Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kwa Chasambi, Yanga kwa Chivaviro

Chivaviroo Chasambi Simba kwa Chasambi, Yanga kwa Chivaviro

Fri, 17 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu, vigogo vya soka nchini ambavyo ni watani wa jadi, Simba na Yanga, tayari vimerusha ndoana zao kwa baadhi ya wachezaji ili kuimarisha vikosi vyao, na mambo yanakwenda bararaba kabisa, imeelezwa.

Na kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hizo, zote zimeanza kwa kumulika katika kuimarisha safu zao za ushambuliaji, Simba ikitua kwa Kiungo Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars, Ladeki Chasambi huku Yanga ikitua Afrika Kusini na kubisha hodi kwa Mshambuliaji wa Kaizer Chiefs, Ranga Chivaviro.

Taarifa za uhakika zilizoifikia Nipashe jana, viongozi wa Klabu ya Simba wamekuwa katika mazungumzo na Chasambi na makubaliano ya awali na klabu yake yanaendelea huku nyota huyo akiwa tayari ameridhia kupewa mkataba.

“Ni kweli usajili umeanza kufanyika, Chasambi amekuwa katika mazungumzo na Simba bado yanaendelea kwa sababu wameshakubaliana kwa mkataba wa awali, huu usajili kwa upande wa mchezaji mzawa,” alisema mtoa habari huyo.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, alipoulizwa alisema ni mapema kuzungumzia suala la usajili kipindi cha dirisha dogo hadi hapo tathimini ya kocha mkuu itakapofanyika.

“Kwa sasa hatuwezi kuongelea usajili wa dirisha dogo kwa sababu wachezaji tuliokuwa nao ni wazuri na suala la kuongeza nguvu kwenye kikosi litafanyika baada ya kufanyika tathimini na benchi la ufundi kuona wapi wanatakiwa kupaboresha,” alisema Ahmed.

Nipashe lilimtafuta Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Swabri Aboubakar, lakini alisema yuko kwenye kikao cha bodi ya  timu hiyo, hivyo atafutwe baadaye na hadi tunakwenda mitamboni hatukufanikiwa kumpata tena.

Kwa upande wa Yanga, taarifa za ndani za klabu hiyo zinasema, Chivaviro, ambaye msimu uliopita aliichezea Marumo Gallants ambayo ilikuwa kundi moja na Yanga katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, ni mmoja wa wachezaji wanaoweza kuongezwa kipindi cha dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 16, mwaka huu.

Straika huyo ilikuwa nusura atue Yanga baada ya msimu kumalizika, lakini aliibukia Kaizer Chiefs, huku taarifa zikisema kwa sasa hana furaha kwenye kikosi hicho kwa kukosa namba ya kudumu, hivyo klabu yake inaweza kukubali kumuuza au kumtoa kwa mkopo.

Taarifa zinasema kuwa moja ya sababu za Injinia Hersi Said kwenda Afrika Kusini, pamoja na mambo mengine ni suala ya usajili wa baadhi ya wachezaji, akiwamo mchezaji huyo.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema jana kuwa tayari faili la Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, limetua kwa viongozi chini ya Injinia na sasa linafanyiwa kazi.

Bila kutaja wachezaji ambao itawasajili au nafasi zao wanazocheza uwanjani, Kamwe alisema tayari viongozi wameshazungumza na wachezaji inaowahitaji na itakapofika dirisha dogo kazi itakayofanyika ni kuwataja na si kutafuta.     "Tayari benchi la ufundi chini ya Miguel Gamondi, limeshawasilisha ripoti kwa uongozi kwa maana ni maeneo gani yanatakiwa kufanyiwa marekebisho, ni aina gani ya wachezaji wanaotakiwa kuja kuiongezea nguvu timu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara, kuna Kombe la FA ambalo halijaanza na Kombe la Mapinduzi.

"Tunataka ikifika mzunguko wa pili, hawa watu tunaowaongeza na dozi ziongezeke siyo mabao matano tena, dirisha likishafunguliwa kazi yetu itakuwa ni kutangaza wachezaji na si kutafuta, tumeshazungumza na wachezaji tunaowahitaji kwa sababu hakuna muda wa kusubiri," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live