Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba miaka 22 imefukuza makocha 24

Robertinho Xdg Simba miaka 22 imefukuza makocha 24

Wed, 8 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kumbukumbu zinaonyesha ndani ya miaka 22 (kuanzia mwaka 2001), Simba imetwaa jumla ya mataji 33, tisa kati ya hayo ni ya Ligi Kuu, Ngao ya Jamii (9), Tusker (5), Kombe la FA(2), Kombe la Mapinduzi (3), Mtani Jembe(2), ABC Super8 (1), Super Cup (1) na Kagame (1).

Mataji hayo iliyopata Simba katika kipindi hicho yamechangiwa na uwepo wa makocha kadhaa waliowahi kuinoa timu hiyo katika nyakati tofauti kuanzia 2001 hadi sasa.

Simba imenolewa na makocha 24 na makala hii inakuletea orodha ya makocha ambao walifanikiwa ndani ya Simba kwa maana ya walioiwezesha kupata taji na wale waliochemka kwa kuondoka bila kutwaa taji lolote wakiwa na timu hiyo.

1. James Siang’a (2001 -2004) Huyu anabakia kuwa shujaa wa Simba katika kipindi cha miaka 20 kwani ndiye amechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu hiyo kutwaa mataji hayo 34. Chini yake, Simba imetwaa jumla ya mataji 10 ikiwa ni sawa na 35.71% ya mataji yote iliyochukua Simba katika uwepo wa Mwanaspoti. Siang’a aliiongoza Simba kutwaa mataji manne (4) ya Ligi Kuu, mataji matatu (3) ya Tusker, mawili (2) ya Ngao ya Jamii na moja (1) la Kagame.

2. Patrick Phiri (2005, 2010, 2013) Kocha huyo raia wa Zambia naye ni miongoni mwa walioondoka wakiacha heshima ya kuipa mataji Simba katika nyakati tatu tofauti alizoinoa Simba, ameiongoza kutwaa jumla ya mataji manne. Amechukua taji moja moja katika mashindano ya Ligi Kuu, Ngao ya Jamii na Mtani Jembe na Tusker mawili likiwamo lile la Afrika Mashariki.

3. Neider dos Santos (2006) Baada ya Simba kupita katika kipindi cha neema chini ya Siang’a na Phiri, ilipita katika kipindi kigumu cha kutotwaa taji lolote chini ya kocha aliyewafuatia, Neider dos Santos, raia wa Brazil. Kocha huyo baada ya kuitumikia kwa mwaka mmoja alitimka na nafasi yake kukaimiwa na Talib Hilal.

4. Talib Hilal (2007) Ndani ya muda mfupi aliokaa ndani ya Simba, nyota huyo wa zamani wa timu hiyo aliondoka akiacha historia ya kutwaa taji moja ambalo lilikuwa ni ubingwa wa Ligi Ndogo mwaka 2007.

5. Nielsen Elias - 2008 Licha ya kutua kwa mbwembwe ndani ya klabu ya Simba, kocha huyo raia wa Brazil alishindwa kufanya lolote ndani ya timu hiyo kwani haikupata taji chini yake.

6. Milovan Cirkovic (2009, 2012) Aliinoa Simba kwa awamu mbili tofauti. Awamu ya kwanza ilikuwa ni kuanzia katika msimu wa 2008/2009 ambapo Simba haikutwaa taji lolote lakini alipokuja mara ya pili aliipa taji la Ligi Kuu msimu wa 2011/2012

7. Krasmir Benziski (2011) Nyota huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Bulgaria, aliondoka akiwa hajatwaa taji lolote akiwa na Simba hadi alipotimuliwa kabla ya msimu wa 2010/2011 haujamalizika

9. Moses Basena (2011) Baada ya Benziski kutimuliwa, Simba ilimuajiri kocha Moses Basena kutoka Uganda ambaye aliiongoza timu hiyo kutwaa taji la Kombe la Mapinduzi mwaka 2011.

10. Patrick Liewig (2013) Mfaransa huyo anaingia katika orodha ya makocha ambao waliondoka wakiwa hawajatwaa taji lolote ndani ya kikosi cha Simba

11. Abdallah Kibaden (2013) Heshima yake ndani ya Simba ni mataji aliyotwaa wakati alipokuwa akiinoa kabla ya mwaka 2000 lakini pindi alipopewa nafasi ya kuinoa Simba msimu wa 2012/2013 aliondoka akiwa hajatwaa taji lolote.

12. Zdravko Logarusic (2013-2014) Baada ya kupita miaka miwili bila kutwaa taji lolote, Logalusic aliwafanya Simba angalau kurudisha furaha kwani licha ya kutoipa ubingwa wa Ligi Kuu, aliwaongoza kutwaa taji la Mtani Jembe mwaka 2013.

13. Goran Kopunovic (2014-2015) Kocha huyo aliletwa kuchukua nafasi ya Patrick Phiri ambaye alitimuliwa kutokana na mwenendo usioridhisha wa Simba katika msimu wa 2014/2015 na japo hakuweza kutwaa taji la Ligi Kuu, aliiongoza kuchukua ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2015

14. Dylan Kerr (2015-2016) Hana la kujivunia ndani ya kikosi cha Simba kwani katika kipindi cha nusu msimu alioifundisha timu hiyo, hakupata taji lolote.

15. Jackson Mayanja (2016) Alikaimu kwa muda nafasi ya Dylan Kerr katika msimu wa 2015/2016 na hakuweza kuiongoza kutwaa taji hata moja.

16. Joseph Omog (2016-2017) Alianza kuirudisha Simba katika mstari wa kutwaa mataji makubwa nchini baada ya kuiongoza kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la FA Cup msimu wa 2016/2017.

17. Pierre Lechantre (2017-2018) Baada ya Omogo kuachana na Simba, msimu uliofuata, Simba ilinolewa na kocha Pierre Lechantre ambaye alijiunga na timu hiyo Januari 2018 hadi June 2018, aliiongoza kutwaa mataji mawili ambayo ni Ligi Kuu kwa msimu wa 2017/2018 pamoja na lile la Ngao ya Jamii mwaka 2017,

18. Patrick Aussems (2018-2019) Kocha huyo raia wa Ubelgiji alianza kwa kuiongoza Simba Julai 2018 hadi Novemba 2019, alitwaa taji la Ngao ya Jamii 2018, akatwaa taji la Ligi Kuu 2018/2019 na akaiacha akiwa ameiongoza kutwaa Ngao ya Jamii mwaka 2019.

19. Sven Vandenbroeck (2019-2021) Nafasi ya Aussems baada ya kuondoka, ilichukuliwa na Mbelgiji mwenzake, Sven Vandenbroeck ambaye aliitumikia Simba kuanzia Desemba 2019 – Januari 2021, alianza na taji la Ngao ya Jamii 2020, pia Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam msimu wa 2019/2020.

20. Didier Gomez (2021) Mfaransa huyu alijiunga na Simba, Januari 2021 – Oktoba 2021 akichukua nafasi ya Sven aliyeachana na timu hiyo na kutimkia FAR Rabat ya Morocco.

Kocha huyo ndani ya muda usiozidi mwezi mmoja, ameiongoza Simba kutwaa taji la Super Cup na kufurushwa baada ya kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Jwaneng Galaxy ya Botswana na kushindwa kuingia Makundi.

21. Pablo Franco Alijiunga na Simba Novemba 2021 hadi Mei 2022, hakufanikiwa kuchukua taji lolote akiwa na Simba na utawala wa miaka minne kwenye Ligi Kuu ya Tanzania ndipo ulianza kuporomoka kabla ya kufungashwa virago kutokana na mwenendo mbaya.

22. Zoran Marc Alijiunga na Simba mwezi Juni 2022 na kudumu kwa miezi mitatu tu hadi Septemba 2022 akiwa amecheza mechi mbili tu za Ligi na kushinda zote lakini aliamua kutimkia Misri.

23. Juma Mgunda Alijiunga na Mnyama Septemba 2022 akitokea Coastal Union kuchukua nafasi ya Zoran Marc ambapo alihudumu ndani ya Simba hadi Januari 2023 akiwa amefungwa mechi moja tu ya Ligi dhidi ya Azam Fc na kuipeleka Timu hiyo kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa Afrika.

24. Robertinho Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo alijiunga na Simba mnamo Januari 2023 akitokea Vipers SC ya Uganda. Alihudumu kama Kocha Mkuu wa Simba akicheza mechi 18 na kushinda 15, sare 2 na kufungwa mechi 1.

Robertinho amefanikiwa kuchukua Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Yanga kwa changamoto ya mikwaju ya penati. Pia amefanikiwa kuifikisha Simba Robo Fainali ya CAFCL msimu uliopita na hatua ya Makundi msimu huu kabla ya kufurushwa jana Novemba 7, 2023 baada ya kipigo kizito cha bao 5-1 kutoka kwa Yanga walichokipata Simba Novemba 5, 2023.

Kati yao yupi aliukosha mtima wako?

Chanzo: www.tanzaniaweb.live