Kwa namna yoyote itakavyokuwa mastaa wa Simba watakuwa na kibarua kizito leo kuwathibitishia mashabiki wao kwamba wana uwezo wa kushinda au kupata matokeo bila kuwepo penalti wala kadi nyekundu ndani ya dakika 90.
Simba wanaikabili timu ngumu ya Namungo leo usiku kwenye Uwanja wa Mkapa huku watani zao Yanga wakiwakejeli mitandaoni kwa kitendo cha mechi zao nne za awali kutawaliwa na kadi nyekundu au penalti.
Kwenye mechi za Simba dhidi ya Biashara United, Dodoma Jiji, Polisi Tanzania na Coastal Union kote ilitolewa penalti au kadi nyekundu au vyote kwa pamoja. Kocha wa Simba, Hitimana Thiery ameahidi mabadiliko kwenye kikosi cha kwanza lakini hayatakuwa makubwa sana lakini mechi itakuwa nzuri.
Simba huenda ikaanza na Aishi, Kapombe, Israel Mwenda, Kennedy, Onyango, Mkude, Dilunga, Bwalya, Bocco, Kibu na Morrison/Muhilu.
Simba yenye pointi nane, inakutana na wanyonge wao Namungo ambao wana rekodi nao nzuri ya kuwapasua. Tangu wamepanda wamekutana mara nne, Simba imeshinda tatu na sare moja. Msimu wa 2019/20, Simba ilishinda 3-2, mzunguko wa pili (0-0), 2020/21 (Namungo 1-3 Simba) na mechi ya raundi ya pili Simba iliichakaza Namungo 4-0.
Simba inahitaji matokeo kwenye mchezo wa leo ili kuamsha hamasa iliyoshuka baada ya kuanza msimu kwa kusuasua.
“Mchezo uliopita tumepata nafasi zaidi ya tano, lakini washambuliaji hawakuwa na watulivu ndio sababu ya kupata pointi moja, tukiwa nyumbani, licha ya kuwa na presha tutapambana kurejea kwenye mstari,” amesema Seleman Matola, kocha msaidizi wa Simba na kuongeza;
“Kila baada ya siku mbili tuna mchezo wa ligi, jambo linalotuwia ugumu kurekebisha makosa kwa haraka, hatuna maana kwamba itakuwa hivyo hadi mwisho, tutarudi kwa kishindo,” amesema akithibitisha kuwakosa Chris Mugalu, Pape Ousmane Sakho, Thadeo Lwanga na Mzamiru Yasin, ambao ni majeruhi.