Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kuja na sera ya usajili

Sera Usajili Simba kuja na sera ya usajili

Sun, 9 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Katika kuhakikisha kwamba Simba SC kuanzia msimu ujao inafanya usajili wake kwa umakini mkubwa ili kutorudia makosa ya nyuma, uongozi wa klabu hiyo umetangaza kuja na sera ya usajili.

Sera hiyo ambayo Simba imepanga kuja nayo, imesema itaifanya kusajili wachezaji wenye sifa za kuitumikia timu hiyo na si kujaza wachezaji wasiokuwa na tija ambao mwisho wanapata shida katika kuvunja mikataba yao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ndani ya Simba ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi klabuni hapo, Dk. Seif Muba, amesema: “Tumeiambia ofisi ya CEO ya Simba itengeneze sera ya usajili ambayo itatumika kusajili wachezaji na kuwaondoa, sera hii itakuwa maalum ambayo tutaitumia wote. Hata ikitokea mimi na wenzangu tukatoka ndani ya uongozi hiyo sera ibaki palepale.”

Katika kukazia hilo, CPA Issa Masoud ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa Fedha Simba na Mjumbe wa Bodi wa klabu hiyo, amesema siyo suala la usajili pekee, pia kamati yoyote hata ile ya usajili ambayo inatajwa kuanzishwa, lazima ifuate utaratibu uliopo.

“Jambo lolote linalofanyika ndani ya Simba ambalo haliendani na katiba yetu hilo haliruhusiwi, tumekuwa tukisikia kwamba kuna Kamati ya Usajili imeanzishwa, huo sio utaratibu.

“Kamati yoyote ndani ya Simba inaundwa na Bodi, nje ya Bodi hiyo kamati hatuitambui. Na tumesema sasa hivi hata usajili utakaofanyika nje ya bodi, huo hatuutambui kwa sababu hatutaki kukiuka utaratibu.

“Kama kuna mchezaji huko atasajiliwa au kocha ataletwa na hajapita katika utaratibu, basi ataenda timu nyingine, hatakuwa ndani ya Simba, hata kama akisajiliwa Cristiano Ronaldo bila ya kupitia kwenye utaratibu wa Bodi atatafuta sehemu ya kuchezea.

“Tumekuwa tukisajili wachezaji wengine wakiwa hawana viwango tunavyovitaka, mwisho wa siku haohao waliomsajili wanakuja kusema mwacheni, akiachwa mchezaji anaacha madeni, klabu imekuwa ikiongezewa madeni yasiyokuwa na vichwa wala miguu. Mwisho wa siku tunatakiwa kufuata utaratibu hata ikitokea kuna deni tunapaswa kulikubali kwani tuliridhia.”

Chanzo: Mwanaspoti