Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba langoni kunawaka moto

Kipa Mmorocco Simba Simba langoni kunawaka moto.

Mon, 21 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sahau kuhusu utitiri wa mastaa walio katika safu ya ushambuliaji ya Simba, sehemu nyingine ambayo hadi sasa inawaka moto kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu ndani ya kikosi hicho ni eneo la kipa na mchuano ni mkali.

Simba kwa sasa ina makipa watano wote wenye uwezo wa kudaka katika michuano yote ndani na nje ya nchi na wote wamesajiliwa kufanya kazi hiyo kwenye michuano iliyo chini ya TFF, sambamba na ile ya CAF kwa msimu huu, jambo linalofanya ushindani kuwa mkali katika eneo hilo.

Wazawa wanne, Ahmed Feruz, Aishi Manula, Hussein Abel, Ally Salim na mgeni, Ayoub Lakred ndio mastaa wanaowania namba moja ya kusimama kwenye milingoti mitatu ya Wekundu wa Msimbazi msimu huu.

Kwa sasa ambao wanapatikana kwenye viwanja vya mazoezi vya Mnyama ni wanne, Lakred, Ally, Feruz na Abel na wote wako fiti huku Manula akiendelea kuuguza jeraha lake la nyonga baada ya kufanyiwa oparesheni lakini anaedelea vizuri na anatarajiwa kuwa timamu mwezi Desemba.

Makipa wote wanne walioko langoni kwa Simba hadi sasa, hakuna mwenye uhakika wa kuwa namba moja kwenye mechi zote kutokana na ushindani na uzoefu walionao.

ALLY SALIM

Ally ndiye amedaka kwenye mechi zaidi ya tano za Simba mfululizo zilizopita ikiwemo zile ngumu dhidi ya Wydad Casablanca kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na dhidi ya Yanga msimu uliopita sambamba na ile fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga aliyoibuka staa wa mchezo kwa kupangua mikwaju ya penalti mitatu na kuipa Simba ubingwa huo.

Hata hivyo, Mwanaspoti linajua, kuna baadhi ya viongozi, makocha na wadau wa soka nchini hawana imani na ubora wa  Salim ndio maana baada ya kuumia kwa Manula na kuondoka kwa Beno Kakolanya aliyetimkia Singida Big Stars, Simba iliingia sokoni kusaka kipa mpya.

Huenda wakawa sahihi kwani Ally licha ya kukaa Simba kwa misimu minne sasa akiibuliwa kutoka timu ya vijana, huu ndio wakati ambao amepata walau mechi tano za kucheza mtawaliwa kikosini hapo.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wanashindwa kujua uimara wa Salim akiwa langoni upo zaidi kwenye jambo gani tofauti na ilivyo kwa Manula akisifika kwa kudaka mashuti ya karibu (1v1), au ilivyo kwa Beno aliyewsifika kuchomoa zaidi michomo ya moto kutoka mbali lakini kwa Salim hadi sasa bado hajaonyewsha ubora wake zaidi ya kudaka penalti zile tatu dhidi ya Yanga.

AYOUB LAKRED

Mwarabu huyu Simba ilimsajili dakika za mwisho baada ya kuumia kwa Mbrazil Jefferson Luis aliyeumia akiwa mazoezini Uturuki siku ya pili tu baada ya kusajiliwa na viongozi kuamua kuachana naye.

Lakred ametua Simba akitokea kwa Mabingwa wa Morocco, Far Rabat alikokuwa kipa namba moja lakini kabla ya hapo aliwahi kuichezea RS Berkane ya  kwao.

Lengo kuu la kumsajili Lakred ni kuisaidia Simba kufikia malengo yake kwa ligi za ndani lakini kubwa zaidi ikiwa ni kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Afrika Super League ambazo Simba itashiriki msimu huu.

Kwa ubora aliuonyesha akiwa na Rabat na Berkane, Lakred anaonekana ni kipa ambaye huenda akampindua Salim pale langoni na kudaka mechi nyingi za Simba wakati Manula akisikilizia kupona.

HUSSEIN ABEL

Jambo ambalo huenda ulikuwa hujui, Simba ilimsajili Abel kwa presha kutoka KMC baada ya dili kipa Mkongoman Lionel Mpasi-Nzau aliyekulia na kuishi Ufaransa kukwama.

Baada ya kuumia kwa Mbrazil Jefferson, Simba ililazimika kutafuta kipa mwingine wa kigeni ndipo ikatua kwa Nzau lakini wakashindwana bei na hapo zikawa zimebaki siku chache ifanye tamasha lake la ‘Simba Day’.

Baada ya kuona jitihada za kupata kipa mgeni zimekwama, ndipo ikamsajili Abel kutoka KMC ikiamini atashirikiana vyema na Feruz na Salim wakati Manula akiendelea kupona, lakini Ghafla ikapata mchongo wa Lakrade na kuvunja benki tena na kumsajili.

Uwezo wa Abel sio wa kubeza kwani msimu uliopita alifanya vizuri akiwa na Tanzania Prisons akifanya ‘saves’, zaidi ya 10 ubora ulivyoendelea hadi alivyotua KMC na sasa Simba ambapo pia ana uwezo wa kuwaweka kina Salim, Lakred na Feruz nje kama akiaminiwa.

AHMED FERUZ

Huu ni msimu wa tatu kwa ‘Bwanamdogo’ huyu akiwa Simba baada ya kupandishwa kutoka timu ya vijana.

Feruz ni kipa aliyeaminiwa na makocha wa makipa waliopita Simba kwa wakati wake ukianza na Mbrazil Milton Nionev hadi sasa kwa Mhispanyora, Dani Cadena.

Sifa yake kubwa ni kujituma, nidhamu jambo ambalo Simba inaamini atakuwa msaada mkubwa kwa klabu hiyo katika miaka ya hivi karibuni na sasa ndio wakati wa kuanza kumpa mechi za kirafiki ili kuimarika taratibu kwani ana kipaji kikubwa.

AISHI MANULA

Watu wengi wanaamini namba ya Manura Simba bado iko palepale na akipona atakuja kuwaweka benchi makipa watakaokuwa wanadaka.

Huenda ikawa kweli kutokana na ubora aliouonyesha tangu mwaka 2013 akianza kucheza Ligi Kuu Azam FC hadi sasa kabla ya kuumia.

Lakini pia inawezekana akipona majeraha aliyoyapata asiweze kurudi kwenye ubora aliokuwa nao kabla ama akawakuta kina Salim, Feruz, Hussein na Lakred wapo kwenye viwango vikubwa vitakavyomfanya asubiri benchi.

Hata hivyo, muda ndio jibu kamili la mitazamo hiyo na akirejea uwanjani atakuwa na la kujibu.

CHUKUA HII

Taarifa nyingine iliyopo kwenye meza za Mwanaspoti kutoka Simba ni kwamba wakali hao wa Msimbazi, wapo mbioni kumtoa kwa mkopo kipa mmoja kati ya Salim, Feruz na Abel ili apate nafasi zaidi ya kucheza licha ya kwamba hawajaamua nani atoke na wanasikilizia ripoti ya kocha mkuu Oliveira Roberto, ‘Robertinho’ na Cadena wa makipa.

Hata hivyo, kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Ivo Mapunda akizungumza na gazeti hili, alisema haina haja ya kuwapunguza kwani kila mmoja ana ubora wake na faida zake kuwepo kikosini.

“Wakiwepo makipa wengi ushindani unaongezeka lakini pia wanalipa benchi la ufundi machaguo mengi kutokana na timu kwani kila kipa huwa ana vitu vyake vya kipekee ambavyo havifanani na mwingine,” alisema Mapunda ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa wa Biashara United ya Championship.

Kocha wa makipa wa Simba, Cadena alisema anafurahia kazi inayofanywa na vijana wake wote na anaamini anatengeneza makipa wanaoweza kudaka mechi za aina yeyote.

“Tangu nimefika hapa mabadiliko ni makubwa, makipa wote wanajituma na kufanya kile ninachowaelekeza kwa bidii na sasa kila mmoja yupo tayari kucheza mechi ya aiana yeyote ile,” alisema Cadena aliyetua kikosini hapo akitokea Azam FC.

Kipa wa zamani wa Twiga Star, Fatuma Omary ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa wa Timu za Taifa za Wanawake, Fatuma Omary alisema Simba inamichuano mingi hivyo kuwa na makipa wengi sio tatizo.

“Msimu huu Simba ina mashindano zaidi ya watatu mfululizo hivyo kuwa na makipa wengi ni faida kwani makocha wanaweza kuwa wanawatumia wote kwa kuwapa mechi tofauti tofauti,” alisema Fatuma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: