Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally amesema wana vitu vitatu vya kufanya Jumamosi kwenye mchezo wao wa mwisho kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy wakienda na kauli mbiu ya 'Revange of the Warriors' ikiwa na maana ya 'Kisasi cha Mashujaa'.
Akizungumza na wanahabari, Ahmed alisema kwanza wanaenda kulipa kisasi walichofanyiwa na wapinzani wao Oktoba 24, 2021 kwa kuwaondoa hatua ya awali Ligi ya Mabingwa baada ya kuwafunga kwao mabao 2-0 lakini mambo yakageuka kwa Mkapa wakifungwa 3-1.
"Jumamosi Machi mbili tunaenda kulipa kisasi kwa kufuta machungu tuliyosababishiwa na Jwaneng, siku hiyo Rais wetu wa heshima aliumia sana hakuwa na raha siku mbili hivyo ni zamu yao kulipa maumivu yetu tuliyoyapata," alisema.
"Tunakwenda kuwapitisha kwenye tanuri la moto, tunakwenda kulipa kisasi, mechi ya Jumamosi tunakwenda na msemo wa 'Revange of the Warrior' ni vita ya kisasi hii, ni baada ya kuumizwa mwaka 2021," alisema.
Ahmed alisema kitu cha pili ni kwenda kuandika rekodi ya kutinga hatua ya robo fainali kwa mara ya tano katika miaka sita.
"Hatuna hofu yoyote kuelekea mchezo huo kwasababu tuna rekodi nzuri tukifika hatua kama hiyo hasa kwenye uwanja wetu wa nyumbani;
"Tulifanya vizuri nyumbani 2018/19 tulimfunga AS Vita mabao 2-1, 2020/21, tulishinda mabao 4-0 dhidi ya US Gendarmerie, 2021/22 na Horoya alilala mabao 7-0 msimu wa 2022/23 Simba tukatinga robo fainali sasa ni zamu ya Jwaneng Galaxy," alisema.
Ahmed alisema kitu cha tatu ni kupata pointi tatu muhimu ambazo zitachagizwa na wingi wa mashabiki uwanjani huku akitumia nafasi hiyo kuwaita mashabiki kujitokeza kwa wingi.
"Njooni tulipe kisasi tuna timu nzuri hasa tunapofika kwenye hatua kama hii hatunaga jambo dogo, tuna rekodi nzuri kama nilivyosema hapo awali kuwa hatujawahi kutolewa tukifika hatua kama hii, tumezifunga timu nne ndani ya misimu minne mfululizo," alisema.