Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba mpo? Azam inataka tena

Azam Friendly Wachezaji wa Azam FC

Mon, 20 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba juzi Jumamosi usiku ilikuwa kwenye kibarua cha kupambana na Raja Casablanca ya Morocco katika mechi ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya Jumanne kurudi tena kwenye Ligi Kuu Bara kuvaana na Azam FC iliyotamba inazitaka tena pointi tatu mbele ya Wekundu hao.

Azam inaendelea kujifua kimya kimya kwa mchezo huo, ikicheza mechi kadhaa za kirafiki ili kujiweka fiti kabla ya kumalizana na Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikiwa na kumbumbuku ya ushindi wa bao 1-0 iliyopata katika mechi ya duru la kwanza.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Oktoba 27, mwaka jana bao la Prince Dube (pichani) liliizamisha Simba na kuipa Azam ushindi huo na mechi ijayo inatajwa kama ngumu na itakayotoa dira ya ubingwa kwa wekundu hao wanaoshika nafasi ya pili kwa sasa ikiwa na pointi 50 nyuma ya vinara Yanga.

Akizungumza na Mwanaspoti, jijini Dar es Salaam kocha mkuu wa kikosi hicho, Danni Cadena alisema maandalizi yote yako vizuri na michezo miwili ya kirafiki waliyocheza hadi sasa imeamsha morali kubwa kwa wachezaji.

“Tulikuwa na muda mrefu tangu mara ya mwisho tulipocheza na Dodoma Jiji hivyo tulihitaji mechi za kirafiki ili tuendelee kujijenga imara zaidi tukitambua wapinzani wetu wanaendelea kucheza michezo ya kiushindani.”

Cadena aliongeza licha ya kumkosa kiungo wake mahiri, Malickou Ndoye aliyepata kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji waliofungwa mabao 2-1 Februari 4, ila bado anajivunia uwepo wa machaguo mengi kikosini.

“Ni kweli tunakosa mchezaji muhimu sana lakini anapokosekana mmoja wao basi ni nafasi kwa mwingine kucheza.”

Tangu mara ya mwisho ilipocheza na Dodoma Jiji, Azam imecheza michezo miwili ya kirafiki na yote imeibuka na ushindi ikianza kwa kuifunga KMKM bao 1-0 kisha kushinda 3-0 na Mlandege zote kutoka visiwani Zanzibar.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live