Wakati Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho Oliveira akisema kikosi chake kiko tayari kwa ajili ya mechi ya Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali itakayochezwa leo Ijumaa saa 3:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kwenye Uwanja wa Mohamed wa Tano dhidi ya Mabingwa Watetezi, Wydad Athletic Club nchini Morocco, kiungo ‘tindo’ wa timu hiyo, Mzamiru Yassin, amesema wao kama wachezaji wanaitaka sana mechi hiyo.
Akizungumza akiwa nchini humo, kocha huyo, amesema mbele ya wanahabari kuwa wachezaji wake hawana hofu na mechi hiyo kutokana na kwamba wengi wao ni wazoefu wa michuano ya kimataifa na wameshacheza mechi nyingi ugenini.
Robertinho amesema kwenye mechi ya leo Ijumaa anachoamini ni mbinu zake ambazo amezitengeneza kwa wachezaji kuelekea mechi hiyo ingawa hakutaka kuzitaja hadharani, akiweka wazi kwamba zitaonekana uwanjani na kuwashangaza wapinzani wao.
“Ni mechi ngumu, tunacheza na mabingwa watetezi, lakini tunaamini kwenye mbinu zetu tulizokuja nazo, sitozitaja hapa, haitokuwa mechi rahisi, lakini nina kundi la wachezaji ambao ni wazoefu wa kucheza mechi na timu kubwa tena ugenini, na pia haitokuwa mara ya kwanza kuja kucheza hapa, tulishawahi kuwapo hapa kucheza na Raja Casablanca kwa hiyo wachezaji wangu wameshazoea mazingira ya hapa, utakuwa mchezo mzuri na mgumu pia,” alisema Robertinho.
Hata hivyo, licha ya baadhi ya wadau wa soka nchini kuikatia tamaa Simba SC kushinda ugenini dhidi ya Wydad, Mzamiru amesema hawana muda wa kusikiliza mengi yanaowakatisha tamaa kuelekea mchezo huo wa marudiano na badala yake imani yao ni moja tu ‘inawezekana’.
Simba SC iliwasili mjini Csablanca juzi Jumanne (Aprili 25) majira ya usiku tayari kwa mchezo huo wa Mkondo wa Pili dhidi ya wenyeji wao, Wydad ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 walioupata Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
Mzamiru amesema ushindi umewaaminisha inawezekana na wanaamini watafikia lengo lao la kutinga hatua ya nusu fainali wanayoisaka zaidi ya miaka minne kwa sababu wachezaji wote wanaari na wanautaka vilivyo mchezo huo.
Amesema anatambua mchezo huo utakuwa mgumu na ushindani mkubwa kwa sababu wanahitaji kuendeleza ushindi walioupata nyumbani na kuhakikisha wanaulinda katika mchezo huo wa marudiano.
“Tutaenda uwanjani tukiwa na akiba ya ushindi wa nyumbani na kitendo cha kumfunga bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ni rekodi kubwa kwetu na inatupa nguvu ya kuamini inawezekana.
“Tumeifunga timu kubwa nikiwa miongoni mwa wachezaji waliocheza dakika 90, ni rekodi kubwa kwetu bado tuna dakika nyingine 90 ngumu kuhakikisha tunatinga hatua inayofuata,” amesema Mzamiru ambaye ametokea kuwa kipenzi kikubwa cha mashabiki wa timu hiyo.
Aliongeza kuwa maneno mengi yanayozungumzwa hawayapi nafasi, wanachokiangalia sasa ni namna watakavyojiandaa kuwakabili Wydad kwa dakika 90 ngumu kwao.
“Wachezaji tunautaka sana huu mchezo, na malengo yetu ni kucheza nusu fainali, tuna waheshimu wapinzani wetu na tutacheza kwa nidhamu kubwa ili kutafuta ushindi ugenini jambo ambalo linawezekana,” alisema kiungo huyo.
Naye aliyekuwa Kocha wa Simba na sasa akiinoa KCCA FC ya Uganda, Jackson Mayanja, aliliambia gazeti hili jana kuwa anaimani na timu yake hiyo ya zamani kufanya vizuri katika mchezo huo wa marudiano dhidi ya Wydad.