Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba mguu sawa kwa AS Vita

169129d6e8dd4946585572518ca81aca Simba mguu sawa kwa AS Vita

Wed, 10 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Simba wamewafuata wapinzani wao AS Vita ya Congo DR kwa ajili ya mchezo wa kwanza hatua ya makundi kundi A utakaochezwa keshokutwa.

Kikosi cha wachezaji 27 cha Simba kimekwenda nchini humo, huku waliokosekana wakiwemo John Bocco ambaye ni mgonjwa kwa muda mrefu na Perfect Chikwende. Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa msimu wa mwaka juzi ambapo Simba ilifungwa ugenini mabao 5-0 kisha ikarudi Dar es Salaam na kushinda mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema msafara wa watu 44 unatarajiwa kuwasili leo Kinshasa. “Viongozi wawili wa klabu ya Simba tayari walishawasili kule (Kinshasa) wakifanya maandalizi ya kuipokea timu, matarajio yetu makubwa ni kufanya vizuri kuliko msimu uliopita. Timu imejiandaa kiakili na kimwili,” alisema.

Kocha wa Simba Didier Gomes alisema michezo aliyocheza ya ligi na ya kirafiki ya kimataifa imemsaidia kujua mapungufu ya kikosi chake na kujipanga vizuri kwa ajili ya mchezo huo.

“Matarajio yetu ni kufanya vizuri katika mchezo huo, naamini kwa ubora wa kikosi changu ilichoonesha kwenye michezo iliyopita imetusaidia kujiweka imara kimazoezi ni mapungufu machache nitayafanyia kazi ili kurahisisha kazi,” alisema.

Simba imecheza michezo miwili ya ligi dhidi ya Dodoma Jiji iliyopata ushindi wa mabao 2-1 na Azam FC iliyotoka sare ya mabao 2-2 kisha michezo ya kimataifa kupitia michuano maalum ya Simba Super Cup na kushinda dhidi ya Al Hilal ya Sudan mabao 4-1 na kutoka suluhu dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.

Kikosi cha Simba kilichokwenda DRC ni Aishi Manula, Beno Kakolanya, Ally Salim, Shomari Kapombe, Joash Onyango, Pascal Wawa, Ibrahim Ame, Erasto Nyoni, Peter Muduhwa, Kenned Juma, Gadiel Michael, Mohamed Hussein, Tadeo Lwanga, Jonas Mkude, Rally Bwalya, Said Ndemla na Mzamiru Yassin. Wengine ni Luis Miqquisone, Hassan Dilunga, Ibrahim Ajibu, Cletus Chama, Bernard Morrison, Francis Kahata, Medie Kagere, Miraji Athumani, Cris Mugalu na Junior Lokosa.

Chanzo: habarileo.co.tz