SIMBA leo inashuka dimbani kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa kumenyana na Namungo FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara.
Mabingwa hao watetezi wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kwenda suluhu na Coastal Union ya Tanga mwishoni mwa wiki iliyopita, sawa na Namungo ambayo ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na KMC kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Ilulu.
Simba ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi nane katika mechi nne ilizocheza mpaka sasa sawa na Namungo iliyopo nafasi ya 10 kwenye msimamo na pointi zao tano.
Kocha Mkuu wa Simba Thiery Hitimana alisema maandalizi yao kuelekea mchezo huo yanakwenda vema na anaamini watapata ushindi na kurudisha furaha kwa mashabiki wao ambao hawakupendezwa na matokeo waliyoyapata kwenye mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union.
“Namungo ni timu ambayo nimewahi kuifundisha nawajua vizuri ingawa kuna maingizo mapya ya wachezaji, lakini wengi wao najua uwezo wao, niseme mchezo utakuwa mgumu lakini tumejiandaa kupambana ili kupata ushindi utakaotuliza presha ya mashabiki wetu,” alisema Hitimana.
Kocha huyo alisema, baada ya safu yake ya ushambuliaji kupoteza nafasi nyingi kwenye mechi iliyopita, yeye na wenzake wa benchi la ufundi wameifanyia marekebisho na anaimani wataitumia vizuri kila nafasi watakayoipata kwenye mchezo huo wa leo.
Mshambuliaji Chiriss Mugalu anatarajiwa kurudi dimbani baada ya kukosekana kwenye mechi tatu za ligi kutokana na kupata majeraha kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji na kocha Hitimana alisema mchezaji atakayemkosa ni beki Hennock Inonga kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata juzi kwenye mchezo dhidi ya Coastal.
Kwa upande wake kocha wa Namungo FC, Hemed Seleman ‘Morocco’ alisema wamekuja Dar es Salaam wakiwa na matumaini makubwa ya kuchukua pointi zote tatu mbele ya bingwa mtetezi Simba, kutokana na miamba hiyo siku za karibuni kupoteza ubora wao.
Morocco alisema anajua hautokua mchezo rahisi lakini wamedhamiria kupambana na kupata ushindi kutokana na aina ya wachezaji aliokuwa nao kwenye kikosi chake kuwa na uwezo wa kucheza mechi kubwa na kupata ushindi.
“Nawaheshimu Simba ndio mabingwa watetezi wa ligi yetu lakini pia wanawachezaji wenye uwezo mkubwa lakini hilo halitupi hofu yakufanya tuwaogope tumekuja kamili kwa ajili ya kupambana nao na ninaamini tutapata ushindi mbele ya mashabiki wao,” alisema Morocco.
Baadhi ya wachezaji wanaotarajiwa kuisumbua Simba kwenye safu ya ushambuliaji ni Obrey Chirwa, Shiza Kichuya, Reliant Lusajo na Bigirimana Blaise aliyerejea mechi iliyopita kutoka kwenye majeraha.
Simba ni miongoni mwa timu ambazo hazijapoteza hata mchezo mmoja zaidi ya kupata sare mechi mbili na kushinda michezo miwili na kipa wake Aishi Manula yupo kwenye orodha ya makipa wawili ambao hawajaruhusu nyavu zao kutikiswa na washambuliaji wa timu pinzani mwingine ni Djigui Diarra wa Yanga.