Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kuivaa Platnum

675d8fe42e71c2644c0fa356353149ec Simba kuivaa Platnum

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SIMBA imesonga mbele hatua ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka suluhu dhidi ya Plateau United ya Nigeria katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana.

Kwa matokeo hayo, Simba itakutana na FC Platnum ya Zimbabwe iliyoshinda mchezo wake dhidi ya Costa Do Songo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 4-1. Simba imevuka hatua hiyo kwa faida ya bao 1-0 iliyopata katika mchezo wa kwanza uliochezwa Nigeria ambalo lilifungwa na Clatous Chama.

Nayo FC Platnum katika mchezo wa kwanza ilishinda ugenini kwa mabao 2-1 na jana ikashinda 2-0 ikiwa nyumbani Zimbabwe. Katika mchezo wa jana dakika za awali Simba ilimiliki mpira na kutengeneza nafasi kadhaa kipindi cha kwanza ila wapinzani wao walikuwa makini kulinda lango lao na kuzuia kupenya kiurahisi. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna aliyefumania nyavu za mwenzake.

Kipindi cha pili Plateau walikuja kwa kasi kidogo ambapo dakika tano za awali waliingia eneo la hatari la Simba ila wekundu hao walikuwa makini kuzuia. Baadaye timu zote zikawa zinashambuliana kwa zamu kwa vipindi tofauti na wote wakiingia ndani ya eneo la hatari lakini hakuna aliyeweza kufunga kutokana na umakini wa ulinzi wa kila mmoja.

Dakika za mwishoni Plateau walipata nafasi ya wazi lakini hawakuwa makini kwani wangeweza kusawazisha lakini bahati haikuwa ya kwao na hadi mwamuzi anapulizwa filimbi ya kumaliza mchezo hakuna aliyeona lango la mwenzake.

Katika mchezo mwingine uliochezwa jana wawakilishi wa Zanzibar katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika wameaga mashindano baada ya kufungwa.

Mlandege ambao walikuwa wanacheza Ligi ya Mabingwa wametolewa kwa jumla ya mabao 8-0 na Csfaxien ya Tunisia na KVZ iliyocheza na Al Amal Atbara ya Sudan wameaga kwa jumla ya mabao 4-0.

Katika mchezo wa awali Mlandege walifungwa nyumbani kwa mabao 5-0 na ugenini imefungwa mabao 3-0 na KVZ ugenini ilifungwa bao 1-0 na nyumbani imekubali kipigo cha mabao 3-0.

Wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Namungo FC wanatarajia kucheza leo dhidi ya Al Ratiba kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.

Chanzo: habarileo.co.tz