Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba mahesabu yote kwa Jwaneng Galaxy

Simba Scaled Kocha Msaidizi wa Simba, Suleiman Matola.

Mon, 26 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kufanikiwa kupata pointi moja kwenye mchezo wa kundi B wa marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas, Simba sasa inapigia mahesabu mchezo wao unaofuata dhidi ya Jwaneng Galaxy ambao utatoa ramani kamili kama wanasonga hatua ya robo fainali au safari yao inaishia hapo.

Juzi Simba ikiwa ugenini ilifanikiwa kuwabana wenyeji wao na kulazimisha kumaliza mchezo 0-0 na hivyo kuendelea kushika nafasi ya pili kwa kundi lao wakiwa na pointi sita wakizidiwa pointi tano na Asec.

Ili kusonga mbele na kuingia hatua ya robo fainali, Simba italazimika kupata ushindi wa lazima kwenye mchezo wao wa mwisho dhidi ya Jwaneng Galaxy utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Machi 2.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana nchini Tanzania kwenye uwanja huo ilikuwa msimu wa 2020/21 ambapo Simba walikubali kipigo cha mabao 3-1 na kuondolewa hatua ya awali ya michuano hiyo.

Akizungumza na Nipashe, Kocha Msaidizi wa Simba, Suleiman Matola alisema wamemalizana na Asec Mimosas na sasa akili na mahesabu yao wanayaelekeza kwenye mchezo wa Machi 2.

"Haukuwa mchezo mwepesi, vijana wamepambana na kufanikiwa kupata alama moja muhimu, tangu tunaingia uwanjani tulipanga kuwazuia wapinzani wetu wasipate bao, na hilo tumefanikiwa na kupata alama moja," alisema Matola na kuongeza, “Leo (jana) tumeanza maandalizi kuelekea mchezo wetu wa mwisho ambao kwetu ni kama fainali, kuna mambo mawili katika mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy kutafuta ushindi utakaotupeleka hatua ya robo fainali na kulipa kisasi.

"Hii haitakuwa mechi ya kawaida bali ni fainali kwetu kuhakikisha tunafikia malengo yetu ya kwenda robo fainali kwa kumfunga mpinzani wetu huyo,” alisema Matola.

Alisema kuwa hawataki kurudia makosa ya msimu wa 2020/2021 kwa kupoteza nyumbani dhidi ya Jwaneng Galaxy na ndio maana maandalizi ya mchezo huo yameanza mara baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Asec Mimosas.

"Tunarejea nyumbani tukiwa na kitu kimoja tu kichwani, mchezo dhidi ya Jwaneng Galaxy, tunaendelea kuwasoma wapinzani wetu kupitia michezo yao ya hivi karibuni waliyoicheza, dhamira yetu ni kuingia tena robo fainali na baadae nusu fainali," alisema Matola.

Akizungumzia mchezo wao wa juzi, Matola alisema walicheza vizuri sana kipindi cha pili na kama wangekuwa makini kwenye safu yao ya ushambuliaji basi wangepata ushindi kwenye mchezo huo.

“Kipindi cha pili tulirudi kwa kasi kwa kuliandama lango la Asec Mimosas, dakika ya 46 Sadio Kanoute alipoteza nafasi ya wazi baada ya kumzidi ujanja mlinda mlango lakini shuti lake lilitoka pembeni kidogo, lakini pia kuna nafasi Chama aliipata nayo tungeweza kunufaika nayo," alisema Matola.

Naye kiungo wa Simba, Clatous Chama alisema mechi haikuwa rahisi kwa sababu wapinzani walikuwa nyumbani na walihitaji kupata matokeo uwanja wa nyumbani. “Ni pointi moja muhimu tumeipata, sasa tunarejea nyumbani  kumaliza kile tulichokianza na kuhakikisha tunasonga mbele,” alisema Chama.

Alisema wanarejea nyumbani kupambana kupata ushindi katika mchezo wa mwisho dhidi ya Jwaneng Galaxy.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’aliwapongeza wachezaji kwa kupambana na kupata pointi moja muhimu dhidi ya Asec Mimosas.

“Mechi ya mwisho ya nyumbani Tanzania itakuwa zaidi ya fainali , kila shabiki ajiandae kwa mchezo huu muhimu,” alisema Try Again.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live