulinzi akiwa nazo nane, amefanya kazi kubwa kwenye michezo ya timu yake msimu huu, hajaonyesha nia ya kuondoka, lakini anatakiwa kubaki Msimbazi kwa ajili ya msimu ujao.

ISRAEL MWENDA (MKOPO)

Apelekwe pale Geita akacheze. Hajapata nafasi ya kutosha msimu huu kutokana na ubora wa mabeki wengine wa pembeni akiwemo mpinzani wake Shomary Kapombe, lakini kwa mechi chache alizocheza ameonyesha uwezo mzuri, anaonekana ni mchezaji mzuri.

JONAS MKUDE (AONDOKE)

Baada ya Simba kumalizana na Wanlo Coulibaly ambaye anatokea Asec Mimosas sioni nafasi ya Mkude kikosini. Huyu anamudu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji na beki wa kati ni dhahiri kuwa Mkude hawezi kuwa na nafasi tena Simba hata ile ndogo aliyokuwa anaipata.

Licha ya heshima yake Simba, lakini msimu huu umekuwa mbaya zaidi kwake akiwa na zaidi ya miaka kumi kwenye timu hiyo, ni vyema akaondoka kwenda kumalizia soka lake kwingine.

KIBU DENIS (ABAKI, LAKINI...)

Pamoja na makocha kumsifu Kibu Denis kuwa msimu huu amefanya vizuri, ukweli ni kwamba namba zinamkataa.

Kibu msimu wa nyuma aliifungia Simba mabao nane, lakini msimu huu amefunga mabao mawili tu bao bora likiwa lile alilofunga dhidi ya Yanga, Simba wambakishe, lakini wampe malengo.

SAIDOO NTIBAZONKIZA (ABAKI)

Huyu ndiye mchezaji mwenye namba bora zaidi kwenye ligi msimu huu pamoja na kwamba timu haikufanya vizuri, amehusika kwenye mabao 29, lakini akitajwa kama mchezaji mwenye nidhamu ya juu. Hakufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa, lakini akibaki msimu ujao atakuwa na moto zaidi kwenye Simba mpya.

SADIO KANOUTE (ABAKI)

Amekuwa na bondi nzuri kila anapocheza na Mzamiru Yassini na ni aina ya viungo wa kisasa.

Mbaya zaidi mkataba wake na Simba umemalizika na mazungumzo ya mwanzoni yalifeli, yupo kwao Mali, Simba wanatakiwa kufanya kazi kubwa kumrudisha kikosini kwani ni ngumu kupata kiungo mwingine wa aina yake bila kuvunja benki.

JIMMYSON MWANUKE (MKOPO)

Mwanuke ni kati ya mawinga machachari kwenye soka la kisasa pia akicheza nafasi ya ulinzi, hajapata nafasi ya kutosha msimu huu tofauti na ulivyokuwa msimu wa nyuma ambao alionekana kuwa bora, inawezekana akawa na kitu ambacho Simba hawajakiona kwake hivyo wampeleke kwa mkopo msimu mmoja wataona kilichojificha.

NASORO KAPAMA (AONDOKE)

Huu ni usajili wa mwanzoni mwa msimu na alitajwa kama mchezaji anayeweza kucheza nafasi nyingi uwanjani, mechi za mwanzoni aliingia baadaye maji na mafuta yakajitenga hakuonekana tena kwenye kikosi cha kwanza cha Simba, aondoke akajaribu kwingine msimu ujao itakuwa ngumu kwake kucheza Simba.

JEAN BALEKE (ABAKI)

Huu ni usajili uliofanya vizuri msimu huu Simba akiwa amejiunga na timu hiyo Januari, lakini hadi mwishoni mwa msimu kwenye michuano ya Caf alikuwa na mabao manne kwenye michezo saba.

Amefunga kwenye michuano yote aliyoshiriki akifunga saba kwenye ligi kuu na matatu FA, anaonekana ana mkataba na Simba hadi mwakani, wakiweza wambakize ashirikiane na Mcameroon mpya wa Simba, Leadro Onana.

CLATOUS CHAMA (ABAKI)

Ameendelea kuonyesha ubora wake kwenye timu ya Simba msimu huu akiwa ametoa pasi 16 za mabao kwenye ligi, amefanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, haonekani kuwa na shida wala maswali mengi akiwa pia ameingia kwenye kikosi bora cha msimu, Simba wanatakiwa kutumia nguvu kumbakiza akitaka kuondoka.

INONGA BAKA (ABAKI)

Huyu pia ni mmoja kati ya mabeki bora kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu pamoja na kwamba msimu uliopita alipewa tuzo ya beki bora, amefanya vizuri kwenye kila mchezo, akiwa ameiongoza timu yake kuruhusu mabao machache, kuna hofu kuwa anaweza kuingia majaribuni endapo vigogo watamfuata, lakini Simba wanatakiwa kuhakikisha wanamlinda msimu ujao ashirikiane na Wanlo Coulibaly.

JOASH ONYANGO (ABAKI)

Hajawa kipenzi cha mashabiki wa Simba kuanzia ametua hapo, pamoja na kwamba amekuwa akicheza michezo yote mikubwa mashabiki wamekuwa wakimlaumu kwenye jambo moja na kusahau mazuri yake yote.

Mwishoni mwa msimu ilielezwa anataka kurudi kwao kumalizia mpira wake, lakini bado anaweza kuisaidia Simba kama watampunguzia mechi au muda wa kucheza uwanjani kutokana na umri wake na presha ya timu.

ALLY SALIM (MKOPO)

Alipata nafasi kwenye michezo migumu mwishoni mwa msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya Aishi Manula kuumia na Beno Kakolanya kushindwana na viongozi wake baada ya kudaiwa ameshasaini sehemu nyingine.

Alifanya makosa kwenye mchezo wa pili dhidi ya Wydad na ule dhidi ya Azam, anakosa uzoefu lakini ni kipa mzuri. Kwa masilahi ya Taifa ni vyema Simba wakasajili kipa mwingine na kumpeleka huyu kwa mkopo akawe bora zaidi. Ana kitu. Anahitaji kucheza.

BENO KAKOLANYA (AONDOKE)

Kama Simba wameshindwa kumuamini kwenye michezo mingi migumu pamoja na kwamba ni kipa waliyekaa naye kwa muda mrefu, vizuri wakamruhusu kuondoka akatafute maisha kwingine wasajili kimpa mzoefu tena wa kigeni kumpa changamoto Manula.

MOHAMMED MUSA (MKOPO)

Alisajiliwa na Simba mara baada ya kumalizika kwa Kombe la Mapinduzi, hajapata nafasi kubwa akiwa amefunga bao moja tu na kuvua jezi, wanatakiwa kumpa muda kutokana na umri wake mdogo, kwa Simba hatacheza aende kwa mkopo sehemu.

AISHI MANULA (ABAKI)

Ni kipa bora mzawa, ameonyesha kiwango cha juu kwa misimu kadhaa mfululizo, baada ya misimu minne huu amepata majeraha yaliyomweka nje kwa muda mrefu na kukosa michezo ya mwisho wa msimu na sasa yupo kitandani, anatakiwa kuendelea kubaki hapo Msimbazi.

PETER BANDA (MKOPO)

Hajapata nafasi kubwa kutokana na majeraha, anaweza kufanya vizuri kama akipewa muda wa kutosha wa kucheza ingawa kwa Simba ni ngumu, msimu huu haukuwa bora kabisa kwake kwa sasa akiwa na miaka 22, akajaribu kwa mkopo kwingine.

MOSES PHIRI (ABAKI)

Alitumika kwenye michezo michache ya mwanzoni msimu huu na kufunga mabao kumi. Hakuna ambaye anashaka na kiwango chake, bali kocha wa timu hiyo Robertinho anaonekana hawezi kufanya naye kazi, Simba wanatakiwa kuwaweka chini wayajenge arudi kwenye mzuka wake wa awali. Ni aina ya wachezaji ambao Simba inawahitaji kurejea kwenye ubora wao.

ERASTO NYONI (AONDOKE)

Kocha anamuangalia zaidi kama kiongozi wa wachezaji ndani na nje ya Uwanja. Lakini apewe heshima yake, akapumzike. Simba ijayo inahitaji watu wa kazi watakaoirejesha kwenye ubora wake si kuangaliana machoni.

GADIEL MICHAEL (AONDOKE)

Alijiunga na Simba akiwa na uwezo mkubwa, lakini hajapata nafasi ya kutosha uwanjani kutokana na uwezo wa Tshabalala kwa faida yake aondoke akacheze kwingine. Bado umri unambeba.

AGUSTINE OKRAH

Huyu ameshaondoka, lakini Simba walikuwa na haraka.

WALIOENDA KWA MKOPO (WASIRUDI)

Victor Akpam, Nelson Okwa wasirudi wamefeli kabisa.

SULUHISHO SIMBA MPYA

Simba ya msimu uliopita haikuwa na mbadala kwenye benchi.Kitendo cha kuingiza wachezaji wengi zaidi kuliko timu zote kwenye tuzo kinaonyesha kuwa walikuwa mahiri. Mfano Simba ilikuwa ikimkosa Clatous Chama, inayumba, ikimkosa Henock Baka, inayumba kwenye safu ya ulinzi. Lakini pia baada ya kumkosa Aishi Manula mwishoni mwa msimu ndiyo kipindi ambacho Simba walimaliza kila kitu kwenye msimu, walipoteza FA, walipoteza Ligi Kuu Bara na wakati huohuo wakapoteza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wanatakiwa kusajili kipa mwenye uwezo sawa na Manula au zaidi yake. Lazima Kakolanya aondoke. Lakini wanatakiwa kusajili beki wa kati mahiri ambaye hakutakuwa na shaka kama Inonga atakosekana, huyu ni lazima atoke kwenye timu zenye uzoefu wa michuano ya kimataifa, kama Asec, Al Ahly, Wydad, Zamalek, Raja na hata Esperance. Lazima pesa itumike. Pale kwa Tshabalala na Kapombe, ni kweli wamekuwa bora, lakini kuna wakati wanaonekana kutumika kwenye michezo mingi zaidi hivyo kuchoka au kukosa ubunifu.

Ni vyema wakasajili mabeki wenye uzoefu badala ya wale wenye vipaji, ili wakati mwingine kuwapumzisha Kapombe na Tshabalala kwenye michezo mingine midogo kama FA na hata ile ya ligi timu ikiwa kwenye michuano ya kimataifa.

Kwa upande wa viungo, Chama, Mzamiru, Saido wanaonekana kuwa bora, lakini ni lazima kuwe na mbadala wao, nafasi zao zinapwaya wanapokuwa na majeraha au kadi, hivyo Simba watakiwa kuhakikisha wanatafuta angalau wachezaji wawili wazoefu wa michuano ya kimataifa kwenye eneo hili ambao wanaweza kucheza nafasi nyingi uwanjani, kama alivyo Yanick Bangala wa Yanga.

Kama Simba watamuacha Sadio Kanoute akaondoka litakuwa pigo lingine kubwa kwao kwa kuwa ni mhimili mkubwa kwenye eneo hili, itakuwa ngumu kutengeneza pacha nyingine kwa Mzamiru.

Kwa washambuliaji, Simba wamefunga mabao yao mengi mzunguko wa pili baada ya kumsajili, Saido na Baleke, kama wangeanza na kasi hii mwanzoni mwa msimu inawezekana sasa lingekuwa jambo lingine.

Ni vyema wakasajili wachezaji mahiri mwanzoni na siyo kwenye dirisha dogo ambalo wanakwenda kukutana na wachezaji wa kubahatisha, hawaepuki kuongeza washambuliaji wawili mahiri. Watu wa kazi wanaojua presha za mechi kubwa. Lakini yote haya yatafanyika wakikubali kutumia fedha za kutosha.

Kocha wampe muda wa kutosha wa maandalizi ya msimu na aongezewe wasaidizi. Nafikiri Super Cup itakuwa picha halisi ya Simba ijayo ni ya makombe au robo tena.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: