Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba mastraika, Yanga viungo 'Derby'

Yanga X Simba Balaa Simba mastraika, Yanga viungo 'Derby'

Tue, 31 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Safu ya ushambuliaji ya Simba na safu ya kiungo ya Yanga ndio idara zinazopaswa kuchungwa zaidi katika mchezo wa watani wa jadi wa timu hzo 'Kariakoo Derby' utakaochezwa Novemba 5 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Idara ya kiungo ya Yanga ndio imekuwa tegemeo katika kuipatia mabao timu hiyo kwenye Ligi Kuu hadi sasa kama ilivyo kwa ile ya ushambuliaji ya Simba katika mechi ambazo kila timu imeshacheza hadi sasa.

Katika mechi sita ilizocheza hadi sasa, Simba imefunga mabao 16 ambapo kati ya hayo, mabao 13 sawa na asilimia 81.25 yamewekwa kimiani na washambuliaji huku mengine matatu yakipachikwa na viungo.

Nyota hao wa Simba ambao wamefunga 81.25% ya mabao yote ya Simba msimu huu ni Jean Baleke aliyefunga mabao 6, Moses Phiri aliyepachika matatu, Willy Onana (1), John Bocco (1) na Saido Ntibazonkiza aliyefumania nyavu mara mbili.

Mabao mengine matatu ya Simba yamefungwa na viungo ambao ni Clatous Chama aliyefumania nyavu mara mbili na Fabrice Ngoma aliye na bao moja.

Kwa upande wa Yanga yenyewe, kati ya mabao 20 iliyopachika katika Ligi Kuu, mabao 16 sawa na 80% yamepachikwa na wachezaji wa nafasi ya kiungo huku mengine manne yakifungwa na wale wanaocheza katika nafasi nyingine.

Viungo wanne wa Yanga ndio wamefunga mabao hayo 16 ambao ni Stephane Aziz Ki aliyepachika mabao sita, Maxi Nzengeli mwenye mabao matano, Pacome Zouzoua aliye na mabao matatu huku Mudathir Yahaya akiwa na mabao mawili.

Ukiondoa hayo, mabao mengine ya Yanga yamefungwa na Kennedy Musonda, Yao Atohoula, Dickson Job na Hafidh Konkoni.

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' alisema kwamba anaridhika na kile kinachofanywa na washambuliaji wake lakini kiwango cha timu kiujumla.

"Tumekuwa na muendelezo mzuri wa kufunga mabao kwenye ligi na mechi za kimataifa na hii inaonyesha ubora wa wachezaji nilionao ambao kila mmjoja amekuwa akifanya vizuri ninapompa nafasi. Lakini sio washambuliaji tu, hadi wachezaji wa nafasi nyingine wanafanya vizuri na ndio maana unaona hatujapoteza mechi msismu huu," alisema Robertinho.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema silaha yake kubwa ni kucheza kitimu na ari ya wachezaji kuipigania timu yake ifanye vizuri.

"Timu haipaswi kumtegemea mchezaji mmoja na kila aliyepo kikosini anapaswa kuonyesha kuwa anastahili kupata nafasi ya kuwemo katika timu. Tunachohitaji kuona ni timu ikipata ushindi na kucheza soka la kuvutia jambo ambalo hadi sasa tumeonyesha kwamba tunaweza kulifanya lakini tunapaswa kuimarika zaidi ili tuweze kutimiza malengo yetu," alisema Gamondi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: