MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Simba, leo wanashuka dimbani kuikabili Biashara United ya Mara katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Karume, mjini Musoma.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa raundi ya kwanza ya ligi hiyo, ambapo Simba ikiwa nyumbani ilishinda kwa mabao 4-0.
Kwa mujibu wa takwimu, Wekundu hao wa Msimbazi hawajawahi kupoteza mchezo wowote dhidi ya timu hiyo, ambapo katika michezo mitano waliyocheza wameshinda minne na sare moja.
Simba inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 39 kwa michezo 17 ilicheza ya Ligi Kuu msimu huu inapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana na ubora wake iliounesha katika michezo kadhaa iliyopita.
Imetoka kushinda mchezo wa kwanza wa makundi Ligi ya Mabingwa Afrika bao 1-0 dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lakini pia hata kwenye ligi ya ndani katika michezo mitano imeshinda minne na sare moja.
Hata hivyo, Biashara sio timu ya kubeza hasa inapokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani haikubali kufungwa kirahisi.
Takwimu za raundi ya kwanza zinaonesha katika michezo nane ya nyumbani imeshinda mitano, sare mbili na kupoteza mmoja. Pia mzunguko wa pili imecheza michezo miwili na kushinda yote.
Biashara inayoshika nafasi ya nne kwa pointi 32 imetoka kushinda mchezo wake wa ugenini dhidi ya Mwadui mabao 2-1 na kuendelea kuwa katika kiwango kizuri.
Mchezo huo utakuwa ni mzuri na wenye ushindani wa hali ya juu kwa timu zote mbili kila moja ikihitaji kuongeza pointi tatu.
Mchezo mwingine leo utazikutanisha Azam FC dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Timu hizo katika michezo yao iliyopita hazikuwa na matokeo mazuri, Azam ikitoka kufungwa na Coastal Union ya Tanga mabao 2-1 na Mbeya City ikitoka kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga hivyo, ni mchezo mgumu timu zote zikihitaji ushindi.
JKT Tanzania itakutana na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Jamhuri na kila moja inahitaji kushinda ili kujiweka mahali pazuri.
Wakati huohuo, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, wenyeji Dodoma Jiji waliibuka na ushidi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.