Kikosi cha wachezaji 23 wa Simba SC na benchi la ufundi pamoja na viongozi wengine wa timu hiyo kinatarajia kuondoka nchini kesho alfajiri kuelekea nchini Ivory Coast kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa hatua ya makundi dhidi ya ASEC Mimosas.
Hayo yamesemwa leo na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally wakati akizungumzia maandalizi ya mchezo huo unaotarajiwa kupigwa Ijumaa, Februari 23, 2024 nchini Ivory Coast.
“Leo tumefanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wa Mo Simba Arena na alfajiri ya Jumanne (kesho), kikosi kitaanza safari kutoka Dar es Salaam kuelekea Abidjan nchini Ivory Coast kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya ASEC.
“Mazoezi ya leo yamekwenda vizuri sana, wachezaji na benchi la ufundi wamepata muda mzuri wa kufanya mazoezi na maandalizi kuelekea mchezo huo. Leo Jumatatu ndiyo mazoezi ya mwisho, baada ya hapa wachezaji watakwenda kwenye mapumziko na tutakutana saa 7 usiku.
“Tunatarajia kuondoka Tanzania majira ya saa 9 alfajiri ya kesho tukipitia Addis Ababa, Ethiopia, tutapumzika kwa saa 3 kisha asubuhi tutaanza safari kuelekea Ivory Coast mwendo usiopungua saa 6. Tutafika Ivory Coast majira ya saa 9 (mchana) kwa saa za huko sawa na saa 11 jioni kwa saa za Tanzania," amesema Ahmed Ally.