Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kupanda nafasi ya pili?

Simba Final Train.jpeg Simba kupanda nafasi ya pili?

Sat, 13 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba SC itarejea katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi leo ikiwa itaibuka na ushindi dhidi ya Ihefu katika Uwanja wa Liti, Singida kuanzia saa 10 jioni.

Matokeo ya ushindi yataifanya Simba kufikisha pointi 48 na kuipiku kwa pointi moja, Azam FC ambayo kwa sasa ipo kwenye nafasi hiyo lakini haitoishia kusogea katika nafasi ya pili tu bali pia itapunguza pengo la pointi kati yake na kinara wa msimamo wa ligi, Yanga kubakia pointi nne.

Lakini kama matokeo yatakuwa tofauti na ushindi kwa Simba, furaha zaidi itakuwa kwa Yanga ambayo pengo la pointi baina yao litabaki kuwa kubwa ama pointi saba au sita, jambo ambalo litazidi kuiweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu.

Sare au kupoteza kwa Simba, kutakuwa na faida pia kwa Azam FC kwani itabakia katika nafasi yake ya pili iliyopo sasa lakini ama itaendeleza pengo la pointi mbili lililopo sasa dhidi ya Simba au tofauti ya pointi baina yao kupungua na kubakia moja.

Kwa upande wa wenyeji Ihefu, ushindi katika nmchezo huo utakuwa na maana kubwa kwao kwani utaifanya timu hiyo kufikisha pointi 26 ambazo zitaisogeza hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi kutoka ile ya 11 ambayo ilikuwepo kabla ya mechi ya jana jioni baina ya Mashujaa na Coastal Union.

Timu hizo zinakutana wakati Ihefu ikiwa imetoka kupata matokeo mazuri kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB baada ya kuichapa KMC kwa mabao 3-0 lakini mambo hayakwenda vyema kwa Simba ambayo ilijikuta ikitupwa nje ya mashindano hayo baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti 6-5 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Lakini kwenye ligi, Ihefu imekuwa haina mwenendo mzuri katika siku za hivi karibuni na katika mechi tano zilizopita, imepata ushindi mara moja tu, ikitoka sare moja na kupoteza mechi tatu.

Hali ni tofauti kwa Simba ambayo katika mechi tano zilizopita za ligi, imepata ushindi mara nne na kupoteza mchezo mmoja tu.

Simba katika mchezo wa leo itakuwa na nguvu ya urejeo wa beki Henock Inonga ambaye alikosa mchezo uliopita dhidi ya Mashujaa kwenye Kombe la Shirikisho la CRDB kwa sababu ya matatizo binafsi.

Katika mnchezo wa leo, Simba inapaswa kuwa makini na kiungo mshambuliaji wa Ihefu, Marouf Tchakei kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga na kupiga pasi za mwisho na hadi sasa ameshahusika na mabao 11, akifunga nane na kupiga pasi tatu za mabao.

Ni kama vile Ihefu wanavyotakiwa kuwa makini na kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama ambaye naye amehusika kwa mabao 11 ya timu hiyo kwenye Ligi Kuu, akifunga sita na kupiga pasi za mwisho tano.

Katika mchezo uliopita baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 yaliyopachikwa na Jean Baleke na Moses Phiri huku lile la Ihefu likifungwa na Ismail Mgunda. Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola alisema licha ya ugumu ambao wanajua wataupata kutoka kwa Ihefu, lengo lao kuu ni kupata ushindi.

"Haitokuwa mechi rahisi, ni ngumu. Ni timu ambayo imesajili vizuri na ina kikosi kizuri na imekuwa na matokeo mazuri katika mechi zake ilizocheza.

Sisi kama Simba tunalielewa hilo kwa hiyo tumefanya maandalizi mazuri pamoja na ubora wao na uzuri wao na kuwa na matokeo mazuri katika mechi zao zilizopita kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika mechi yetu.

"Utakuvwa ni mchezo mzuri na wa ushindani. Tunaelewa ugumu wao. Kikosi kiko vizuri kabisa na tuko tayari kwa mchezo. Bado tupo katika nafasi ya kugombea ubingwa," alisema Matola.

Kocha wa Ihefu SC, Mecky Maxime alisema wanaingia katika mechi hiyo wakihitaji ushindi ingawa wanaipa heshimna kubwa Simba.

"Tunajua tuna mchezo mgumu tunacheza na Simba. Kikubwa tunajua kwenye Ligi Kuu bado hatuna matokeo mazuri kwa hiyo pointi tatu ndio sisi hasa tunazitaka. Mashabiki waje kwa wingi kwa vile mchezo utakuwa mzuri.

"Mechi itakuwa ngumu. Kuna wachezaji majeruhi wawili watatu ambao siwezi kuwataja lakini timu ina wachezaji wengi ambao wanaweza kucheza na wako fiti. Itabaki kuwa wazi kuwa Simba ni timu kubwa. Hayo matokeo mabaya ambayo imepata ni ajali kazini kwa hiyo tunajua tunakutana na timu ya namna gani," alisema Maxime.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live